3357; Rahisi ni ngumu zaidi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa inatamanisha sana kutafuta na kutumia njia rahisi za kupata kile tunachotaka.
Lakini hizo huwa zinaishia kuwa njia ngumu zaidi.
Kutumia njia rahisi huwa inafanya maisha kuwa magumu sana.
Kutafuta njia za mkato kunapelekea kupoteza muda mwingi zaidi.
Kununua vitu vya bei rahisi huwa kunaishia kutumia gharama kubwa zaidi.
Kukwepa kufanya mazungumzo magumu ambayo unapaswa kuyafanya na watu muhimu kwako, kunaathiri zaidi mahusiano yenu.
Yote hayo ni kwa sababu wengi huwa wanakimbilia kwenye urahisi na hivyo thamani yake inakuwa ni ndogo.
Ili kuacha kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi ya yalivyo sasa, mara zote chagua njia ngumu.
Kunapokuwa na njia mbili mbele yako, moja ngumu na nyingine rahisi, chagua ile ngumu.
Wekeza kwenye vitu ambavyo gharama zake ni kubwa.
Tumia njia sahihi na ndefu na achana na njia za mkato.
Kufanya hayo yote magumu kutakuumiza mwanzoni, lakini baadaye kutakuwa na msaada mkubwa sana wa kukupa matokeo makubwa na ya tofauti.
Mwanzo watu watakuona ni mshamba na usiyejua mambo mazuri na rahisi yaliyopo. Lakini wakati unapata matokeo makubwa na wale waliohangaika na njia hizo rahisi kuishia kwenye ugumu, itajidhihirisha wazi nani ndiyo mshamba zaidi.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mara zote tunafanya kile kilicho sahihi na siyo kilicho rahisi.
Tunaangalia kile kinachotupa matokeo makubwa na rahisi.
Sasa kwa kuwa wengi huwa wanayaacha mambo magumu na kwenda kwenye mambo rahisi, sisi tunayaendea hayo magumu yasiyokuwa na wengi.
Unachotaka ni mafanikio makubwa, hivyo kuwa tayari kuumia na yale magumu mwanzoni na ambayo yatakupa matokeo makubwa na ya tofauti.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe