Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, nguvu yetu ipo kwenye ushirikiano mzuri na wengine katika kupata kile ambacho tunataka.
Wakati tupo shule kuna hadithi mbalimbali tulikuwa tunafundishwa kuhusu wanyama kujaribu ushirikiano wa binadamu kwa manufaa yao lakini wakashindwa.

Hadithi ya nyani kulima shamba lao ili wasiwindwe na binadamu pale wanapoenda kula mazao yao ni moja ya hizo. Tuliona jinsi ambavyo nyani hao walikua wanaambiana kesho ndiyo watafanya. Mpaka leo kuna usemi wa kesho ya manyani.
Pia kuna hadithi ya nani kumfunga paka kengele. Hii ilieleza panya kuchoshwa na manyanyaso ya paka na kuamua wafunge paka kengele ili wawe wanasikika pale wanapowakaribia. Lakini mtihani ukabaki nani wa kuweza kufanya hivyo? Ndoto kubwa na nzuri ikaishia hapo.
Ukija kwetu sisi binadamu, tumeweza kufanya makubwa sana ambayo hayajawahi kudhaniwa kabisa hapa duniani. Yote hayo ni kwa sababu ya kuweza kushirikiana vizuri na wengine.
Na ushirikiano huo mzuri na wengine umewezeshwa na kitu kimoja muhimu; Mawasiliano. Mawasiliano baina ya binadamu yamechochea sana kasi ya mabadiliko na maendeleo ambayo yametokea hapa duniani.
Hivyo ndivyo sayansi na teknolojia zimeweza kukua kwa kasi sana, kwa sababu ya uwepo wa mawasiliano mazuri.
Licha ya manufaa hayo makubwa kimaendeleo ambayo yametokana na mawasiliano, bado kwa mtu mmoja mmoja hatujaweza kuyatumia vizuri mawasiliano.
Kushindwa kutumia vizuri mawasiliano imekuwa kikwazo kikubwa kwa watu kuweza kufanya makubwa. Watu wameshindwa kupata vile wanavyotaka, kwa sababu tu hawakuweza kueleweka vizuri na wale ambao wangewapa.
Mawasiliano huwa yana pande mbili, upande wa kwanza ni unaowasilisha na upande wa pili ni unaopokea. Ili mawasiliano yakamilike na kuwa na tija, pande zote mbili lazima ziweke umakini wa kutosha kwenye zoezi zima la mawasiliano.
Pamoja na upande wa pili kuwajibika, pale mawasiliano yanapokuhusisha wewe, bila kujali uko upande upi, unapaswa kuwajibika kwa asilimia 100. Kama wewe ndiye unayewasilisha, unapaswa kuwajibika kuhakikisha upande wa pili unakuelewa vizuri. Na kama wewe ndiye unayepokea mawasiliano, unapaswa kuwajibika kuhakikisha umeelewa kwa usahihi.
Swali ni unawezaje kuhakikisha umeeleweka pale unapowasilisha na umeelewa pale unapopokea? Jibu ni kwa kuuliza maswali sahihi. Nasema maswali sahihi kwa sababu swali la kuelewa ambalo wengi huwa wanauliza halina maana.
Pale unapomweleza mtu kitu, halafu mwisho ukamuuliza, je umeelewa? Unafikiri atakujibu nini? Kwa sehemu kubwa sana atakuambia ameelewa. Lakini hilo mara nyingi huwa siyo jibu sahihi na hapo ndipo mawasiliano yanapovunjika.
Swali sahihi la kuwauliza watu unaowapa maelekezo ni; Umeelewaje? Swali hilo linamtaka mtu akueleze vile alivyoelewa kile ulichomweleza. Na hapo sasa ndiyo utaweza kupima kama kweli umeeleweka. Mara nyingi utakapouliza swali hili, majibu utakayoyapata ni tofauti kabisa na kile ulichomaanisha. Na hapo unapata nafasi ya kufafanua zaidi na kuhakikisha upande wa pili umeelewa kwa usahihi.
Kwa upande wa pili, pale unapokuwa wewe ndiye unayesikiliza, anayekupa maelekezo anapofika mwisho, usimwambie umeelewa. Badala yake mwambie; Kwa nilivyokuelewa, unamaanisha…. Hapo unampa mrejesho wa jinsi ulivyomwelewa. Na hapo mtu anapata nafasi ya kukuambia kama ndicho alichomaanisha au kuboresha zaidi kama hukuelewa. Kwa kutoa mrejesho wako wa jinsi ulivyoelewa unajihakikishia kuondoka na maelekezo sahihi.
Zoezi hili ulilojifunza hapa, wakati unawasilisha na wakati unapokea, lifanye mara zote. Ukitoa maelekezo waulize watu wameelewaje na ukipokea maelekezo waambie watu jinsi ulivyoelewa. Hili tu litaboresha mawasiliano yako kwa kiasi kikubwa sana na kukuweka kwenye nafasi ya kupata mafanikio makubwa.
Kuna mambo manne muhimu ya kuzingatia kwenye mawasiliano ili yaweze kuwa bora. Mambo hayo nimeyaelezea kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA kuhusu mawasiliano na breki. Sikiliza kipindi hicho, ujifunze na kwenda kuyafanyia kazi ili uweze kuwa na mawasiliano bora yatakayokupa mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.