3387; Kupoteza au kuvurugwa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Nzuri ni adui wa bora, huwezi kupata kilicho bora kama haupo tayari kupoteza kizuri ulichonacho.
Kukumbatia kile kilicho kizuri imekuwa kikwazo kwa wengi kupata kilicho bora.
Na kwa walio wengi, hawana hata kilicho kizuri, bali wana kile ambacho ni cha kawaida, ambacho kinawafanya wawe chini kabisa.

Ili mtu aweze kutoka pale alipo na kwenda mbali zaidi, anatakiwa kupata hasira ambazo zinamtoa hapo.
Hasira hizo zinaweza kutokana na kupoteza kile alichonacho sasa au kuvurugwa na hali anayokuwa nayo sasa.

Kama umekuwa kwenye hatua uliyopo sasa kwa muda mrefu, ni kwa sababu umeridhika nayo.
Hata kama siyo hatua unayoitaka, lakini bado unaweza kuizoea na ikawa kikwazo kikubwa kwako.

Kwa sababu ya mazoea na kupenda uhakika, tunaweza kuona tulichonacho sasa ndiyo pekee tunachoweza kuwa nacho.
Ni mpaka tupoteze tulichonacho au kuvurugwa na pale tulipo ndiyo tunaona jinsi tunavyoweza kufanya makubwa zaidi.

Wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kujivuruga wewe mwenyewe ili usizoee sana kwenye hatua unayokuwa umefikia.
Sisi binadamu huwa tunazoea hali tunazokuwa nazo haraka sana.
Kama hautachukua hatua za makusudi za kujaribu vitu vipya kila wakati, tutajizuia kupata ukuaji mkubwa zaidi.

Kwenye mafanikio kwenye biashara na maisha kwa ujumla, unapaswa kujivuruga mwenyewe kabla hujavurugwa na wengine. Unapaswa kuyavunja mazoea yako mwenyewe kabla hayajawa mzigo kwako.
Kila wakati kuwa unachukua hatua za kukutoa pale ulipo sasa na kwenda mbele zaidi, hata kama unaona hakuna ulichokosa. Hatua hizo ndiyo zitakuweka mbele ya ushindani na kukuwezesha kufanya makubwa.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, sisi ndiyo washindani wetu namba moja. Yaani tunakuwa wa kwanza kujitoa wenyewe pale tulipofika. Tunafanya hivyo kupitia kujifunza vitu vipya na kuchukua hatua mpya kila wakati.
Kupitia kujifunza na kuchukua hatua mpya, tunaona uwezekano mpya ambao unatutoa kwenye mazoea tuliyonayo na kutupa matokeo ya tofauti.
Ni kwa njia hiyo ndiyo tunapiga hatua kubwa kila wakati.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, haijalishi ni mafanikio makubwa kiasi gani tunayo, bado tunaendelea na mchakato wa kuweka malengo makubwa zaidi, kujifunza na kujaribu vitu vipya.
Tunajua mafanikio hayana kilele cha mwisho kabisa, kilele cha kuwa umemaliza kila kitu.
Kwa kila hatua tunayofikia tunakuwa tunajua kuna hatua kubwa zaidi ya hiyo.
Hilo linatuzuia kujenga mazoea ambayo yamekuwa ndiyo kikwazo cha kuendelea kupata mafanikio makubwa.

Kamwe usiridhike na hatua yoyote ambayo umeshafikia, kwani bado kuna hatua nyingine nyingi mbele yako.
Endelea kuweka malengo makubwa kuliko pale ambapo umeshafika na endelea kujifunza na kujaribu vitu vipya wakati wote.

Steve Jobs alisema ili upate mafanikio makubwa, mara zote baki mjinga na baki na njaa.
Baki mjinga kwa kuwa tayari kujifunza na baki na njaa kwa kutoridhika na popote ulipofika.
Hayo yana nguvu ya kukupa mafanikio makubwa na kwa uendelevu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe