Wauzaji bora kuwahi kutokea, karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya kuendelea kutufanya kuwa bora na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Tunaendelea kupata masomo ya usakaji ili kupata wateja wengi zaidi kwenye biashara na kuwafuatilia kwa karibu. Mambo hayo mawili yana nguvu kubwa ya kukuza mauzo kwenye biashara yoyote, pale yanapofanyika kwa ukubwa na msimamo.
Kuwafikia wateja kwa njia ya kuongea na simu tumeiona kuwa njia yenye matokeo makubwa. Hiyo ni kwa sababu kupitia upigaji wa simu unaweza kuwafikia wateja wengi kwa muda mfupi kuliko kutembelea.
Lakini ili zoezi la kuwafikia wateja kwa simu liwe na tija, lazima lifanyike kwa ukubwa na kwa kurudia rudia bila kukata tamaa. Kulingana na hali ya wateja, kama ni wa baridi, vuguvugu au wa moto, utahitajika kuwasiliana na wateja kwa muda mrefu mpaka uweze kukubalika.

Hilo hitaji la kuwasiliana na wateja kwa muda mrefu ndiyo uweze kujenga ushawishi ndiyo limewakwamisha wengi. Wengi wamekuwa wanakata tamaa haraka pale wanapoona wanapiga simu kwa wateja na hawauzi. Wanachokuwa hawajui ni kwamba hawapaswi kuacha, kwani kwa kuendelea wanazidi kujenga ushawishi na kuaminika na wateja.
Ili kuhakikisha unalifanya zoezi la upigaji simu kuwa la tija na kutokukata tamaa pale matokeo yanapochelewa, unapaswa kulipangilia vizuri. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kupangilia upigaji wako wa simu ili uwe na tija na uweze kufanya mauzo makubwa zaidi.
Karibu ujifunze, ukayaweke haya unayojifunza kwenye matendo na kuweza kupata matokeo makubwa na ya tofauti.
Moja; Tenga Muda Wa Kupiga Simu.
Kitu cha kwanza unachopaswa kupangilia kwenye zoezi la kupiga simu ni muda. Unapaswa kutenga muda maalumu kwa ajili ya kupiga simu kwenye siku yako ya mauzo. Hata kama unafanya zoezi hilo siku nzima, lazima upange muda kabisa.
Wengi wamekuwa wanashindwa kupiga simu kwa wingi kwa kusingizia kwamba hawana muda. Lakini ukweli ni kila mtu ana muda, wanachoshindwa ni kupangilia vizuri muda wa kupiga simu.
Kufanya jukumu lolote bila ya muda maalumu, unakuwa na ufanisi mdogo. Hiyo ni kwa sababu unaweza kuona muda unao mwingi, halafu ghafla unakuja kushtuka muda umeisha.
Kwenye kila siku yako ya mauzo, pangilia muda wa kupiga simu na kisha fanya zoezi la kupiga simu tu kwenye huo muda.
Muda mzuri wa kupiga simu kwa wateja ni asubuhi, pale muda wa kazi unapoanza, kuanzia saa mbili mpaka saa nne. Huo muda ni rahisi kuwapata wateja wengi na hata kuwashawishi kwa sababu wanakuwa hawajafanya maamuzi mengi kwenye siku zao.
Hivyo kwa kila muuzaji, masaa mawili ya kwanza kwenye siku ya mauzo yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya kupiga simu tu na siyo kingine chochote. Kuanzia saa mbili kamili asubuhi mpaka saa nne kamili asubuhi, au kuendelea, unapaswa kuwa muda wa kupiga simu tu.
Kwa wastani, muuzaji aliyejipanga vizuri, anaweza kupiga simu zisizopungua 10 ndani ya nusu saa. Hivyo kwa saa moja ni simu 20 na kwa masaa mawili simu zisizopungua 40.
Kwa muuzaji yeyote yule, ambaye yupo kwenye CHUO CHA MAUZO, anapaswa kutenga siyo chini ya masaa mawili kwenye siku yake ya mauzo kwa zoezi la kupiga simu tu. Hapo ni kama ana majukumu mengine kama ya kuwahudumia wateja n.k. Lakini kama ni msakaji au mkamilishaji, siku nzima ya mauzo, ambayo siyo chini ya masaa 9, inatakiwa kuwa ya kuongea na wateja, ana kwa ana au simu.
Baada ya kutenga muda wa asubuhi, unatenga pia muda wa mchana na muda wa jioni kwa ajili ya zoezi la kupiga simu kwa wateja. Kwenye ratiba yako ya kila siku, tenga kabisa muda wa kupiga simu na kwenye muda huo fanya zoezi hilo la kupiga simu tu.
SOMA; Usakaji Wa Wateja Kwa Kupiga Simu.
Mbili; Wagawe Wateja Kulingana Na Hali Zao.
Kabla ya kupiga simu, wagawe wateja wako kulingana na hali zao. Tumeona kwenye kuwapigia wateja simu, wanagawanyika kwenye makundi matatu; wateja baridi – ambao hawakujui, vuguvugu – ambao wamewahi kukusikia na wa moto – ambao wana msukumo wa kuchukua hatua.
Wateja wa baridi unapaswa kuwapanga wengi kwenye orodha yako ya kuwasiliana nao, kwa sababu hao wengi hutawapata na hata ukiwapata mazungumzo hayatakuwa ya muda mrefu. Unachotaka kwa hawa wateja ni wajue upo na waendelee kukuzoea ili wawe vuguvugu na baadaye moto na uweze kuwauzia.
Wateja vuguvugu pia wanapaswa kuwa wengi ili uwasogeze karibu na manunuzi. Na wateja wa moto, unakuwa nao wa kutosha kulingana na muda wako na mahitaji yao ili uweze kuwapa muda wa kutosha kuzungumza nao. Kwa idadi ya wateja unaopanga kuwapigia, wagawe kwenye theluthi tatu kulingana na hali zao.
Tatu; Andaa Orodha Ya Wateja Utakaowapigia Mapema.
Hakuna kitu ambacho kimekuwa kinapoteza muda wa kupiga simu kama kutafuta wateja wa kuwapigia simu kwenye muda ambao ndiyo umepanga kupiga simu. Na hivyo ndivyo wauzaji wengi wanavyofanya. Ule muda ambao wamepanga kupiga simu, ndiyo wanaanza kutafuta kwenye simu zao wampigie mteja gani. Matokeo yake ni kati ya simu moja na simu nyingine muda mwingi unapotea. Pia kunakuwa na sababu nyingi za kwa nini baadhi wasipigiwe.
Kuokoa muda na kuongeza ufanisi kwenye zoezi la simu, andaa orodha ya wateja utakaowapigia mapema kabla ya muda wa kupigia wateja. Hilo unapaswa kulifanya siku moja kabla, au asubuhi na mapema kabla ya muda wa kazi kuanza. Unapoandaa orodha ya wateja anza na waliotoa ahadi ambao ahadi zao zimefikia, kisha nenda kwa wale ambao hawajafikiwa kwa muda mrefu na malizia kwa waliofikiwa karibuni.
Hakikisha kwa wateja wote unaowafuatilia, unaongea nao kwa simu angalau mara moja kila wiki. Hivyo hakikisha unawagawa vizuri wateja kwenye siku na muda wako wa kupiga simu ili uweze kuwa na ufanisi mzuri.
Nne; Kuwa Na Hatua Ya Mteja Kuchukua.
Unapopiga simu kwa wateja, kuwa kabisa umejipanga nini unakwenda kuongea na hatua gani unataka mteja achukue. Usiwapigie simu wateja kama unawapigia jamaa zako, kwamba mpige soga tu. Japo unaweza kumfanya mteja aone hivyo, lakini wewe una lengo.
Kwanza kabisa kuwa na skripti ambayo unaifuata wakati wa mazungumzo ya simu na wateja. Hiyo inafanya mazungumzo yako kuwa na mpangilio mzuri mara zote na kuwa na ushawishi zaidi.
Kisha kuwa na hatua ambayo unataka mteja achukue kwenye mwisho wa mazungumzo hayo. Hatua ya kwanza ni akubali kununua, hivyo utapanga namna ya kumpeleka kwenye hilo. Kama hiyo itashindikana kabisa basi akupe ahadi ya lini atachukua hatua, ili uweze kumfuatilia kwenye ahadi hiyo. Usikubali kumaliza mazungumzo ya simu na mteja bila manunuzi au ahadi, kwa sababu utakuwa na wakati mgumu kumfuatilia tena baada ya hapo.
Kuna malengo mengine unayoweza kuwa nayo, kama kupata taarifa zaidi, kupata wateja wa rufaa na kadhalika. Muhimu ni uanze mazungumzo ukiwa na malengo kabisa, ili pamoja na yote, uhakikishe kuna kitu unapata.
Tano; Wasiopatikana, Wasiopokea Na Wanaokata Simu.
Malalamiko ya wauzaji wengi kwenye zoezi la kupiga simu ni wateja wengi hawapatikani, wakipatikana hawapokei simu na hata wakipokea simu wanakata.
Muuzaji, hebu pata picha umekutana na bondia ambaye anakuambia amechoshwa na kazi yake ya ubondia. Unamuuliza tatizo ni nini, anakuambia anapigwa sana ngumi. Au mchezaji wa mpira anakuambia anachoshwa na kazi yake kwa sababu anapigwa chenga na kufungwa magoli.
Unajua kabisa hayo hayatokei, kwa sababu wote wanajua ni sehemu ya mchezo. Sasa kwa nini wewe unataka simu zako zote zipatikane, zipokelewe au kusikilizwa? Simu kutokupatikana, kutokupokelewa au kukatwa ni sehemu ya mchezo. Siyo kwa sababu yako, bali ndivyo hali ilivyo na kila muuzaji anakutana na hali hiyo.
Ili kufuka hiyo hali na kuendelea na zoezi ili ufanye mauzo makubwa zaidi, fanya hivi;
Simu isipopatikana, jaribu kupiga mara ya pili, isipopatikana tena endelea kupiga simu nyingine na utajaribu tena baadaye ukiwa umemaliza orodha ya siku. Isipopatikana utapeleka namna hiyo kwenye siku nyingine, huku ukijihakikishia ni sahihi.
Simu isipopokelewa, usirudie kupiga hapo hapo, endelea na simu nyingine na utakuja kupiga tena mwishoni baada ya kumaliza orodha yako. kama bado haitapokelewa, tuma ujumbe ukimsalimia mteja na kumtaja kwa jina na kumwambia una habari njema kwake. Kama bado hatajibu, mweke kwenye orodha ya kumpigia tena wiki inayofuata.
Mteja anayepokea simu na kukata baada ya kukusikia, mpelekee ujumbe, msalimie kwa kumtaja jina lake na mwambie una habari njema kwake. Na kama amekuwa anarudia hivyo, mpelekee ujumbe mkali zaidi ukimwambia; “Ungejua kitu kizuri ninachotaka kukuambia, usingekata simu.” Hapo hakikisha kweli una habari njema za kuwapa wateja wako.
Kwa vyovyote vile, wateja ambao hujawapata kwenye zoezi la kupiga simu, waweke kwenye ratiba ya siku nyingine, angalau wiki moja baadaye. Kisha nenda kwa mpango huo bila kuacha, iwe wamenunua au hawajanunua.
Ili zoezi la upigaji simu liende vizuri, unapaswa kuwa na orodha kubwa ya wateja unaowafuatilia. Kwa wastani kila muuzaji aliyepo kwenye chuo cha mauzo anapaswa kuwa na wateja kamili wasiopungua 100 (mia moja) na wateja tarajiwa wasiopungua 1000 (elfu moja). Kwa idadi hiyo kubwa ya wateja, utakuwa na kazi kubwa ya kufanya na lazima utapata matokeo mazuri.
Pangilia vizuri upigaji wako wa simu kama ulivyojifunza hapa na utaweza kujenga kuzoeleka na wateja, kuaminika na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.