Rafiki yangu mpendwa,
Licha ya watu wengi kutaka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao, bado ni kikundi cha watu wachache sana ambao ndiyo huwa wanaweza kupata mafanikio makubwa wanayoyataka. Kundi kubwa la watu wamekuwa wanabaki chini, huku wachache wakiwa kati.
Pamoja na mengi ambayo yanaweza kuwa yanachangia tofauti hizo za watu kwenye mafanikio, kutokutaka lawama imekuwa ni moja ya kikwazo. Ukienda kwenye jamii yoyote ile, ukiwasikiliza masikini wanavyowaongelea matajiri, utapata picha nzuri.
Mara nyingi matajiri wamekuwa wanaonekana ni watu wenye roho mbaya, wasiojali na wanaowanyonya wengine. Hiyo ni kwa sababu matajiri wanaweka mbele kile wanachotaka kabla ya kingine chochote. Hata mambo yao binafsi huwa hawaruhusu yaingilie kile ambacho wanataka.

Kwa kufanya hivyo, wanakuwa wanajua kabisa kwamba wanalaumiwa na wengi, lakini hawajali, kwa sababu hata kwa upande wao wenyewe kuna mengi ambayo wamejinyima. Kwa wale wanaofanikiwa, mafanikio wanayokuwa wanayataka ndiyo yanakuwa kitu pekee kwao, vitu vingine vyote vinabaki kuwa ni usumbufu.
Wanaofanikiwa hawajali sana wengine wanawachukuliaje, wao wanachotaka ni kupata kile wanachokipigania. Wanachohakikisha ni wanafuata sheria na taratibu bila kuzivunja, lakini mengine yote zaidi ya hilo, hawayajali.
Wale wanaoshindwa huwa wanajali sana wengine wanawachukuliaje, hawapendi kulaumiwa. Wanataka kumfurahisha kila mtu, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwenye hii dunia. Katika mahangaiko yao ya kuwaridhisha wengine, wanaishia kujiangusha wao wenyewe, huku pia wakiwa hawajawafurahisha hao wengine.
Kitu kimoja unachotakiwa kukikubali mapema kama umechagua hii safari ya mafanikio ni kwamba huwezi kufanikiwa kama hujapeleka umakini wako wote kwenye kile unachotaka upate mafanikio. Na kitendo cha wewe kupeleka umakini wako wote kwenye kitu unachotaka kufanikiwa, hakitawafurahisha watu wote. Hivyo kuna ambao watakulaumu kwa namna mbalimbali. Huwezi kuacha kupambania ndoto zako kwa sababu kuna watu hawajaridhishwa na hilo. Kama tu huvunji sheria na taratibu, hupaswi kusumbuka sana na wengine wanakufurahiaje.
Hili ni rahisi kusema lakini ni ngumu kutekeleza kwa sababu sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, ambao tunajali sana tunachukuliwaje na wengine. Na hilo ndiyo linalowakwamisha walio wengi. Wewe usikubali kuendelea kukwamishwa na hili. Badala yake amua kwamba utaendea kile unachokitaka na hakuna chochote kitakachoweza kukuzuia kwenye hilo.
Jambo la kushangaza sasa ni pale unapopata matokeo watu wanabadilika. Kama utakuwa umeshindwa, hata wale ambao ulikuwa unawaridhisha wanakudharau na kukuona wewe ni wa kupoteza. Hawatajali kwamba wao walichangia kwenye hilo, kwa kukufanya usipeleke umakini wako kwenye yale muhimu.
Kwa upande wa pili, kama utapata matokeo ya mafanikio makubwa, hata wale ambao walikuwa wanakulaumu kwa kutokujali, watakuwa kwenye kundi la wanaokusifia na kuona wana mchango kwenye mafanikio hayo au wanastahili kunufaika nayo.
Ipo kauli inayosema kushindwa ni yatima wakati mafanikio yana wazazi wengi. Hilo ndiyo linalopaswa kukusukuma ili usijali kabisa wengine wanakulaumu kiasi gani. Kwa sababu unajua ukishindwa, utabaki umesimama mwenyewe. Lakini ukifanikiwa, utakuwa umezungukwa na watu wengi.
Wajibu wako ni mmoja tu, kupata mafanikio makubwa. Na ili upate mafanikio makubwa lazima uwe tayari kulaumiwa na wengine, kwa sababu utaweka umakini wako mkubwa kwenye kile unachofanya kuliko vitu vingine vyovyote. Fanikiwa na mengine yote yatasahaulika.
Wapo wanaojiambia, kuliko niwapuuze watu halafu nikishindwa narudi kwao, bora nijali ili hata nikishindwa wanipokee. Moja, kwa nini ushindwe kama utaweka juhudi zako zote? Ni unapambana mpaka ufanikiwe au utakufa ukiwa unapambana. Na mbili, hakuna anayempokea mtu aliyeshindwa, hata kama amekuwa anaonyesha ushirikiano kiasi gani. Usijidanganye kwa namna yoyote ile, fanikiwa, hiyo ndiyo kinga pekee uliyonayo dhidi ya makwazo ya watu wengine kwenye maisha yako.
Karibu uangalie kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo nimeeleza zaidi dhana hii ya kukubali lawama ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako. angalia, jifunze na nenda kachukue hatua ili uweze kuvuka kikwazo cha kutaka kuwaridhisha wengi ambacho kimekuzuia kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.