Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya uwekezaji, ambayo yanatupa maarifa sahihi kwenye eneo la uwekezaji, kisha tunachukua hatua ya kuwekeza ili kujenga utajiri mkubwa. Huo ndiyo mpango wetu kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU.
Tunaendelea kujifunza kwa kina uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja (Mutual Funds) na tunaiangalia kwa kina mifuko iliyo chini ya UTT AMIS. Mpaka sasa tumeshajifunza mifuko miwili; Umoja na Wekeza Maisha na tumeona jinsi kila mfuko unavyofanya kazi.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza kuhusu mfuko mwingine ambao ni Mfuko wa Watoto. Karibu ujifunze, uelewe na kuchukua hatua sahihi za uwekezaji.
KUKOSEKANA KWA ELIMU YA FEDHA.
Sisi wote tumezaliwa kwenye familia, tumekulia kwenye jamii na tumekaa kwenye mfumo wa elimu kwa vipindi tofauti. Lakini kwenye safari yako yote ya tangu utotoni, ni wapi umewahi kufundishwa kuhusu fedha, utajiri na uwekezaji? Ni wapi ambapo uliwahi kupata kufanya kwa vitendo uwekezaji wakati ukiwa mtoto?
Kwa wengi wetu, kitu pekee tulichojifunza kuhusu fedha tukiwa watoto ni kwamba hazipo za kutosha. Kila ulipokuwa na mahitaji fulani na kumtaka mzazi wako akutimizie, uliambiwa hela hakuna. Kwa hiyo hilo ndiyo somo ambalo wengi tunakua nalo, kuanzia kwenye familia, jamii na hata kwenye elimu.
Kwa miaka yote ambayo tumekaa shuleni, tumefundishwa mambo mengi, mengi tumeshayasahau sasa. Tumefundishwa jografia za maeneo ambayo hatutakuja kufika, tukakariri historia za miaka mingi iliyopita na kujifunza kanuni za hisabati ambazo sasa hatuna matumizi nazo kwenye maisha. Lakini kitu kimoja ambacho kinatuhangaisha kila siku, kinatufanya tuwahi kuamka na kuchelewa kulala, hatukupata nafasi ya kufundishwa kwa kina. Kitu hicho ni fedha.
Tuna mengi ya kueleza juu ya ukosefu wa elimu ya fedha na hivyo kutukwamisha. Lakini hebu pia tujiulize, nini cha tofauti ambacho tunafanya kwa watoto wetu? Kama sisi tulikosa elimu ya fedha na hivyo kupata changamoto nyingi, je tunahakikishaje watoto wetu nao hawapiti huko?
Bado familia zipo vile vile kwenye eneo la fedha, jamii pia zipo vile vile na mfumo wa elimu haujabadilika. Lakini kwa mzazi mmoja mmoja, ambaye ana kiu ya mafanikio yake na familia yake, hupaswi kuacha watoto wako wakapitia yale ambayo umepitia wewe.
Kwa bahati nzuri sana, sasa kuna fursa nyingi za kuwapa watoto elimu na kuwawezesha kuchukua hatua kwa vitendo kwenye kujifunza fedha na uwekezaji. Zipo fursa za akaunti za watoto kwenye mabenki mbalimbali kama sehemu ya kuweka akiba. Halafu ipo fursa ya uwekezaji kupitia mfumo wa watoto wa UTT, ambao tunakwenda kujifunza kwa kina hapa.

MFUKO WA WATOTO WA UTT AMIS.
Mfuko wa Watoto ni mfuko wa tatu kuanzishwa na UTT AMIS mnamo tarehe 1 Octoba, 2008. UTT AMIS inatambua umuhimu wa mtoto katika maendeleo ya taifa siku zijazo. Kwa sababu hiyo, mfuko wa watoto (Watoto Fund) ulizinduliwa. Mfuko wa watoto ni suluhisho la kifedha kupitia uwekezaji ambalo linalenga katika kukuza mtaji kwa faida ya muda mrefu kwa ajili ya maendeleo ya watoto wetu wapendwa.
MALENGO YA MFUKO
Mfuko wa watoto ni mfuko wa wazi unaowafaa wawekezaji wenye lengo la kukuza mtaji kupitia kuwekeza pesa kwenye hisa zilizoorodheshwa na maeneo yenye mapato ya kudumu. Kila mzazi/Mlezi angependa mwanae;
1. Awe na furaha ya kudumu.
2. Awe na hisia nzuri katika maisha yake.
3. Apate kazi bora na nzuri.
4. Aweze kujitegemea kutokana na kipato chake.
Jibu la maswali hayo ni moja tu; wekeza katika mfuko wa watoto
Mfuko una aina mbili za uwekezaji:
1. Kulipia ada za masomo – Mpango huu ni kwa ajili ya malipo ya ada ya masomo ya mtoto.
2. Kukuza mtaji – Mpango huu ni wa kukuza mtaji wa mtoto ambae ndiye mwekezaji.
NANI ANARUHUSIWA KUWEKEZA:
1. Mzazi/Mlezi kwa jina la mtoto ambaye yupo chini ya umri wa miaka 18.
2. Taasisi, kampuni na vikundi vinaweza kuwawekezea watoto kama sehemu ya huduma kwa jamii.
UKWASI/KUUZA VIPANDE
Mwekezaji anaweza kuuza vipande vyote au baadhi ya vipande baada ya mtoto kutimiza umri wa miaka 12. Malipo ya mauzo ya vipande yatashughulikiwa ndani ya 10 za kazi baada ya kupokelewa.
SIFA ZA MFUKO
1. Uwekezaji unafanywa kwa jina la mtoto aliye chini ya miaka 18.
2. Mfuko unaruhusu umiliki wa mtu binafsi tu.
3. Kiwango cha chini cha uwekezaji ni TZS. 10,000.
4. Kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza ni TZS. 5,000.
5. Hakuna kiwango cha juu cha uwekezaji.
6. Vipande vinauzwa kwa thamani halisi ya wakati huo [hakuna gharama za kujiunga].
Gharama za kutoka;
(a) 1% ya thamani ya kipande kwa uwekezaji uliodumu kwa kipindi kisichozidi miaka 3.
(b) Hakuna gharama za kutoka endapo uwekezaji utadumu zaidi ya miaka 3.
Mfuko una mipango miwili ya uwekezaji kama ifuatavyo:
1. Mpango wa malipo ya ada ya masomo (scholarship option) –
Malipo ya ada yatalipwa kwa awamu mbili, kila nusu mwaka au kila mwaka kwa ajili ya mtoto, baada ya kufikisha umri wa miaka 12. Madhumuni ya kupokea malipo haya ni kukidhi gharama za ada ya shule ya sekondari au elimu ya juu.
2. Mpango wa kukuza mtaji (growth option) – Mwekezaji hatapata malipo ya mara kwa mara na badala yake mwekezaji atafaidika na ukuaji wa mtaji unaotokana na kukua kwa thamani halisi ya kipande.
(a). Mwekezaji anaruhusiwa kuuzaa vipande vyake pindi mtoto anapofikisha umri wa miaka 12.
(b). Mfuko unaruhusu uhamishaji wa vipande kutoka mwekezaji mmoja kwenda mwekezaji mwingine.
(c). Mwekezaji akifariki, mrithi ataruhusiwa kuendeleza uwekezaji huo.
(d). Vipande vinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo katika taasisi za fedha.
(e). Kupevuka kwa mpango wa mwekezaji (Ukomo).
Ingawa mfuko ni endelevu (hauna ukomo), uwekezaji kwa mtoto mnufaika utafikia ukomo pindi atakapotimiza umri wa miaka 24. Uwekezaji huo unapopevuka kila mwenye vipande ana uhuru wa kuchagua kati ya mambo yafuatayo:
a) Kudai thamani ya vipande vyake kwenye mfuko kwa thamani ya wakati huo.
b) Kuwekeza tena kwa kupitia mtoto mbadala (mwenye umri chini ya miaka 18),
c) Kuhamishia vipande vyake kwenye mfuko mwingine wowote unaoendeshwa na UTT AMIS.
KIGEZO CHA UFANISI
Mfuko umekuwa na ukuaji mzuri kwa kipindi chote ambacho umekuwepo na hivyo kuongeza thamani kwenye uwekezaji ambao umefanyika.
MJADALA WA SOMO.
Kupitia yale uliyojifunza kwenye somo hili, karibu ushirikishe mrejesho wako kwa kujibu maswali yafuatayo.
1. Kabla hujafika umri ambapo ulianza kujitegemea kwa kuingiza kipato, je uliwahi kupata elimu yoyote kuhusu fedha, utajiri na uwekezaji? Kama ndiyo ilikuwa elimu gani? Na kama siyo, unafikiri ungepata elimu hiyo ingeleta mabadiliko gani kwenye maisha yako?
2. Kama una watoto ni hatua zipi ambazo umekuwa unachukua ili kuwapa elimu ya fedha, utajiri na uwekezaji? Kama bado hujawa na watoto, umejipangaje pale utakapowapata wapate elimu hiyo adimu ambayo wewe uliikosa?
3. Kama una watoto, je umeshawafundisha kwa vitendo kuchukua hatua kwenye eneo la fedha, kama kuwa na akaunti za benki, kuwekeza mfuko wa watoto UTT? Kama ndiyo shirikisha namna gani umefanya, kama siyo shirikisha hatua zipi unazoenda kuchukua baada ya somo hili. Kama huna watoto shirikisha mpango wako kwenye kuwafundisha kwa vitendo watoto utakaowapata.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya mrejesho wa somo hili la uwekezaji ambalo tumelipata.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.