Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Hongereni na karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya mauzo, ambayo yanaendelea kutujenga kifikra na kutupa hatua za kuchukua ili kuendelea kuwa bora sisi wenyewe na kuweza kufanya mauzo makubwa.

Tunachoamini, bila ya shaka yoyote ni kwamba ili kuwa wauzaji bora kuwahi kutokea, lazima kwanza tuwe watu bora sisi wenyewe. Na ili tuwe bora ni lazima tupate maarifa sahihi na kuyaweka kwenye vitendo.

Kwenye somo hili la kutufanya sisi kuwa bora, tunakwenda kujifunza jinsi uwajibikaji unavyoweza kukufanya muuzaji bora na kukupa mafanikio makubwa.

Muuzaji, hivi umewahi kukaa chini na kujihoji wewe mwenyewe kwa nini hufanyi mauzo makubwa kama ambavyo ungepaswa kufanya? Umewahi kujiweka kitimoto wewe mwenyewe na kujikamata hasa ili upate majibu ya uhakika? Hili ni zoezi muhimu sana ambalo wauzaji wengi hawajawahi kupata nafasi ya kulifanya. Unapomaliza somo hili, utakwenda kuweka ratiba ya kufanya zoezi hili kila wiki ili ujiwajibishe, uwe bora, ufanye mauzo makubwa na kupata mafanikio makubwa.

Sababu rahisi kwa nini huuzi kwa ukubwa.

Kwa kipindi ambacho tumekuwa tunafundisha na kufuatilia wauzaji, tumesikia kila aina ya sababu kwa nini watu hawafanyi mauzo kwa ukubwa. Sababu ambazo zimekuwa zinarudiwa mara kwa mara ni hizi;

1. Bei ya bidhaa/huduma tunayouza ni ghali.

2. Wateja hawana hela.

3. Wateja wako mashambani.

4. Siyo msimu mzuri wa biashara.

5. Wateja hawana imani.

Sababu zote hizo, ambazo ni rahisi, zipo kwenye kila biashara na kila muuzaji anazitumia. Japo zinakuwa na ukweli, bado kuna watu wanafanya mauzo licha ya uwepo wa sababu hizo. Ndiyo maana tunaziita sababu rahisi, kwa sababu unaweza kuzitoa kama hutaki kuweka kazi kubwa.

Sababu za kweli kwa nini huuzi kwa ukubwa.

Kuna sababu za ukweli ambazo zimekuwa zinawazuia wauzaji wasifanye mauzo makubwa, lakini hutawasikia wakizitaja. Hawazitaji kwa sababu ukweli unauma. Lakini sasa, hatuwezi kupata mafanikio tunayoyataka kama hatutakuwa tayari kuukabili ukweli. Zifuatazo ni sababu za kweli kwa nini wauzaji wengi hawafanyi mauzo makubwa;

1. Hawaijui biashara yao kwa kina.

2. Hawana shauku kubwa kwenye kila eneo la maisha yao.

3. Hawana vipaumbele sahihi kwenye juhudi wanazoweka, hawaweki kazi ya kutosha au wakiweka kazi inakuwa siyo kwenye vipaumbele sahihi.

4. Hawana ung’ang’anizi, wanakata tamaa haraka wanapokutana na mapingamizi.

5. Hawana malengo makubwa wanayoyapambania kwenye maisha yao, hivyo wanajiendea tu na kuridhika haraka.

Hebu angalia hiyo orodha na uwe mkweli kwako, unakosa sababu zote hizo? Ukiwa mkweli kwako, utaona wapi pa kuanzia ili uwe bora na ufanye mauzo makubwa.

Maana ya uwajibikaji.

Uwajibikaji maana yake ni kujua kwamba matokeo yoyote unayoyapata, wewe ndiye uliyeyasababisha.

Uwajibikaji kwenye mauzo maana yake ni kukubali kwamba pale unaposhindwa kufanya mauzo makubwa, ni wewe ndiye umesababisha. Sababu zote za nje unazojipa, zimekuja tu kumalizia kile ambacho tayari kilishaanzia ndani yako.

Matokeo unayoyapata, kuna namna ambavyo wewe mwenyewe umeyachangia kwa vitu ambavyo umefanya au umeshindwa kufanya. Utaweza kuona mchango wako kwenye matokeo unayoyapata pale unapojihoji na kujipa majibu ya kweli kuhusu wewe na kile unachofanya.

Ili uweze kuwajibika, unapaswa kuacha kulalamika au kulaumu wengine kwa matokeo yoyote unayoyapata. Hata kama kuna mambo mengine ambayo unaona kabisa yamechangia kwenye matokeo uliyopata, usiridhike na kuishia hapo. Badala yake jihoji wewe umechangiaje?

Kitu kimoja unachopaswa kuelewa ni kwamba, kwa sababu hizo hizo ambazo wewe unazo, kuna wenzako wanazo na bado wanauza kuliko wewe. Je wao wana nini mpaka waweze kuuza zaidi na wewe umekosa nini ushindwe kuuza kama wao? Kama hutakaa chini na kujiuliza swali hilo na kujipa majibu sahihi, utaendelea kulalamika na kulaumu na mauzo yako hayatapanda kamwe.

Jiweke kitimoto.

Kama tulivyoona mwanzo wa somo hili, lengo ni utoke hapa na zoezi ambalo litaenda kukufanya uwajibike na kuweza kufanya mauzo makubwa. Wauzaji wote ambao wameweza kufanikiwa, wamekuwa ni watu wa kweli kwao wenyewe. Wanaujua ukweli huo baada ya kujiweka wao wenyewe kitimoto na kujihoji maswali yanayowawezesha kuuona ukweli.

Kila wiki, tenga siku moja ambayo unajifanyia tathmini wewe mwenyewe, ambapo unapitia namba zako za mauzo za wiki nzima. Kisha kwenye kila namba angalia matokeo uliyopata ukilinganisha na lengo ulilonalo. Pale ambapo umefikia lengo jipongeze na kuza lengo hilo.

Na pale ambapo hujafikia lengo, jiulize kwa nini hujafikia hilo lengo? Acha kupokea sababu rahisi zinazokujia, jiulize wewe mwenyewe umechangiaje matokeo uliyopata? Jiulize ni wapi ambapo ‘unazingua’ mpaka matokeo yamekuja vile yamekuja?

Ukijiuliza maswali hayo na kuwa mkweli kwako, utaona wazi maeneo ambayo wewe mwenyewe umejiangusha katika kuyafikia malengo ya namba zako za mauzo.

Hatua baada ya kitimoto.

Hatua za kuchukua baada ya kujiweka kitimoto ni WINGI, UBORA na UPYA.

Wingi ni unatoka na hatua ambazo unaenda kuchukua kwa wingi, kwa sababu moja ya vitu vinavyokuwa vimekukwamisha ni hujafanya kwa wingi.

Ubora ni pale ambapo umeshachukua hatua kwa wingi lakini bado matokeo hayaji kama unavyotaka na hapo inabidi uboreshe namna unavyochukua hatua hizo.

Na upya ni pale unapofanya kwa wingi na ubora, lakini bado hupati matokeo unayotaka, hapo sasa ndiyo unaangalia kipi kipya cha kufanya.

Watu wengi wamekuwa wanaenda kinyume na hilo, wanapokosa matokeo wanayotaka, wanakimbilia kufanya vitu vipya, wakati hata hawajafanya walichokuwa wanafanya kwa wingi. Usikimbilie kufanya vitu vipya kabla hujafanya vile unavyofanya sasa kwa wingi na kwa ubora. Mara nyingi sana matokeo yanakuja baada ya kufanya kwa wingi, hivyo ongeza wingi wa ufanyaji.

Ugumu na urahisi wa mauzo.

Wauzaji wengi wanapojifunza kuhusu uwajibikaji unaohitajika ili wafanikiwe, wanaona ni kazi ngumu sana na ambayo haiwezekani. Hapo kuna ukweli na uongo, ukweli ni ndiyo kazi ni ngumu na uongo ni kwamba haiwezekani, hakuna kisichowezekana.

Ugumu ni sehemu ya maisha na hayupo mtu aliye hai ambaye ameshaweza kutatua kikwazo cha ugumu. Ambacho tumefanikiwa kufanya ni kusogeza tu huo ugumu. Ni labda utaukabili ugumu mwanzoni na mbele mambo yawe rahisi au utafute urahisi sasa hivi na mbeleni mambo yawe magumu.

Mauzo ni kazi rahisi kama utaifanya kwa ugumu na kazi ngumu kama utaifanya kwa urahisi. Hivyo chagua unataka ugumu gani. Unataka ugumu wakati wa kufanya ili upate matokeo kwa urahisi? Au unataka urahisi wakati wa kufanya ila matokeo yawe magumu?

Ukiwajibika, ukichagua ugumu kwenye kutekeleza mchakato wa mauzo unaojifunza, utakuwa bora sana, utayapata matokeo kwa urahisi na kufikia mafanikio makubwa.

Wajibika, uwe bora, ufanye mauzo makubwa na upate mafanikio makubwa pia.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.