Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,

Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi.
Na leo ikiwa ni jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Kwenye somo lililopita tulijifunza jinsi tabasamu lilivyokuwa na nguvu kwenye maisha yetu. Natumaini ulilifanyia kazi somo lile na ulijijengea wa kuwa mtu wa tabasamu muda wote.

Kwenye somo letu la leo, tunakwenda kujifunza njia ya tatu ya kuwafanya watu wakukubali ambayo ni tambua kwamba jina la mtu ndiyo kitu muhimu zaidi kwake.

Mtoto mdogo anapozaliwa wazazi huwa wanahangaika kumtafutia mtoto jina au hata kabla ya kuzaliwa tayari wanakuwa na majina kabisa mawili ya kike na wa kiume.

Hata watu wa karibu, wanaposikia familia fulani imepata mtoto lazima watakuuliza anaitwa nani.
Jina la mtu ndiyo kitu muhimu ambacho mtu tu akizaliwa anapewa na kuanza kuitwa jina hilo anakuwa amelizoea tokea akiwa mdogo kabisa.

Rafiki, Sina uhakika kama itakufaa lakini hakuna sauti ambayo mtu yeyote yule anapenda kuisikia kuliko sauti ya jina lake.

Jina la mtu ndiyo kitu ambacho mtu yeyote anakithamini zaidi, hivyo kama unataka kumfanya mtu akubaliane na wewe, mwite jina lake kwa usahihi.

Kumbuka jina la mtu na kulitamka kwa usahihi inamfanya mtu ajisikie anatambulika na kuthaminiwa.
Ukisahau jina la mtu au kulitamka kwa makosa inamfanya mtu aone  humjali na  hivyo hatakubaliana na wewe.

Mwandishi mmoja Dale anasema kwamba moja ya kitu kilichomwezesha Andrew Carnegie kufanikiwa sana kwenye biashara zake ni tabia ya kukumbuka na kutumia majina ya watu.
Anasema alikuwa na uwezo wa kukumbuka majina ya wafanyakazi wake karibu wote kwenye kiwanda chake.

Watu wanayapenda na kuyathamini majina yao kiasi cha kuwa tayari kuingia gharama kubwa kuhakikisha yanakumbukwa. Kwa mfano matajiri wengi hujitolea kujenga majengo ya umma na ya vyuo kwa sababu majengo hayo yatapewa majina yao.
Wanaona kwamba hiyo ni njia ya kuhakikisha majina yao hayasahauliki.

Watu wamekuwa hawakumbuki majina ya watu kwa kisingizio kwamba ni magumu au hawana kumbukumbu nzuri.
Lakini siyo sababu sahihi, kila kitu kizuri kinahitaji kazi, kadhalika kwenye kukumbuka majina ya watu ni lazima uweke kazi.

Hatua ya kuchukua leo;
1. Jua jinsi ya kutamka jina la mtu kwa usahihi bila kulikosea.

2. Kama unaona unashindwa kulitamka mwambie jina lako linatamkwaje na hata linaandikwaje.

3. Kila unayeongea naye, hakikisha unajua jina lake na jitambulishe wewe unaitwa nani kisha na yeye atasema. Kwa mfano, jina langu ni Deo, je, wewe jina lako ni?

4. Tambua vyeo na wadhifa wa mtu pale unapokuwa unamwita jina lake. Kwa mfano, kama ni Wakili, mwalimu, daktari waite kwa vyeo vyao.

5. Jua jina ambalo mtu anapenda umuite na mwite jina hilo.

6. Jua majina na sura za wateja wako na yatumie majina yao mnapokutana au kuwa kwenye mazungumzo.

Kitu kimoja zaidi, kama unataka kujenga ushawishi na kuimarisha mahusiano yako na watu wengine na wakukubali basi unapaswa kutambua nguvu ya jina la mtu.
Jina la mtu ndiyo kitu pekee ambacho mtu anakimiliki kwenye hii dunia.
Hivyo basi, unapotumia jina lake kwa usahihi anaona unamthamini na atakuwa tayari kukubaliana na wewe.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz