Kwa walio wengi, wanapofanya makosa, kitu cha kwanza ni kuangalia nani wa kumsingizia makosa hayo. Anatafutwa anayeweza kuwa amechangia kwenye makosa hayo kwa namna yoyote ile.
Akikosa wa kusingiziwa, basi hatua inayofuata ni kutafuta wa kulaumiwa kwa makosa hayo. Mara nyingi hapa huwa anapatikana wa kulaumiwa. Kwa sababu kwenye maisha ya watu huwa kuna watu wapo kwa ajili ya kulaumiwa.
Wanaoongoza kwa kulaumiwa pale maisha ya watu yanapokwenda tofauti na walivyotarajia ni wazazi, serikali na watu wengine wa karibu. Kwa matokeo yoyote ambayo mtu anayapata kwenye maisha, huwa hawezi kukosa kitu cha kuwalaumu wazazi au serikali kwa kuhusika. Watu wengine wa karibu kama ndugu, jamaa na marafiki pia huwa hawawezi kukikwepa kikombe hicho cha lawama.

Kama unataka kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako, lazima ubadili hilo. Ni lazima uchukue hatua za tofauti pale unapofanya makosa au unapopata matokeo ambayo hukuyategemea, bila kujali nani aliyesababisha.
Kinachofuata baada ya kufanya makosa au kupata matokeo ambayo ni tofauti na matarajio ni kumiliki makosa au matokeo hayo kisha kuchukua hatua za kuyabadilisha.
Hupaswi kupoteza muda hata kidogo kwenye kuangalia nani anahusika au wa kulaumiwa. Bali unapaswa kuwajibika wewe mwenyewe, ukijua kwamba chochote kinachokuhusu wewe, ni wewe umechangia kwa asilimia kubwa.
Kwamba hata kama wengine wanaonekana kuhusika, lakini wewe ndiye unayewajibika wa kwanza, kwa sababu wewe ndiye unayekuwa umewaruhusu hao wengine kuweza kufanya kile walichofanya.
Hivyo basi, unachofanya baada ya makosa au matokeo ya tofauti ni kukubali wewe ndiye umesababisha na kuamua kuchuka hatua kubadili hali hiyo. Unachukua hatua kwa kufanya yale yaliyo sahihi na yenye uwezo wa kuleta matokeo ambayo ni kinyume na yaliyopatikana.
Unapokubali kuwajibika kama hivyo, unakuwa mfano mzuri kwa wale wanaokuzunguka ambao wanajifunza na wao kuwajibika. Lakini pia inakujengea heshima kwa wote wanaokuona ukiwa kwenye hali hiyo ya kuwajibika.
Unaaminika zaidi pale unapofanya makosa, ukakubali kuwajibika na kuyabadili makosa hayo, kuliko pale unapowalaumu wengine kwa makosa yaliyotokea, hata kama hao wengine wamehusika. Watu watakufuata wewe kama kiongozi pale wanapokuona hulaumu wala kulalamikia wengine, bali unachukua hatua kuyafanya mambo yawe kama vile unavyotaka wewe.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyotengenezwa kwenye kitu chochote ambacho watu wanafanya, siyo kwa kuwa sahihi mara zote, bali kwa kukosea na kuwajibika.
Wale wanaoshindwa huwa hawana picha sahihi ya safari ya mafanikio, huwa wanadhani ni njia iliyonyooka na isiyokuwa na changamoto zozote. Lakini ukweli ni safari ya mafanikio ni njia yenye kila aina ya vilima na mabonde. Kukosea na kuanguka ni kwa kiasi kikubwa sana. Wanaofanikiwa ni wale wanaoinuka kila wanapoanguka.
SOMA; Kama unataka uhuru kamili wa maisha yako, kuwa tayari kwa hili.
Wanaoshindwa huwa wakishaanguka, wanabaki pale pale na hawanyanyuki tena. Na hata ikitokea wamenyanyuka, huwa wanabadili kabisa safari kwa kuona hawaifai. Kwa bahati mbaya, popote wanapokwenda hali ile ile inajirudia. Watalaumu sana watu, lakini mara zote wanajikuta wakianguka.
Ni sawa na mtu anayejikwaa kwenye jiwe, kisha analilaumu jiwe kwa kumwumiza. Halafu kesho tena anajikwaa kwenye jiwe hilo hilo na kulilaumu linazidi kumuumiza. Keshokutwa tena anajikwaa. Unaweza kusema mtu huyo hayupo makini na maisha yake, lakini hivyo ndivyo wengi wanavyoyaendesha maisha yao.
Inawezekanaje mtu mzima, kwa miaka yote ya maisha yake anawalaumu watu wengine kama ndiyo kikwazo cha wao kufanikiwa? Unaona hiyo imekaa sawa? Kwamba kwa miaka zaidi ya 10 ambayo mtu amekuwa anahangaika, ameshindwa kwa sababu ya wengine. Hapo unaona wazi mtu anajikwaa kwenye jiwe lile lile na hataki kubadilika.
Shika uwajibikaji wa maisha yako, kwa lolote linalotokea kubali wewe ndiye umehusika na chukua hatua ya kuleta matokeo ya tofauti. Hivyo ndivyo unavyoweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Zingatia sana hili, litakuwa na manufaa makubwa kwako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.