Rafiki yangu mpendwa,
Waswahili huwa wana kauli; kuanza upya siyo ujinga.
Hiyo ni kauli inayoweza kuonekana rahisi, lakini nyuma yake imebeba maana kubwa.
Kuna wakati mtu unakuwa umepambana na kitu kwa muda mrefu, umefanya uwekezaji mkubwa ndani ya kitu hicho, lakini kinakuwa hakina mwelekeo.
Huo ndiyo wakati wa kufanya maamuzi ya kuanza upya, ili kufanya kilicho sahihi kwa misingi sahihi ambayo itakupa kile unachotaka.

Hili la kuanza upya limekuwa ni gumu kwa wengi kufanya maamuzi, kwa sababu ni vigumu kujua ni wakati gani sahihi kufanya maamuzi hayo.
Tunajua jinsi ambavyo mafunzo ya mafanikio yanavyotutaka tuwe na ung’ang’anizi na kutokukata tamaa. Je huo ung’ang’anizi unapaswa kwenda mpaka wapi? Hilo ni eneo ambalo halina majibu ya moja kwa moja.
Maamuzi ya kuendelea au kuanza upya yanakuwa magumu kwa wengi kufanya kwa sababu kuu moja, watu wengi hawajui nini hasa wanachotaka. Ndiyo, unaweza kuwaona watu wakihangaika na mambo mengi, lakini kwa hakika hawajui wanataka nini. Ndiyo maana wengi ni rahisi kubadilika au kutokubadilika kabisa.
Kitu cha kwanza ambacho kila mtu anapaswa kujua ni nini hasa anachokitaka kwenye maisha yake. Ni malengo yapi makubwa aliyonayo ambayo atayapambania kwa kila namna. Hapo ndipo pa kuanzia na hayo ndiyo hayabadiliki.
Ukishajua unachotaka, hicho ndiyo hakitabadilika. Njia za kukupa kile unachotaka ambazo unazitumia ndiyo zinaweza kubadilika, kulingana na matokeo unayokuwa unayapata.
Chukua mfano umepanga safari ya kutoka Dar kwenda Arusha. Umechagua njia utakayotumia na ukiwa katikati ya safari, unakuta daraja limevunjika na njia haipitiki. Hapo ni lazima ubadili njia, lakini hupaswi kubadili safari yako ya kufika Arusha.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuendelea na malengo yako, kwa kuangalia njia ambayo ina uelekeo wa kukufikisha kwenye malengo hayo. Using’ang’ane tu na kitu kama saa mbovu, utapoteza muda na nguvu na utakosa unachokitaka.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha zaidi kuhusu hii dhana ya kuanza upya kwenye safari yako ya mafanikio, ili kufikia malengo ambayo unayo. Haijalishi umekutana na nini, kamwe usiyaache malengo yako makubwa. Karibu uangalie kipindi hicho, ujifunze na kupata msukumo wa kuyapambania malengo yako makubwa bila kuyaacha.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.