3325; Kama siyo lazima.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Kupata matokeo yoyote makubwa kwenye maisha, unahitajika kufanya vitu ambavyo haupo tayari kuvifanya.
Unakuwa haupo tayari kufanya vitu hivyo kwa sababu ya ugumu wake.
Unapokuwa na machaguo mengi ya vitu vya kufanya, huwezi kudumu kwenye kitu ambacho tayari kimeshaonyesha ugumu.
Kwani vingine ambavyo ni mbadala kwako kufanya, vitaonekana ni rahisi kuliko kile unachofanya.
Unaenda kwenye kitu hicho kingine, mwanzoni kinakuwa rahisi.
Lakini baada ya muda nacho kinaanza kuwa na ugumu.
Hapo tena unaona vingine ni rahisi zaidi.
Na kuvutiwa kwenda kwenye hivyo vingine.
Huwezi kujenga mafanikio makubwa kama kila wakati unakimbizana na fursa mpya.
Unapaswa kufanya kitu kimoja kwa muda mrefu na kwa ukubwa wa hali ya juu sana.
Na hilo litawezekana kama tu itakuwa lazima kwako kufanya kile unachopaswa kufanya ili ufanikiwe.
Inapokuwa ni lazima kufanya kitu, huwezi kukitoroka pale mambo yanapokuwa magumu.
Hiyo ni kwa sababu unakuwa hauna namna nyingine yoyote bali kufanya.
Kwa jinsi sisi binadamu tulivyo, kwa asili yetu ya uvivu na kutaka urahisi, kama siyo lazima kufanya kitu, huwa hatujisumbui kukifanya.
Tutatafuta kila aina ya sababu ili tu tusiendelee na kitu hicho.
Unapokuwa unalazimika kufanya vitu fulani, huku ukiwa huna mbadala mwingine, unavifanya na kuvikamilisha vizuri.
Hiyo ni kwa sababu juhudi zako zinaenda kwenye kitu kwa umakini mkubwa na kwa muda mrefu.
Kwenye safari yako ya mafanikio, ni lazima ujiwekee vitu ambavyo ni lazima kwako kufanya.
Kwenye vitu hivyo, huweki nafasi yoyote ile ya majadiliano na wewe mwenyewe. Bali wewe unafanya kama ulivyopanga.
Ukiruhusu tu uwanja wa majadiliano, utajikuta unatumia muda mwingi wa kufikiria na kutetea kila unachoona ni rahisi zaidi kufanya kuliko kufanya kwa uhalisia wake.
Na ili kuhakikisha kweli unalazimika kufanya, unapaswa kuweka mfumo ambao utakuwajibisha pale unapokwepa kufanya yale unayolazimika kufanya.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii bora na ya kipekee tunayoijenga, vitu vya lazima kwa kila mwanachama kufanya ni vingi.
Ni lazima kuielewa na kuiishi falsafa kuu ya jamii hii ambayo ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Ni lazima kuelewa na kuishi misingi mikuu ya jamii hii bila kuivunja. Misingi hiyo ipo mwisho wa makala hii.
Ni lazima kuzingatia vitu vikuu vitatu vya kunufaika na mafunzo, ambavyo ni KUONEKANA, KUWEKA KAZI na KUSIKILIZA.
Unapokuwa ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA unafanya hayo yote kwa lazima, iwe unapenda kufanya au hupendi, unajisikia au hujisikii kufanya.
Ni ufanyaji huo wa lazima ndiyo unamsukuma mtu kwenda zaidi ya mazoea yake na kuweza kufanya makubwa.
Jiwekee mambo ambayo ni lazima ufanye na yafanye kwa lazima bila ya kuruhusu majadiliano na wewe binafsi.
Kwa njia hiyo utaweza kufanya makubwa sana.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe