Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu maalumu ya kujenga utajiri kupitia uwekezaji wa hatua ndogo ndogo kwa muda mrefu bila kuacha.
Kanuni kuu ya uwekezaji tunayoifanyia kazi kwenye programu yetu ni WEKEZA NA SAHAU. Kanuni hiyo inatutaka tuwekeze kisha tuendelee na mambo yetu mengine, ili tuuache uwekezaji ukikua na kutuzalishia faida.
Hiyo ni rahisi kusema na kupanga, lakini kutekeleza, inakutaka uwe na roho mbaya sana na ngozi ngumu. Nakueleza hayo siyo kukupa hofu, bali kukupa uhalisia ambao utakutana nao kwenye hii safari ya uwekezaji. Kama hutauelewa huo uhalisia na kuweza kuuvuka, hutaweza kunufaika na uwekezaji kwa kanuni ya WEKEZA NA SAHAU.

Katika hali mbalimbali ambao mtu unakuwa unapitia kwenye maisha, moja ya kitu muhimu unachopaswa kufanya ni KUTOKUFANYA CHOCHOTE. Ndiyo, yaani kuna hali fulani unazokuwa unapitia ambapo suluhisho ni kutulia tu, halafu muda unafanya mambo yake. Katika hali kama hizo, pale tu unapojaribu kufanya kitu, unaishia kuharibu zaidi.
Sasa basi, kama kuna kitu kigumu kwetu binadamu kufanya, ni kutokufanya chochote. Yaani tusipofanya kitu, huwa tunaona kama tunakosea hivi. Hilo limekuwa linapelekea hata kufanya mambo ambayo yanatuumiza au kukudhuru, kwa sababu tu hatupo tayari kukaa bila kufanya chochote.
Hili limewahi kufanyiwa utafiti na majibu yalidhihirisha wazi jinsi kutokufanya chochote ni kitu kigumu sana kwetu binadamu. Watu waliwekwa kwenye chumba chenye kamera na hakikuwa na kitu kingine chochote isipokuwa nyaya ambazo mtu akizigusa anapigwa shoti. Na mtu aliambiwa kabisa ukigusa hizo nyaya utapigwa shoti. Watu waliachwa kwenye vyumba hivyo kwa muda na haikuchukua muda mrefu, walianza kushika nyaya hizo na kupigwa shoti. Ilidhaniwa kwamba kama mtu atapigwa shoti mara moja, hatarudia tena kuzishika nyaya hizo. Lakini haikuwa hivyo, kwani watu waliendelea kuzishika kwa namna ya tofauti na kuendelea kupigwa shoti. Yote hayo yalitokana na kwamba hawakuwa na kitu kingine cha kufanya na watu huwa hawapendi kutokuwa na kitu cha kufanya.
Tukirudi kwenye uwekezaji, ukishaweka mpango wako wa uwekezaji, wa kiasi unachowekeza mara kwa mara na muda wa kuwekeza, umemaliza, hupaswi kufanya kitu kingine chochote, zaidi ya kuendelea na mpango wako.
Maswali yatakuja, vipi kama uwekezaji unashuka thamani, nifanye nini? Jibu ni moja, usifanye chochote, wewe endelea na mpango wako kama ulivyoweka.
Swali jingine, vipi kama nimeona fursa nzuri sana nje ya uwekezaji, kwa nini nisitoe huo uwekezaji na kupeleka kwenye fursa hiyo. Jibu ni moja, usifanye chochote, acha uwekezaji wako uendelee kukutengenezea thamani.
Mara nyingi sana mipango tunayokuwa nayo huwa ni sahihi, kwa sababu tumeiweka kwa kufikiri wakati ambapo tuna utulivu na akili zetu zinafanya kazi vizuri. Lakini tunapokuja kubadili mipango hiyo, huwa tunaishia kukosea kwa sababu tunayafanya mabadiliko hayo kwa kusukumwa na hisia. Na pale hisia zinapokuwa juu, fikra zinakuwa chini. Maamuzi yoyote unayoyafanya kwa kusukumwa na hisia huwa yanakuwa ni maamuzi mabovu kwako.
Usifanye chochote bali endelea na mpango wako ni kitu cha kuelewa na kukisimamia kwenye uwekezaji kama unataka mafanikio. Ukiwa tayari kubadili mipango uliyoweka kwa sababu ya mambo unayokutana nayo, utaishia kuharibu vitu vizuri ambavyo vilikuwa vinaendelea.
SOMA; Hii Ndiyo Njia Ya Uhakika Ya Kuongeza Kipato Chako Kwa Kuanzia Hapo Ulipo Sasa.
Kwa nini inabidi uwe na roho mbaya sana?
Ni kwa sababu unatakiwa kuendelea na mpango wako bila ya kujali unapitia nini kwenye maisha yako. Unaweza kuwa na sababu sahihi kabisa za kutokuendelea na mpango wako wa uwekezaji, lakini inabidi uendelee nao kama ulivyopanga, hata kama itakuwa ni kwa kujiumiza wewe mwenyewe.
Kwa mfano kama mpango wako wa uwekezaji ulioweka ni kutoa fedha kwenye kipato chako cha mshahara na kuwekeza, halafu ikatokea huna tena kazi hiyo inayokupa mshahara, si una sababu sahihi ya kutokuendelea na mpango huo? Jibu ni ndiyo kama una roho nyepesi na kwa roho ya aina hiyo huwezi kufanikiwa. Unahitaji kuwa na roho mbaya ya kuhakikisha unaendelea na mpango wako wa uwekezaji hata kama chanzo cha kipato ulichokuwa unategemea hakipo tena. Na hapo utalazimika ufanye chochote unachoweza, ambacho ni halali kupata fedha ya kuwekeza. Kama utafanya kazi za kutumia nguvu, kama utaomba na kama utaacha kula ili uwekeze, haijalishi, muhimu ni uendelee kuwekeza.
Kama hujafikia ngazi ya kujitoa kiasi hicho kwenye uwekezaji, kama unawekeza mambo yakiwa mazuri na kuacha mambo yakiwa magumu, upo kwenye mchezo wa watoto na sahau kuhusu mafanikio makubwa kwenye uwekezaji.
Kwa nini unahitaji ngozi ngumu?
Kwa sababu watu watakusema kwa mambo mengi kuhusu mpango wako wa uwekezaji na jinsi unavyoenda nao. Watu watakuwa na kiherehere cha kukushauri hata kama hujawaomba ushauri. Watu wasiokuwa na uelewa kabisa kuhusu unachofanya watajipa umuhimu wa kukuambia ni jinsi gani unapaswa kuyaishi maisha yako.
Unahitaji ngozi ngumu ili kuwapuuza hao wote na kuendelea na mpango wako wa uwekezaji kama ulivyouweka. Unapaswa kuacha kuhangaika na mambo ya wengine na kuhangaika na mambo yako ili uweze kuyafanya kwa usahihi.
Watu wengi sana wamejikwamisha kwenye maisha kwa sababu ya kusikiliza maoni ya wengine na kupuuza ukweli ulio ndani yako. Unapaswa kujua kwamba chochote unachoambiwa na wengine kuhusu maisha yako na yale unayofanya ni maoni tu, ukweli halisi kuhusu wewe unaujua wewe peke yako.
Utakosolewa, utakatishwa tamaa na utasemwa vibaya na wengine kwa sababu ya kuyaishi maisha yako tofauti kama mwekezaji. Ukiwa na ngozi nyepesi, mishale yao yenye sumu itakuingia na utatetereka. Unahitaji ngozi ngumu ambapo mishale wanayokurushia inadunda na kurudi kwao. Hivyo ndivyo utaweza kuendelea na mpango wako wa uwekezaji kama ulivyoweka.
Kuwa na mengi yanayokutinga.
Tumeona kinachotusukuma kufanya mambo ambayo yanatudhuru, ni pale tunapokuwa hatuna kitu tunachofanya. Na kama unavyoeleza usemi kwamba akili tupu ni karakana ya maovu, kama huna mambo yanayokuweka ‘bize’ unajiweka kwenye nafasi ya kuanza kufanya mambo yanayovuruga uwekezaji wako. Kama huna kazi ambazo zinakupa changamoto kubwa na kukuchosha, ndiyo utajikuta unaanza kusikiliza maoni ya watu ambao hawajielewi na kuchukua hatua ambazo zinakuharibia.
Tumechagua kufanya uwekezaji wa mifuko ya pamoja, ili tukishawekeza tunaendelea na majukumu yetu mengine. Hivyo hakikisha unakuwa na majukumu yanayokutinga ili usijikute huna cha kufanya na kuanza kuingilia uwekezaji wako. Na kitu bora kwa kila mwekezaji aliye kwenye programu ya NGUVU YA BUKU kufanya ni kuwa na biashara ambayo anapambana kuikuza.
Unatakiwa uwe na biashara ambayo inakuweka bize kiasi kwamba huna muda wa kuanza kusikiliza maoni ya watu ambao hawajielewi. Kila wakati unakuwa unapambana na majukumu ya kuikuza biashara yako kiasi cha kukosa kabisa muda wa kuanza kuingilia uwekezaji wako na kuuvuruga.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili la uwekezaji, ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Kwa nini ni vigumu sana kwetu binadamu kutokufanya chochote hata kama hilo ndiyo bora zaidi?
2. Ni kwa jinsi gani umejiandaa kuwa na roho mbaya na ngozi ngumu ili kufanikiwa kwenye uwekezaji?
3. Ni kitu gani umechagua kitakuweka ‘bize’ muda wote ili usisikilize maoni ya wasiojielewa na kuvuruga uwekezaji wako?
4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo hili au programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali haya kama kiashiria kwamba umejifunza na kulielewa somo hili na unaenda kuliweka kwenye matendo ili kufanikiwa kwenye uwekezaji.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
Naipenda matini hii
LikeLike
Karibu
LikeLike