Rafiki yangu mpendwa,
Kupata watu sahihi wa kushirikiana nao imekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye zama tunazoishi sasa.
Hiyo ni kwa sababu watu wengi kwenye zama hizi ni wepesi kusema na kuahidi, ila kwenye utekelezaji ni tofauti kabisa.

Ukiwapa watu nafasi ya kujieleza, watajieleza vizuri sana mpaka utashawishika. Lakini inapokuja kwenye kufanya, wengi huwa ni sifuri kabisa.
Hali hiyo imekuwa inawafanya wengi kukata tamaa na kuona watu wazuri hawapatikani tena. Lakini hilo siyo sahihi, watu wazuri bado wapo, ni wewe tu hujajua njia nzuri za kuwapata.
Hapa unakwenda kujifunza sifa tatu za kuangalia kwa watu unaotaka kushirikiana nao. Kama mtu anakosa sifa hizo tatu, usijaribu kushirikiana naye, kwa sababu atakuangusha tu.
Sifa ya kwanza ni ARI.
ARI ni ule msukumo wa ndani wa mtu kufanya kitu bila ya kusubiri kuambiwa au kusukumwa kufanya. Mtu mwenye ari anafanya kile kilicho sahihi kabla hata ya kuambiwa. Na pale anapoambiwa, anafanya mara moja bila ya kusubiri kukumbushwa au kusukumwa.
Angalia watu ambao tayari wana ari ndani yao, kupitia yale ambayo tayari wanayafanya. Watu hao ndiyo unaweza kuwategemea kwenye mambo mbalimbali kwa sababu watafanya.
Sifa ya pili ni NIDHAMU.
NIDHAMU ni mtu kufanya kile anachopaswa kufanya, iwe anajisikia kufanya au hajisikii. Kila mtu anaweza kufanya kitu, lakini wengi hufanya pale wanapojisikia. Ni mara chache sana watu wakajisikia kufanya vitu ambavyo ni vigumu. Hivyo vitu vigumu huwa havifanyiki kwa sababu watu wanakosa nidhamu.
Chagua watu ambao tayari wana nidhamu ili uwe na uhakika nao katika nyakati zote. Watu wasio na nidhamu huwa wanakuangusha kwenye wakati unaokuwa unawategemea zaidi.
Sifa ya tatu ni UJASIRI.
UJASIRI ni utayari wa mtu kufanya kitu, licha ya kuwa anahofia kukifanya. Kila binadamu huwa ana hofu, kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni ujasiri. Ujasiri unampa mtu msukumo wa kufanya kile anachohofia na hivyo kumfanya aweze kufanya yale wengine hawawezi kufanya.
Chagua kushirikiana na watu wenye ujasiri kwa sababu watakupa na wewe ujasiri wa kupambania yale unayotaka kufikia. Ukizungukwa na ambao hawana ujasiri, utajikuta na wewe unakosa ujasiri.
Kwa kuwa unataka watu wengine wawe na sifa hizo tatu ndiyo ushirikiane nao, hakikisha kwanza wewe mwenyewe una hizo sifa. Kwa sababu kama utataka wengine wawe na sifa ambazo huna, haitawezekana. Huwa unaishia kuwavuta kwako watu unaoendana nao. Anza kwa kuwa mwenye ARI, NIDHAMU na UJASIRI na utaanza kuwavutia watu wenye sifa kama hizo kushirikiana na wewe.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeelezea zaidi kuhusu sifa hizo tatu za kuangalia kwa wale unaotaka kushirikiana nao. Karibu ujifunze ili uweze kuchagua watu sahihi kwako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.