Rafiki yangu mpendwa,
Kikwazo kikubwa kwa watu wengi kujenga utajiri siyo kipato, bali kutokujua.
Wengi hudhani kwamba wanakosa utajiri kwa sababu kipato chao ni kidogo.
Lakini angalia watu wengi ambao huwa wanakuwa na kipato kikubwa, maisha yao huwa yanaishiaje? Wengi sana kipato kinapoisha, wanadondokea kwenye umasikini mkubwa.
Kama ingekuwa kikwazo cha kujenga utajiri ni kipato, basi watu wote wenye kipato kikubwa wangekuwa na utajiri wanaodumu nao. Lakini kwa sababu uhalisia sivyo ulivyo, basi kujenga utajiri ni zaidi ya kipato. Na hilo ndiyo ambalo wengi hawajui.
Kwa sababu wewe ni rafiki yangu, ambaye nakupenda na kukujali sana, wajibu wangu umekuwa ni kukupa wewe maarifa sahihi, ambayo ukiyaweka kwenye vitendo basi unafanikiwa.
Kwenye kujenga utajiri, unachokosa ni maarifa sahihi na kama unayo basi kuyaweka kwenye vitendo. Na hayo mawili ndiyo unayoyapata kwenye mafunzo ninayotoa, maarifa pamoja na kuchukua hatua.

Mwandishi Ramit Sethi, kwenye kitabu chake cha I WILL TEACH YOU TO BE RICH ametushirikisha hatua muhimu sana ya kujenga utajiri ambayo ni UWEKEZAJI.
Karibu tujifunze kutoka kitabu hicho na kwenda kuchukua hatua ili kunufaika.
SURA YA 3; KUWA TAYARI KUWEKEZA.
Kuweka akiba peke yake haitoshi kujenga utajiri. Hiyo ni kwa sababu riba ambazo benki zinatoa kwenye kuweka akiba ni ndogo sana, huku kukiwa na gharama ambazo zinafanya mtu kupoteza fedha.
Utajiri unajengwa kwa kuwekeza maeneo sahihi, kwa msimamo na muda mrefu bila kuacha. Kwa bahati mbaya sana uwekezaji ni kitu ambacho kimekuwa hakifundishwi.
Lakini kibaya zaidi ni kwamba watu wengi wanapoiga matajiri, huwa wanaiga matumizi yao na siyo uwekezaji wao, ambao ndiyo umewapa utajiri walionao.
Ukweli ni kwamba kila mtu anaweza kuwekeza, hata kwa kiasi kidogo kabisa. Kinachohitajika zaidi kwenye uwekezaji ni muda ambao mtu amewekeza kuliko hata kiasi.
Katika kufanya uwekezaji ili kujenga utajiri wa uhakika, kuna ngazi sita za kufuata.
Ngazi ya kwanza; Kuwa na mfuko wa uwekezaji wa kustaafu. Huu ni mfuko ambao unawekeza kwa ajili ya mafao yako ya baadaye. Kwa kila kipato unachoingiza unahakikisha kuwekeza kwenye mfuko huo.
Ngazi ya pili; Lipa madeni uliyonayo ili kupunguza gharama zinazokukwamisha kujenga utajiri. Riba unayolipa kwenye madeni, kadiri inavyoenda kwa muda mrefu ndivyo inavyokuwa kikwazo kwako.
Ngazi ya tatu; Kuwa na akaunti binafsi ya uwekezaji. Wakati unafanya uwekezaji kwa ajili ya kustaafu, fanya pia uwekezaji wa aina nyingine kwa ajili ya kujenga utajiri wako wa baadaye.
Ngazi ya nne; Fanya uwekezaji mkubwa kwenye maeneo uliyochagua. Kila ongezeko la kipato unalopata usitumie, badala yake wekeza.
Ngazi ya tano; Tumia fursa nyingine za uwekezaji zenye unafuu wa kikodi. Unapokuwa kwenye uwekezaji, utaziona fursa za kuwekeza ambazo hazina makato makubwa ya kodi, zifanyie kazi.
Ngazi ya sita; Endelea kuwekeza kwa ukubwa na pia wekeza ndani yako ili kuwa bora zaidi.
Weka mpango wako wa uwekezaji na kuufanyia kazi. Kwenye somo linalofuata, (sura ya 7) utajifunza maeneo ya kufanya uwekezaji.
SOMA; KITABU; MTAALA WA UTAJIRI.
SURA YA 4; DHIBITI MATUMIZI.
Siri kuu ya utajiri ni UBAHILI. Kwa kila kipato ambacho mtu unaingiza, hupaswi kutumia chote, badala yake unapaswa kuweka akiba na kuwekeza.
Neno UBAHILI limepewa picha ambayo ni mbaya na watu kutokupenda kufikiria kwa namna hiyo. Wengi huona ubahili ni kujitesa na kushindwa kuyafurahia maisha. Huona ina maana gani ya kujenga utajiri kama utaishia kujitesa kwa kutokutumia?
Mwandishi Ramit Sethi anaamini kwamba changamoto zetu kwenye fedha hazitokani na fedha, bali saikolojia, hisia na tabia zetu. Hata kwenye kudhibiti matumizi, tatizo siyo matumizi, bali saikolojia, hisia na tabia.
Watu hawapendi kudhibiti matumizi kwa sababu wanaona ni kujitesa. Wanataka wakipata pesa watumie vile wanavyotaka na siyo kujibana na bajeti. Ili kuvuka hilo, lazima tucheze na saikolojia yetu wenyewe.
Hapo ndipo mwandishi amekuja na MPANGO SAHIHI WA MATUMIZI, ambao unaendana na saikolojia yako. Kwa mpango huo, unakuwa huru kutumia fedha yako vile unavyotaka wewe mwenyewe, kwa sharti la kuweka akiba na kuwekeza kiasi fulani kwanza.
Yaani kwa kila kipato, unatenga pembeni kiasi unachoweka akiba na kuwekeza, halafu kile kinachobaki unakuwa tayari kutumia vile unavyotaka wewe mwenyewe, bila ya kuwa na hatia yoyote.
Kwa njia hiyo huwezi kuona kama unajinyima, kwa sababu hulazimiki kufanya au kutokufanya chochote. Wewe unahakikisha akiba na uwekezaji vimefanyika, baada ya hapo upo huru.
Mpango sahihi wa matumizi una vipengele vinne;
1. Gharama za msingi – asilimia 50 mpaka 60 ya kipato.
Hapa zinaingia gharama za msingi ili maisha yaweze kwenda.
2. Uwekezaji – asilimia 10.
Hapa unatenga kiasi kwa ajili ya kufanya uwekezaji wa muda mrefu.
3. Malengo ya akiba – asilimia 5 mpaka 10.
Hapa unatenga akiba kwa ajili ya malengo unayokuwa nayo, ya muda mfupi na mrefu, kama kujenga, kununua gari n.k.
4. Matumizi yasiyo na majuto – asilimia 20 mpaka 35.
Hapa ndiyo unakuwa huru kutumia vile unavyotaka wewe bila ya kuwa na majuto au kuona unajinyima.
Ili mpango sahihi wa matumizi ufanye kazi kwako, unapaswa kuendana na maisha yako na siyo kuiga wengine. Lazima uzingatie yale mambo unayoyapenda wewe kisha kuyapa kipaumbele zaidi kwenye matumizi yako.
Wengi sana wanakwama kwa sababu wanaiga matumizi ya wengine, yanakuwa na gharama kubwa kwao huku pia yakiwa hayawaridhishi. Kama mtu atasikiliza nafsi yake na kufanya yale anayoyapenda, ataweza kuyafurahia maisha yake kwa kipato chochote anachokuwa nacho.
Tengeneza mpango sahihi wa matumizi kwako ili uweze kuweka akiba na kuwekeza kisha kutumia vile unavyotaka bila ya majuto au kujitesa.
Masomo yote ya kujenga utajiri kutoka kitabu kinachoitwa I WILL TEACH YOU TO BE RICH kilichoandikwa na Ramit Seth yanapatikana kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.
Hapo chini ni kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu somo hili. Fungua ujifunze kwa kina na kupata shuhuda za wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.