Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka CHUO CHA MAUZO.
Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.
Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.
Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 23 na 24.
Kwenye mbinu namba 23 tulijifunza ukamilishaji fanya kwa ajili yangu na kwenye mbinu namba 24 tulijifunza ukamilishaji wa bidhaa ya chini
Kama ulienda kuzifanyia kazi na kupata matokeo basi karibu sana utushirikishe namna ulivyonufaika nazo mbinu hizo.
Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 23-24
Leo kwenye ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 25 na 26.
Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo;

- Ukamilishaji wa bidhaa ya juu.
Ukamilishaji huu wa bidhaa ya juu unatumika kupima uhitaji wa mtu kwenye kile anachoulizia.
Pia unaweza kutumika pale mtu anaposema bei ni kubwa, maana anaweza kuona thamani anayopata haiendani na bei anayolipa.
Kwa kumpa thamani ya juu zaidi kwa malipo ya ziada anaweza kuwa tayari kununua.
Kwa mfano, unamwambia mteja;
“Kabla hatujakamilisha napenda kukushirikisha kwamba kama utachukua hii ya juu zaidi, itaongeza gharama kidogo lakini itakupa thamani zaidi.
Je utakuwa tayari kwa ajili ya hii ya juu?”
Kwahiyo, ukamilishaji huu unampa mtu thamani kubwa licha ya bei kuwa kubwa lakini unamuonesha kwamba anakwenda kupata manufaa makubwa kwa kiasi kikubwa cha bei anayolipia.
Kama mteja anataka ubora na thamani, ukitumia mbinu atakua tayari kununua na kama hayuko tayari kununua basi utajua mapema na hilo litakusaidia wewe kuelekeza nguvu zako sehemu nyingine muhimu.
- Ukamilishaji wa bidhaa mbadala.
Huu ni ukamilishaji wa mbadala wa bei ya juu, mteja ameshindwa bei ya juu uliyokuwa umempendekezea na kumuonesha namba bidha au huduma unayotoa ilivyokuwa na thamani.
Kabla mteja hajaondoka kwa kushindwa bei au thamani, anapaswa kuelezwa kuhusu mbadala unaopatikana, iwe ni juu au chini.
Hivyo basi, wewe kama muuzaji unapaswa kumwambia hivi mteja wako.
“Kama malipo yamekuwa makubwa kwako, napendekeza turudi kwenye bidhaa ambayo iko chini ya hii.”
Kwa kumpendekezea mteja bei mbadala kama alikuwa hana uwezo wa kumudu bei ya juu, kwa bei ya chini ataweza kumudu kununua.
Lakini pia, hapa utakua unatumia ule ukamilishaji wa uza juu, kati , chini kama tulivyojifunza kwenye kitabu cha CHUO CHA MAUZO kwenye somo la 58.
Rafiki yangu na muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, ni muhimu sana kuhakikisha humwachii mteja akaondoka bila kununua au kulipia kiasi kidogo cha fedha ambacho kitamfanya arudi.
Mara nyingi watu hawaoni shida kupoteza muda wako wote ambao umetumia kwao.
Kwahiyo, unapaswa kuthamini muda wako, kama umeenda ha mteja mpaka hatua za mwisho, usikubali kuondoka mikono mitupu, hakikisha unalipwa kweli kwa muda uliotumia kwake.
Usikubali kushindwa kwenye kila kitu, ondoka na ushindi wowote ule kutoka kwa mteja anunue kitu chochote kile.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz