Rafiki yangu mpendwa,
Ushindi huwa hauamuliwi kwenye uwanja wa mapambano, bali kabla ya mashindano yenyewe. Timu inaenda uwanjani ikiwa inajua kabisa kama itashinda au itashindwa. Kinachokuwa kimebaki ni kutangazwa tu.
Unafikiri kwa nini kwenye kila mchezo baina ya timu mbili, kila timu inayoshinda inakuwa na sababu za kushinda na kila timu inayoshindwa pia inakuwa na sababu za kushindwa? Kwa sababu timu hizo zinaingia uwanjani tayari zikiwa na sababu za kushinda na za kushindwa.
Timu inayoshinda ni ile ambayo ina sababu nyingi za kushinda kuliko za kushindwa na kuliko za kushinda za mshindani wake. Unaweza kuelezea mengi kuhusu michezo, lakini hiyo ndiyo saikolojia ya ushindi, ambayo ipo kwenye mambo yote.

Saikolojia hiyo ya ushindi pia ipo kwenye mafanikio. Mafanikio ambayo mtu anayapata kwenye kitu chochote anachofanya, hayaanzii kwenye hicho anachofanya, bali yanaanzia ndani yake kwanza. Unaweza kulidhihirisha hilo kwa sababu unaweza kukuta watu wawili, wanafanya kazi au biashara ya aina moja, walianzia ngazi moja na muda mmoja, lakini baada ya muda mmoja anakuwa amefanikiwa na mwingine ameshindwa. Unawezaje kuelezea hilo kama siyo kwa ushindi kuanzia ndani ya mtu?
Ni kwa misingi hiyo ndiyo tunaweza kuona nini kinawafanya watu kushinda na kushindwa. Na kama huwezi kujua yanayowafanya watu kushindwa, ukijua yanayowafanya kushindwa na ukayaepuka, utapata ushindi.
Kuna dalili tatu ambazo zimekuwa zinaonekana sana kwa watu wote ambao huwa wanaishia kushindwa. Dalili hizo zinaweza kuonekana ni kitu cha kawaida, lakini zimekuwa na nguvu kubwa sana.
Moja ya dalili hizo ni kuwa na mpango mbadala pale mpango mkuu unaposhindwa. Yaani mtu anakuwa na mpango wake mkuu wa mafanikio, lakini pia anakuwa na mpango mbadala kama ule mpango mkuu utashindwa. Hii ni fikra inayoonekana ni nzuri, kwamba kama utashindwa, basi uwe na mahali pa kuanzia.
Sasa hebu niambie ukweli rafiki yangu, kama una mpango mbadala, nini kitakachotokea? Pale utakapokutana tu na ugumu kwenye mpango wako mkuu, kwa haraka sana utakimbilia kwenye mpango huo mbadala. Kwa bahati mbaya sana, hakuna mpango ambao huwa unaenda kama ambavyo mtu amepanga. Kila mpango huwa unakutana na changamoto na vikwazo mbalimbali. Kama mtu ana mpango mbadala, atakata tamaa haraka kwenye mpango wake mkuu pale anapokutana na vikwazo na changamoto.
Hivyo basi rafiki, kama kweli unataka kupata mafanikio kwenye kitu chochote kile, unapaswa kuwa na mpango mmoja tu. Na kisha kupambana na mpango huo mmoja mpaka ukupe matokeo ambayo unayataka. Ukikutana na magumu au changamoto zozote, unavuka zote na kupambana mpaka upate unachotaka. Achana kabisa na mpango wowote mbadala unaoweza kuwa nao, kwa sababu huo utakutorosha kwenye mpango wako mkuu.
Unaweza kuona huu ni ushauri mkali na unaoweza kukupoteza, hasa kwenye hizi zama ambazo hatari ni nyingi na ushindani ni mkali. Lakini ninachotaka kukuambia huu ni ushauri sahihi kwa wale wanaotaka kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Kwa sababu hakuna njia nyingine ya kujenga mafanikio makubwa kwenye zama hizi zenye changamoto nyingi.
Kuwa na mpango mmoja ambao unapambana nao mpaka ufanikiwe pia ni dalili ya mtu kujiamini kwenye kile ambacho unataka. Huonekani kuwa mtu unayebahatisha, hivyo hata wengine wanaotaka kushindana na wewe, lazima wajipange sana. Kwa namna unavyokuwa na msukumo mkubwa kwenye hicho unachofanya, unawafanya wengi wakuhofie.
Rafiki, hii ni dalili moja, ambayo kama umesoma kwa kina hapa, umeshaona kwa nini wewe mwenyewe unajikwamisha kufanikiwa. Dalili nyingine mbili nimezielezea vizuri sana kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kipo hapo chini. Angalia kipindi hicho, zielewe dalili hizo na uzifute mara moja kwenye maisha yako ili uweze kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.