Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.

Maeneo makubwa mawili tunayoyafanyia kazi kwa uhakika ili kukuza mauzo ni USAKAJI ambao ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote na UFUATILIAJI ambapo ni kuwafuatilia wateja kwa karibu bila kukoma.

Kwenye usakaji, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE. Zipo njia mbalimbali za kusaka na kufuatilia wateja, moja wapo ni kwa kutuma jumbe fupi za simu (SMS) kwa watu wengi.

Kwenye somo lililopita tulijifunza kutuma ujumbe wa simu kwa mtu mmoja mmoja, ambayo ni njia yenye matokeo mazuri pale inapofanyiwa kazi vizuri.

KUTUMA UJUMBE KWA WATU WENGI (BROADCAST MESSAGE).

Huu ni mfumo wa kutuma ujumbe mmoja kwa watu wengi kwa wakati mmoja. Wakati kwenye kutuma ujumbe kwa mtu mmoja mmoja inakuwa kama mazungumzo, kutuma ujumbe kwa wengi inakuwa kama kutoa taarifa.

Ipo mifumo ya kuwezesha hili kufanyika kwa namna bora, kiasi kwamba wanaopokea ujumbe wanaweza wasijue kama ni ujumbe ambao umetumwa kwa wengi.

Mifumo ya kutuma ujumbe wa simu kwa watu wengi inaweza kutaja jina la mtu kwenye ujumbe kiasi cha mtu kuona ujumbe umeandikwa kwa ajili yao tu.

Mfano mzuri ni jumbe unazopokea kutoka mitandao ya simu, ambazo zinakutaja kwa jina. Unajisikia vizuri kwamba ujumbe umetaja jina lako, lakini ukweli ni hakuna aliyefanya hivyo kwenye hiyo mitandao, ni mifumo inachukua taarifa na kuzitumia.

Sisi kama wauzaji tunapaswa kutumia mifumo ya ujumbe wa simu kwa watu wengi kama njia ya kusaka wateja wapya na kuwafuatilia wateja tarajiwa na kamili ili kuendelea kuwa nao karibu.

MATUMIZI YA UJUMBE KWA WENGI KWENYE MAUZO.

Tunaweza kutumia mifumo ya kutuma ujumbe kwa wengi kwenye maeneo mengi ya mauzo, hapa tunakwenda kuangalia maeneo matatu ya msingi.

Moja ni kuchuja wateja tarajiwa na kujua wenye maumivu.

Kupitia usakaji, kwa njia mbalimbali zinazotumika, unapata mawasiliano ya watu wengi. Wengi wanaweza wasiwe na uhitaji kwenye wakati ambapo wamefikiwa. Lakini hupaswi kuwaacha kabisa kwa kuona hawafai. Kuna gharama zimeshatumika kuwafikia watu hao.

Katika hali kama hiyo, unaweka watu wote waliofikiwa kwa usakaji kwenye orodha maalumu ambapo mara kwa mara watakuwa wanatumiwa ujumbe wa simu. Kwa kuwa wanakuwa wengi, kutuma kwa mtu mmoja mmoja inakuwa kazi kubwa. Hivyo mfumo wa kutuma ujumbe kwa wengi unaweza kutumika.

Kwa mfumo huo, mara kwa mara unatuma ujumbe kwenye orodha ya wateja kuwakumbushe kile unachouza na wanavyoweza kunufaika nacho. Kwa kuona jumbe hizo, wanapokuwa na uhitaji wataweza kuchukua hatua ya kukutafuta na kuwafuatilia kukamilisha mauzo.

Mbili ni kuwakumbusha wateja kwenye ahadi zao.

Wateja wanaweza kutoa ahadi mbalimbali ambazo zinahitaji ufuatiliaji ili kukamilisha au kuwakumbusha wakamilishe. Kadiri wateja wanavyokuwa wengi, ndivyo inakuwa vigumu kumkumbusha mmoja mmoja.

Hapo unaweza kutumia mfumo wa kutuma ujumbe kwa wengi kuwa unawakumbusha wateja. Kwa kuunganisha na mfumo wako wa mauzo, ujumbe unaweza kutumwa kwa wateja moja kwa moja kuwapa taarifa mbalimbali kama kukamilisha malipo, kurudi tena kununua na taarifa nyingine unazoweza kuwa unataka wateja wazipate.

Kwa kuunganisha mfumo wa ujumbe na mifumo mingine iliyopo kwenye biashara, jumbe mbalimbali zinaweza kutumwa moja kwa moja kwa wateja, bila ya kuhitaji kuandikwa kila mara. Chukua mfano wa jumbe unazopokea kwenye mitandao ya simu pale unapotumiwa fedha, siyo kwamba mtu anakaa chini na kuandika ujumbe mmoja mmoja na kutuma, bali mifumo inatengeneza ujumbe na kutuma moja kwa moja.

Hilo pia linawezekana kwa kila biashara kulingana na mahitaji yake. Muhimu ni mawasiliano na wateja yasikwamishwe kwa sababu zozote zile.

Tatu ni kutuma salamu mbalimbali kwa wateja.

Kwa sikukuu za kitaifa au za kidini ambapo unahitaji kutuma salamu kwa wateja wako, itakuwa kazi kubwa kutuma kwa mmoja mmoja. Kwa kutumia mfumo wa kutuma ujumbe kwa wengi, unaweza kuandaa ujumbe mmoja na kuutuma kwa maelfu ya wateja wako.

Hilo linarahisisha sana kuwafikia wateja wengi kwa urahisi na uhakika. Na uzuri ni unaweza kuandaa jumbe zote unazotaka kutuma mapema na wakati unapofika zinaenda bila ya wewe kuhitajika kutuma moja kwa moja. Yaani unaweza kuandaa ujumbe na kuupanga leo, ila ukaenda kwa wateja siku zijazo.

SOMA; Usakaji Wa Wateja Kwa Kupiga Simu.

MAMBO YA KUZINGATIA ILI UJUMBE KWA WENGI UWE NA UFANISI.

Kwenye kutuma ujumbe kwa wengi kwa wakati mmoja, kuna mambo muhimu ya kuzingatia ili zoezi liwe na ufanisi mzuri.

1. Ujumbe unapaswa kuwa mfupi na wenye ushawishi. Wateja wanapokea jumbe nyingi kwa siku, ili wasome ujumbe wako, lazima uwe na kitu cha kuwashawishi.

2. Ujumbe utaje jina la mteja kwa usahihi. Kwa mteja kuona jina lake limetajwa, anajisikia vizuri na kuzingatia ujumbe huo. Ili jina liende kwa usahihi, lazima taarifa za wateja zichukuliwe na kutunzwa kwa usahihi.

3. Ujumbe uwe na hatua ya mteja kuchukua. Ujumbe usiishie tu na maelezo, bali umpe mteja hatua ya kuchukua mara moja ili mawasiliano yaweze kukamilika kama inavyotegemewa.

4. Ujumbe uwe na jina la biashara na mawasiliano ili mteja akumbuke vizuri. Mara nyingi jumbe za kutuma kwa wengi huwa haziendi kwa namba ya simu kama jumbe za kawaida. Hivyo jina la biashara unalotuma nalo linapaswa kusajiliwa kwenye mfumo wa jumbe ili lionekane kwa wateja. Pia ndani ya ujumbe uweke mawasiliano ya simu ambayo mteja anaweza kuyatumia.

5. Tuma jumbe kwa mpangilio mzuri, kwenye muda na aina ya ujumbe. Jumbe zisiwe nyingi na za kujirudia rudia na wala zisionekane kama matangazo maana watu watajifunza kuzipuuza.

MFANO WA MFUMO WA JUMBE KWA WENGI.

Kuna mifumo mingi inayoweza kutumika kutuma ujumbe kwa watu wengi. Mfano mmoja ni BEEM ambayo ni kampuni inayotoa huduma hizo za kutuma ujumbe kwa watu wengi.

Kuna gharama za kutuma jumbe hizo ambazo zinatozwa kwa kila ujumbe. Gharama huwa zinategemea idadi ya jumbe ambazo mtu ananunua.

Kwa maelezo zaidi kuhusu mfumo wa BEEM, tembelea tovuti yao kwa anwani hii; https://beem.africa/

Kama wauzaji tutumie mifumo ya kutuma ujumbe kwa watu wengi ili kurahisisha na kuboresha mawasiliano na wateja wetu na kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.