Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya SITA ambayo ni mpe mtu nafasi ya kuongea zaidi.
Na kwenye kanuni ya SITA tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni wape watu nafasi ya kuongea zaidi, watajiona ni wa muhimu na unawathamini na hivyo kukubaliana na wewe.
SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Sita
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi yetu ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya SABA ambayo ni mfanye mtu aone ni wazo lake.
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hakuna mtu anayependa kuambiwa au kupangiwa kitu cha kufanya. Kwa sababu kila mtu huwa anaamini anajua anachopaswa kufanya.
Hivyo kama kuna kitu unataka mtu afanye, kumwambia moja kwa moja afanye haitakupa matokeo mazuri, kwa sababu ataona unamlazimisha.
Badala yake, unapaswa kumfanya aone ni wazo lake kufanya kitu hicho.
Na unaweza kufanya hivyo kwa kujua mahitaji halisi ya mtu na kisha kupendekeza ni jinsi gani anaweza kufikia mahitaji hayo.
Hapo mtu ataona amechagua mwenyewe na hivyo kuwa tayari kufanyia kazi.
Lakini pia, unaweza kufanya hivyo kwa kujiweka chini ya mwingine, badala ya kumkosoa mtu kwa kile ambacho anafanya siyo sahihi, chagua kupendekeza njia mbadala kwake kufanya.
Hapo mtu ataona ni wazo lake kuchagua na atafanya.
Tunapokuja kwenye mauzo wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, hili lina nguvu sana. Unapoongea na mteja, usikazane kumuuzia kitu, maana hakuna mteja anayependa kuuziwa.
Badala yake, msaidie afanye maamuzi sahihi ya kununua.

Kila mtu anapenda kununua, hakuna anayependa kuuziwa. Hivyo basi, jua mahitaji yake au changamoto alizonazo na kisha pendekeza njia sahihi kwake kuondokana na changamoto hizo, kwa kufanya hivyo, ataona ni maamuzi yake na kuyafanyia kazi.
Mwandishi Dale Carnegie anamnukuu mwanafalsafa Lao Tse, ambaye alikuwa ni mwanafalsa wa China ambaye aliandika hivi.
Mto na bahari huwa vinapokea maji kutoka kwenye mlima na chemchem zote kwa sababu imekubali kuwa chini ya milima hiyo na hivyo kuweza kupokea maji hayo ambayo yanatiririka kutoka juu kwenda chini.
Mtu mwenye hekima anapaswa kufanya hivyo, kama anataka kuwa juu ya watu, basi awe chini yao na kama anataka kuwa mbele ya watu hasi awe nyuma yao.
Hatua ya kuchukua leo;
Wasaidie wateja au watu kufanya maamuzi wao wenyewe kwa kuwapendekezea kitu, na siyo kuwalazimisha wafanye au wanunue badala yake wapendekezee ili wajione wamefanya maamuzi sahihi ya kununua.
Kumbuka, watu huwa hawapendi kuuziwa, ila wanapenda kununua. Kazi yako kama muuzaji bora kuwahi kutokea ni kutengeneza mazingira ambayo mteja atataka kununua.
Kwa kufanya hivi, utajenga ushawishi kwa watu na wateja wako kwa ujumla kwa kuwafanya waone ni wazo na maamuzi yake kufanya kitu hicho.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504