Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi.
Na kwenye jumamosi ya ushawishi, tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Kumbe basi, kwenye mauzo na hata maisha kwa ujumla, hupati unachostahili bali kile unachopambania. Na ili upate kile unachotaka kwenye maisha yako, unahitaji ushawishi zaidi ili kupata matokeo unayotaka.
Kwa somo letu la wiki iliyopita, tuliangalia njia ya kwanza ya kuwafanya watu watukubali. Na tuliona asili ya kila binadamu ni kupenda kukubalika na wengine.
Kila mtu anapenda kupendwa ndiyo maana tuko kwenye mahusiano.
Tuliona jinsi gani njia ya kwanza ya kuwafanya watu wengine watukubali ambayo ni wajali wengine kutoka ndani ya moyo wako.
Na tulijifunza somo zuri sana kutoka kwa mbwa ambalo ni kumpenda na kumjali kweli yule anayemfuga na ukaondoka na somo kwamba na wewe unapaswa kuwapenda na kuwajali wateja wako. Kwa sababu kadiri unavyowakubali watu kweli ndivyo nao wanavyokukubali.
Habari njema ni kwamba, katika somo letu la leo tunakwenda kujifunza njia ya pili ya kuwafanya watu wakukubali ambayo ni tabasamu.
Aliyekuwa mkurugenzi wa kiwanda cha chuma na aliyekuwa na mafanikio makubwa Charles Schwab amewahi kunukuliwa akisema, tabasamu lake, lina thamani ya mamilioni ya dola. Ameweza kufanikisha mengi kwa kutabasamu kuliko kununa.

Je, wewe unalitumiaje tabasamu kwenye mchakato mzima wa mauzo?
Je, unakuwa na kisirani na kununa kwa wateja au mara zote unakuwa na uso wa tabasamu?
Kwenye sheria 13 za mauzo, sheria namba 10 inasema, nina hakikisha mara zote ninakuwa na uso wa tabasamu.
Je, wewe mara zote unahakikisha unakuwa na uso wa tabasamu pale unapokuwa na mteja au wale ambao unahusiana nao?
Yaani, ukitoka tu kwenye chumba cha mlango wako ,vaa USO wa tabasamu na kuacha kisirani chako chumbani.
Hata kama kuna watu wamekuudhi na kukukera, unapoenda kuwatumikia wengine onesha kufurahi kukutana na watu ukiwa na uso wa tabasamu na shauku.
Tabasamu ni tendo linalowatangazia wengine kwamba unawakubali, umefurahia kuwaona.
Unafikiri kwa nini tunawapenda mbwa? Kwa sababu wanapotuona huwa wanaruka ruka kabisa, kuashiria wamefurahi kutuona.
Na unafikiri kwa nini watu huwa wanawapenda watoto wadogo?
Kwa sababu, huwa wanatabasamu muda wote.
Sina uhakika kama itakufaa lakini, kama unataka watu wakukubali na kuwa tayari kufanya unachotaka, hakikisha usoni kwako unakuwa na uso wa tabasamu.
Mwanasaikolojia mmoja James V. McConnell aliwahi kunukuliwa akisema, watu wanaotabasamu huwa ni wauzaji, walimu na viongozi wazuri na huwa wanakuza watoto wenye furaha.
Kadiri ya mwanasaikolojia James, na wewe unapaswa kukuza wateja wengi wenye furaha, watu wajisikie tu vizuri kukutana na wewe.
Mwandishi Dale Carnegie anatuambia kwamba, kuna meneja mmoja wa duka la dawa amewahi kusema yuko tayari kuajiri mfanyakazi ambaye hajamaliza shule ila anatabasamu kuliko kuajiri mtu mwenye PhD ambaye hatabasamu.
Tabasamu huwa lina nguvu kubwa, ambayo huwa haionekani. Kwa mfano, unapoongea na simu, hata kama mtu hakuoni, ukiwa na tabasamu anayekusikiliza anapata nguvu ya tabasamu hilo.
Hivyo basi, popote ulipo, kuwa na uso wa tabasamu, ongea na wateja wako kwa tabasamu kwa njia ya ana kwa ana au hata ya kuongea kwa simu utakua na ushawishi mkubwa sana.
Habari njema ni kwamba kila mtu anaweza kuwa na tabasamu. Hata kama kwa asili wewe siyo mtu wa tabasamu bado unaweza kutengeneza tabia hiyo ya kutabasamu.
Unaweza kufanya hivyo kwa kuchagua kufanya kile unachopenda kufanya.
Hatua ya kuchukua leo; jijengee utaratibu huu kila unapotoka nyumbani kwako, rudisha kidevu chako ndani, nyanyua paji lako la uso juu, jaza mapafu yako hewa, furahia hali inayoendelea, wasalimie watu kwa tabasamu na jali kila unayekutana naye.
Usijali wengine watakuchukuliaje, wewe angalia kile unachotaka na siyo watu watakuchukuliaje. Hilo siyo lengo lako la mauzo.
Kwa kufanya hivyo, utawavutia watu wengi ambao watakubaliana na wewe kwenye kile unachotaka.
Kitu kimoja zaidi, wanachina wana usemi unaosema kwamba, mtu asiye na tabasamu hapaswi kufungua biashara ya duka.
Tambua umuhimu wa tabasamu kwa sababu tabasamu lako ni ujumbe wa nia njema na linaangaza maisha ya watu unaokutana nao.
Nenda kauze zaidi kwa kuwa na uso wa tabasamu na utajenga ushawishi na kuimarisha mahusiano na wateja lakini wote unaohusiana nao.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz