Rafiki yangu mpendwa,
Wewe ulivyo sasa na wewe unayepaswa kuwa kwenye haya maisha, ni watu wawili tofauti kabisa ambao huenda mkikutana mnaweza hata msijuane. Na wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kuhakikisha kadiri unavyokwenda, unafanana na yule unayepaswa kuwa. Yaani pale unapoyamaliza maisha yako hapa duniani, uwe ni pacha wa kufanana na yule unayepaswa kuwa.
Kwa bahati mbaya sana, wengi huwa wanayamaliza maisha yao hapa duniani wakiwa tofauti sana na wale wanaopaswa kuwa. Na hiyo siyo kwa sababu hawakujua wanapaswa kuwa wa aina gani au hawakuweza kuwa. Yote hayo yalikuwa yanawezekana kabisa, lakini walichagua kutokuyafanya.

Nasema walichagua, japo inaweza kuwa ni kwa kutokujua, kwa sababu kikwazo kikubwa kwa wengi kimekuwa ni breki ambazo zimekuwa zinawazuia kutumia uwezo wao mkubwa na kufanya makubwa. Breki hizo zinazuia ule uwezo mkubwa usijidhihirishe na kuleta matokeo ya tofauti.
Hili ndiyo limekuwa linachangia hali ambayo tunaiona kwa wengi, ambapo unakuta mtu anaweka juhudi kubwa sana kwenye yale anayofanya, lakini bado hapati matokeo mazuri. Watu wa aina hiyo wanaweza kuonewa huruma na hata kuonekana kama hawana bahati. Lakini ukweli ni hatuwezi kuona ndani yao na huko ndani ndipo penye mambo yote.
Wengi sana wanaweka juhudi kubwa, lakini pia wana breki ambazo zinazuia juhudi hizo zisilete madhara ambayo yalitegemewa kutokea. Ubaya ni breki hizo ambazo zinawakwamisha watu zipo ndani yao, hivyo hata wakisukumwa kiasi gani kwa nje, bado wanabaki kwenye mkwamo.
Ndiyo maana njia pekee ya watu kutoka popote walipokwama siyo msukumo wa nje, huo tayari unakuwepo, wala siyo msukumo wa ndani ambao pia wengi wanao. Badala yake kinachohitajika ni mtu kuachilia breki ambazo amezishikilia na ndiyo zinazomkwamisha.
Kuna njia nyingi za kuachilia breki ambazo tutaendelea kujifunza kwa kina na kuzifanyia kazi ili kuweza kufanya makubwa. Tumeshajifunza njia ya kufanya tahajudi (meditation) kuachilia breki, ambapo hapa tunazidungua fikra zetu. Njia ya pili tumejifunza kutumia malengo kuachilia breki, ambapo tunaweka malengo sahihi na yanayotufungua maeneo ambayo tumefungika.
Njia nyingine ya kuachilia breki ambayo tunajifunza hapa ni mtu KUJIKUBALI wewe mwenyewe. Unaweza kuchukulia kirahisi neno kujikubali, lakini ni neno lenye nguvu kubwa sana. Kujikubali wewe mwenyewe ni kujiona mtu wa thamani na unayestahili kupata makubwa. Unajikubali kwamba unao uwezo wa kufanya makubwa unayoyataka. Ni katika kujikubali huko ndiyo unaweza kuvuka magumu na changamoto ambazo zimekuwa zinawazuia watu wengi.
Kutokujikubali au kujidharau ni breki ambayo kwa wengi imewazuia wasiweze kufanya makubwa. Kila wanapojaribu kufanya makubwa na kukutana na magumu au changamoto, wanaona hawawezi na hivyo kuacha. Kutokujikubali kunawafanya watu wajione hawana thamani na hawawezi kufanya makubwa kama wengine.
Kwa bahari mbaya sana, hali ya kutokujikubali huwa imejengwa kwa muda mrefu sana, miaka na miaka ya mtu kusikia na kuona matokeo ambayo yanamfanya ashawishike hawezi. Unakuta mtoto tangu akiwa mdogo anaambiwa huwezi au huna akili. Anaambiwa maneno hayo nyumbani, shuleni na kwenye jamii kwa ujumla. Pale anapopata matokeo ambayo siyo mazuri, anaona ni kweli, hawezi na hana akili.
Anakua akiamini hilo na maisha yake yote anakuwa hajikubali wala kujithamini, kitu ambacho kinakuwa breki kwake na kumzuia asiweze kufanya makubwa.
Kuachilia breki kupitia kujikubali kunahitaji mtu ufanye mambo mawili;
Jambo la kwanza ni kurudia zoezi lililojenga kutokujikubali, ambalo ilikuwa ni kuambiwa na kuamini. Kwa sasa unaanza kujiambia wewe mwenyewe kwamba unajikubali na unaweza. Unajiambia kwa kurudia rudia kila mara, huku ukipata taswira ya wewe ukifanya makubwa. Unapata hisia kama tayari umeshapata hayo makubwa. Kwa kurudia rudia ujumbe huo kunakufanya uanze kujikubali.
Jambo la pili ni kutafuta ushindi mdogo mdogo kwenye kila kitu unachofanya. Haijalishi matokeo ya mwisho ya kile unachofanya, wewe angalia ni ushindi gani umepata. Kitendo tu cha kuweza kufanya, tayari ni ushindi tosha. Na kwa kila hatua unayopiga ni ushindi. Ushindi mdogo mdogo unaoupata unakupa ushahidi wa kuzidi kujikubali. Badala ya kuangalia magumu na kukata tamaa, unaangalia ushindi na kupata matumaini ya kuendelea.
Ukifanya hayo mawili kwa kurudia rudia kila siku, utaweza kuachilia breki ambazo zimekuwa kikwazo kwako kufanya makubwa.
Karibu usikilize kipindi cha ONGEA NA KOCHA ili ujifunze kwa kina zaidi kuhusu kuachilia breki kupitia kujikubali.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.