Rafiki yangu mpendwa,
Mauzo ndiyo moyo wa biashara, kama ambavyo mwili hauwezi kuwa na uhai bila mapigo ya moyo, ndivyo pia biashara haiwezi kuwa na uhai kama hakuna mauzo.
Lakini jambo la kushangaza ni kwamba watu wengi waliopo kwenye biashara huwa hawayapi mauzo uzito wa kutosha. Huwa wanadhani mauzo ni kitu kitakachotokea tu, wakati ni kitu kinachotakiwa kufanyiwa kazi.
Kwa hakika, jukumu la kwanza la kila mwanzilishi na kiongozi wa biashara ni mauzo. Katika kugawanya muda na rasilimali zake, asilimia 80 inapaswa kuwekwa kwenye mauzo na asilimia 20 kwenye mambo mengine yote.

Kuna biashara nyingi ambazo huwa zipo sokoni, lakini hazina ukuaji mzuri. Kwa muda mrefu zinakuwa zimedumaa kwenye ngazi ile ile ambayo zimefikia. Mauzo yanakuwa ni ya kupanda na kushuka wakati huo.
Mara nyingi hizi zinakuwa ni biashara zenye uwezo wa kufanya makubwa, lakini zinakuwa zimekwama kwenye hilo eneo la mauzo.
Kuna mambo mengi yanayozikwamisha biashara kwenye kudumaa kwa mauzo, lakini moja ambalo limekuwa ni kubwa ni utegemezi kwenye mauzo rahisi.
Wafanyabiashara wengi, kwa kukosa uelewa na pia kuwa na uvivu, huwa wanahangaika kupata mauzo ambayo ni rahisi na yasiyowataka kufanya kazi. Na kweli huwa wanayapata mauzo hayo rahisi, lakini huwa yanakuwa mkwamo mkubwa kwenye ukuaji.
Pale biashara inapopata mauzo rahisi, huwa yanafanya biashara iwe ngumu sana kuendesha. Wateja rahisi kuwapata huwa wanakuwa siyo wenye uwezo wa kumudu kufanya manunuzi makubwa. Wanakuwa ni wateja wanaoangalia bei rahisi, wanaotaka punguzo, wanaokopa na wagumu kulipa.
Wateja wa aina hiyo wanapatikana kirahisi sana, lakini kuwahudumia huwa ni kazi ngumu, wanatumia rasilimali nyingi za biashara huku faida wanayoingiza ikiwa kidogo au hakuna kabisa.
Ili kupata mauzo makubwa na ambayo yataiwezesha biashara kuwa na ukuaji mkubwa, mauzo hayo yanapaswa kufanyiwa kazi tangu mwanzo. Biashara inapaswa kuachana na mauzo rahisi na badala yake kwenda kwenye mauzo magumu.
Biashara inapaswa kuwekeza kwenye kuwatengeneza wateja wazuri, ambao huwa ni wagumu kuwapata. Lakini wateja hao wakishapatikana, huwa wanakuwa na manufaa makubwa kwenye biashara. Kwani huwa na uwezo wa kufanya manunuzi makubwa na kulipa vizuri.
Kila biashara inao uwezo wa kujenga wateja hao wazuri kama itakuwa tayari kuweka kazi ya kutosha kwenye kuwajenga wateja hao sahihi na siyo kuchukua tu wale wanaopatikana kirahisi.
Uchaguzi wa wateja na kufanyiwa kazi ni hitaji muhimu kwenye kufanya mauzo makubwa kwenye biashara.
Kitu kingine muhimu ambacho kinapaswa kufanyiwa kazi kwa ugumu ili kuwa na mauzo rahisi na makubwa ni kujenga timu bora ya mauzo. Mauzo hayawezi kufanywa na mtu mmoja au watu wa kawaida. Mauzo makubwa yanafanywa na timu bora, ambayo inaweka kazi ya kutosha kwenye mchakato wa mauzo.
Timu ya mauzo inapaswa kuwa na mafunzo sahihi na kuwa tayari kuwekea juhudi kubwa kwenye kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi na pia kuwafuatilia ili kuweza kujenga nao mahusiano mazuri na wakawa wateja wazuri wa biashara. Tunajua jinsi ambavyo timu zinazoshinda michezo zinavyokuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa na wanaojituma. Hivyo ndivyo pia timu ya mauzo inavyopaswa kuwa, wachezaji wenye uwezo na wanaojituma.
Uwepo wa timu, unategemea pia uwepo wa mchakato mzuri wa mauzo ambao unafanyiwa kazi. Kwa sababu timu bila ya mchakato, juhudi zitawekwa kubwa lakini matokeo yatakuwa madogo. Kila biashara inapaswa kuwa na mchakato wa mauzo ambao unafanyiwa kazi kwa msimamo, kutathminiwa na kuboreshwa kadiri ya matokeo yanayopatikana.
Kama unaona hayo yote ni kazi na magumu, unaweza kuona kwa nini umekuwa hufanyi mauzo makubwa kwenye biashara yako. Nikukaribishe kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA upate nafasi ya kujifunza kwa kina jinsi ya kuchagua ugumu kwenye mauzo, ili matokeo yake yawe rahisi na makubwa. Sikiliza kipindi hicho hapo chini na uchukue hatua kwenye mauzo yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.