3414; Msimamo na kubadilika.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Msimamo ni moja ya sifa muhimu sana kwenye safari ya mafanikio.
Hakuna kitu chochote unachofanya mara moja au chache ukapata matokeo mazuri.
Ni lazima urudie rudie kufanya ndiyo utaweza kupata unachotaka.

Lakini pia kila safari ya mafanikio huwa inabadilika.
Mambo mengi huwa hayaendi kama jinsi mtu unavyokuwa umepanga.
Hivyo kuendelea na mpango vile vile ulivyouweka inakuwa ni kuzidi kujikwamisha.
Hivyo maboresho ya mpango wowote ule ni muhimu ili mpango huo uweze kufikiwa.

Kwenye maisha, ili uweze kupata chochote unachotaka, lazima ujue gharama unazopaswa kulipa na kuzilipa.
Kadiri unavyokwenda na unachukua hatua, unapaswa kujitathmini kwa juhudi unazoweka na matokeo unayotapata.

Pale juhudi unazoweka ni kubwa, lakini matokeo ni madogo, unapaswa kuchunguza nini kunasababisha hali hiyo.

Kile unachoona ndiyo kitaamua ni maboresho gani yafanyike ili juhudi zinazowekwa ziweze kuzalisha matokeo mazuri.

Kwa nadharia, msimamo ni kuwa na nidhamu kali ya kuamua na kufanya bila ya kuyumbishwa na chochote.
Hiyo ni kuchukulia kama mipango yote huwa inakwenda kama ilivyowekwa, kitu ambacho siyo.

Kwenye uhalisia, msimamo ni kuweza kubadilika na kuendana na hali. Hii inaendana vizuri na uhalisia wa maisha, ambapo mipango na uhalisia kuwa tofauti.
Hii pia inahakikisha mtu anaendelea kuchukua hatua mpaka kufika anakotaka kufika, bila ya kukwamishwa.

Unachohitaji wewe ni kuendelea kubaki kwenye njia ya kuelekea kwenye malengo uliyonayo mpaka kuyafikia.
Chochote unachopaswa kufanya ili kuwezesha hilo, ndiyo msimamo wenyewe, hata kama ni kubadilika ili kuendelea na safari.

Tunapozungumzia msimamo, siyo kwenye matukio, bali kwenye matokeo ya mwisho.
Fanya kila uwezalo ili kubaki kwenye safari ya kupata kile unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe