3377; Raia au mtalii?

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye kila eneo la maisha yetu, watu wamegawanyika kwenye makundi makubwa mawili ambayo ni raia na watalii.

Raia ni watu ambao wana makazi ya kudumu kwenye nchi au eneo husika wakati watalii ni watu wa kupita tu ambao hawana makazi ya kuduku.

Raia wanakaa kwenye eneo kwa muda mrefu na hivyo kulitunza ili maisha yao yaweze kuwa bora wakati watalii ni wapitaji tu kwenye eneo na hivyo hawahangaiki kulifanya kuwa bora.

Raia wamejitoa hasa na hawakimbii pale wanapokutana na vikwazo na changamoto wakati watalii wanakimbia haraka pale wanapokutana na vikwazo na changamoto.

Kwenye mafanikio, raia ni wale waliojitoa hasa kufanikiwa na kuwa tayari kukabiliana na chochote mpaka kuyapata mafanikio. Watalii ni wale wanaoyatamani mafanikio lakini hawajajitoa hasa kuyapata, wanapokutana na magumu na changamoto wanaachana na safari hiyo.

Kwenye biashara, raia ni wale wanaochagua aina ya biashara na kisha kuweka kazi kubwa kwenye kuijenga na kutoa thamani kubwa kwa wengine, anapokutana na changamoto anazivuka na kuendelea. Watalii ni wale wanaoingia kwenye biashara kwa mihemko, kwa kudhani ni rahisi kufanikiwa kwenye biashara hiyo, wanapokutana na changamoto wanakimbia na kuacha.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunatengeneza raia wa safari ya mafanikio, ambao wamejitoa hasa mpaka wafanikiwe bila kukwamishwa na chochote.
Katiba ya jamii hiyo ni mchakato ambao kila mwanajamii anaufuata kwa msimamo na uaminifu bila kuacha.
Ni jamii inayoamini kwenye kujenga mafanikio sahihi kwa kufuata misingi sahihi.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, watalii pia wamekuwa hawakosekani. Hawa hujulikana haraka kwa jinsi ambavyo huwa wanakuja kwa kelele na kuondoka kimya kimya.
Wakati wanaingia wanakuwa wanaeleza jinsi wanavyotaka kufanya makubwa na kuwa tayari kujitoa sana katika kuufuata mchakato. Lakini dalili ya kwanza inayoonekana kwao, tena kwa haraka sana ni kushindwa kuufuata mchakato.
Watakuja na maelezo mengi ya nini kinawakwamisha kwenye mchakato, lakini ukweli unabaki kwamba siyo raia bali ni watalii na hawachukui muda mrefu kabla hawajapita na kuondoka.

Kuwa raia wa jamii ya KISIMA CHA MAARIFA kunakupa tiketi ya kuwa raia wa ile shughuli yako kuu unayofanya. Kwa jinsi unavyokuwa umejitoa kwenye mchakato wa mafanikio, ndivyo pia unavyojitoa kwenye mambo yote unayoyafanya na hilo linakuweka kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa kuliko wale wanaohangaika na mambo mengi kwa kutafuta urahisi.

Rafiki, je wewe ni raia au mtalii kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA?
Kwenye shughuli kuu unayofanya, umechagua kuwa raia wa shughuli gani? Umejitoa kiasi gani ili kuhakikisha kweli unafanikiwa?
Kila raia wa KISIMA CHA MAARIFA ashirikishe majibu ya maswali haya hapo chini.
Kwa watalii, unaweza kufanya hivyo kama utapenda, japo watalii wengi hata hii taarifa hawataiona na wakiiona hawataisoma.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe