3332; Utajua kwa kufanya.

Kutoka mezani kwa Kocha.

Rafiki yangu mpendwa,
Vitu vingi sana kwenye maisha yako, utaweza kuvijua na hata kuvitumia vizuri, kama utavifanya.

Utaweza kujua ni mbali kiasi gani unaweza kwenda, kama utaenda mbali zaidi.

Utaweza kujua uko imara kiasi gani kukabiliana na magumu, kama utakutana na magumu zaidi.

Mara zote tunapokutana na kitu kipya, huwa tunachukua moja kati ya pande hizi mbili.
Moja ni tunaona ni kitu rahisi sana na hatuwezi kukishindwa. Tunaona hatuna hata haja ya kuhangaika nacho sana kwa kuwa ni rahisi.
Mbili ni tunaona ni kitu kigumu sana na kisichowezekana kabisa. Tunaona hakuna hata haja ya kuhangaika nacho kwa sababu hakuna kitu tunaweza kufanya.

Mara nyingi, ukweli huwa unakuwa katikati ya hali hizo mbili, yaani siyo rahisi sana na siyo ngumu kwamba haiwezekani.
Lakini hilo utalijua kama utafanya.
Maana ni kupitia kufanya ndiyo matokeo yatajidhihirisha yenyewe.

Watu wengi wamejikwamisha kufanya makubwa kwenye maisha yao kwa kukimbilia kwenye moja ya hali hizo mbili kabla hata ya kufanya chochote.
Wewe usiwe hivyo, sema baada ya kufanya, maana hapo ndipo unapokuwa na uhakika wa unachokisema.

Chochote unachosema kabla ya kufanya siyo sahihi. Ni mpaka ufanye ndiyo unaweza kuwa na majibu sahihi juu ya  kitu chochote kile.
Kusema ni rahisi kabla hujafanya, kunakuwa na mengi ambayo hujayazingatia, utakuwa na matumaini hewa.
Kusema haiwezekani kabla hujafanya, kuna fursa nzuri unakuwa hujaziona na hivyo unakata tamaa haraka.

Unaweza kuwa na maoni yako kuhusu kitu chochote kile, lakini usiyatoe maoni hayo kabla hujafanya kitu hicho.
Utajifunza mengi sana kwa kufanya kuliko kuongea tu.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, hatusemi kitu kabla ya kufanya.
Tunaamini kwenye kufanya kabla ya kusema, kwa sababu maneno ni rahisi ila vitendo vinahitaji juhudi.

Ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA huna haki ya kukizungumzia kitu kama hujakifanya.
Na hata ukikifanya, bado matokeo unayoyapata siyo ndiyo mwisho.
Bali pia utaangalia na historia ya wengine ambao tayari wameshafanya na kupata matokeo mazuri.

Kuchagua kuwa ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni kuchagua ufanyaji kabla ya usemaji.
Ni kuchagua kufikiri wewe mwenyewe badala ya kufuata mkumbo.
Ni kujitoa hasa kuwa bora kila wakati badala ya kubaki kwenye mazoea yanayowameza wengi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe