Rafiki yangu mpendwa,
Kile ambacho watu wanaita ni biashara, kwa wengi siyo, bali ni ajira binafsi. Pale biashara inapokuwa inakutegemea wewe kwa kila kitu, haiwi na sifa ya biashara, bali inakuwa kujiajiri. Ili biashara iweze kuwa na mafanikio makubwa, lazima iweze kujiendesha bila ya kumtegemea mwanzilishi au mmiliki wake moja kwa moja.
Hilo limekuwa gumu kwa watu kuelewa na kutekeleza kwa sababu hakuna mafunzo ambayo watu wanayapata kabla ya kuingia kwenye biashara. Wengi wanaingia kwenye biashara kwa msukumo wa kuwa na kipato cha uhakika na wanaishia kwenye gereza ambalo linawatesa kwa miaka mingi.

Kuondokana na hayo yote, kuna P NNE za kufanyia kazi kwenye biashara ili iweze kuwa imara na yenye mafanikio.
P YA KWANZA NI PEOPLE (WATU).
Biashara ni watu, hakuna namna mtu unaweza kujenga biashara yenye mafanikio makubwa bila ya kuwahusisha watu.
1. Inaanza na wewe mwenyewe mmiliki wa biashara kuwa na utimamu wa afya ya mwili, akili, hisia na roho. Usipokuwa imara, safari itakushinda.
2. Inakusisha wafanyakazi unaohitaji ili kujenga biashara kubwa, lazima wawe na tabia sahihi na wachapakazi hasa.
3. Watu wako wa karibu wanaokuzunguka wana mchango kwako kufanikiwa au kushindwa kwenye biashara. Zungukwa na watu sahihi watakaokusukuma kufanikiwa.
4. Wateja wa biashara yako ni watu muhimu, lazima uwatengeneze wakati wote na kujenga nao mahusiano mazuri.
5. Wadau wengine wa biashara yako kama wasambazaji, wawekezaji na wengine wanaochangia biashara kwenda ni muhimu. Wachague kwa usahihi ili wasikwamishe biashara.
Fanya kazi kubwa kwenye kupata watu sahihi ili biashara iweze kukua.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Timu Bora Ya Kukupa Mafanikio Kwenye Biashara.
P YA PILI NI PROCESS (MCHAKATO).
Mchakato ni mfumo mzima wa jinsi mambo yanavyofanyika kwenye biashara. Kila kitu kinachofanywa kwenye biashara kinapaswa kuelezewa hatua kwa hatua jinsi kinavyofanyika. Na kila anayetekeleza anapaswa kufuata mchakato kama ulivyoeleza na siyo kufanya vile anavyojisikia yeye. Uzuri wa mchakato ni ukiwa sahihi na ukafuatwa kwa usahihi, matokeo yanakuwa ni ya uhakika.
Andika jinsi kila kitu kwenye biashara kinapaswa kufanyika, hatua kwa hatua. Kisha hivyo ndivyo itakavyofanyika. Pale kunapokuwa na changamoto kwenye utekelezaji wa mchakato, maboresho yanafanyika na mchakato kufuatwa kwenye maboresho hayo.
P YA TATU NI PRODUCT (BIDHAA).
Bidhaa ni kile ambacho biashara inauza ili kupata fedha. Inaweza kuwa bidhaa inayoshikika au huduma ambayo haishikiki. Kilicho muhimu hapa ni bidhaa au huduma kutoa thamani kubwa kwa wateja wanaolengwa. Wateja wawe tayari kununua kwa sababu wanaona thamani kubwa wanayoipata ukilinganisha na bei ambayo wanalipa.
Bidhaa au huduma unayouza inapaswa kuanza na tatizo ambalo tayari wateja wanalo na wanatafuta namna ya kulitatua. Unapowafikia watu wa aina hiyo, ukiwa na utatuzi wa matatizo yao, wanakuwa tayari kununua. Bidhaa na huduma zinapaswa kuendelea kuboreshwa kadiri muda unavyokwenda ili kuendelea kutoa thamani kubwa kwa wateja.
P YA NNE NI PROFIT (FAIDA).
Faida ndiyo kipimo cha ukuaji wa biashara, lakini pia ndiyo kitu kigumu zaidi kukokotolewa kwenye biashara. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanapambana sana kukuza mauzo, lakini bado biashara zinakuwa zinakufa. Hiyo ni kwa sababu wanaweza kuwa wanauza sana, lakini hakuna faida kubwa wanayotengeneza. Au wanauza sana, lakini kwa hasara.
Ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio makubwa, lazima uweze kukokotoa faida kwa uhakika kwenye biashara yako. Na pia uweze kuiona faida hiyo kwa uhalisia na siyo tu kwenye hesabu za biashara zilizopo kwenye makaratasi. Biashara ikiweza kutengeneza faida kwa uhakika, itafanya makubwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua zaidi hizi P NNE na namna ya kuzifanyia kazi. Fungua kipindi hapo chini ujifunze na uweze kujenga biashara yenye mafanikio makubwa kwa kufanyia kazi mambo hayo manne.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.