Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka CHUO CHA MAUZO.
Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.
Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.
Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.
Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 35 na 36.
Kwenye mbinu namba 35 tulijifunza ukamilishaji wa kufikiria -1. Na hapa unatumia ukamilishaji huu pale mtu anapokuambia ngoja akafikirie zaidi.
Na kwenye ukamilishaji wa namba 36 tulijifunza ukamilishaji wa kufikiria zaidi -2
tulijifunza kwamba pale mtu anapokuambia ngoja akafikirie zaidi wewe mwambie fanya maamuzi sasa ili uweze kuendelea kufikiria vitu vingine vinavyohitaji umakini wako.
SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 35-36
Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 37 na 38

Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;
- Ukamilishaji wa kufikiria zaidi – 3.
Mteja amekuja kwako, anataka bidhaa au huduma fulani. Unampendekezea huduma au bidhaa lakini anakuja na pingamizi la ngoja akafikirie zaidi.
Wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, usiwe na wasiwasi, akikuambia hivyo, wewe mwambie hivi;
“Vizuri! Unadhani siku 2 mpaka 3 zitatosha kufikiria, au wiki 2 mpaka 3 ndiyo zitakutosha? (Mteja ataona siku 2 mpaka 3 ni nyingi.) Ukweli ni kwamba, haijalishi utachukua muda mrefu kiasi gani kufikiria, utakabiliana na maswali haya matatu;
1) Je bidhaa hii inakupa unachotaka?
2) Je unaweza kuimudu?
3)Je mimi ni aina ya mtu unayetaka kufanya naye biashara? Kama majibu ni ndiyo kwenye maswali hayo, weka sahihi yako hapa.” tukamilishe hili, nahitaji ulipie sasa ili uende ukafurahie uwekezaji wako.
Ukamilishaji huu una nguvu ya kumwondolea mtu sababu za kufikiria au kumfanya atoe sababu za kweli badala ya kusingizia kufikiria zaidi.
- Ukamilishaji wa kufikiria zaidi(1-10) – 4.
Kama kawaida, mapingamizi mbalimbali huwa hayakomi kwa mteja. Anakuja tena mteja kwenye kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma anakuambia sawa, nimeipenda au nimeona kile unachouza, basi ngoja nikafikirie kwanza halafu nitakutafuta baadaye.
Mteja akikuambia hivyo, wewe tabasamu na mwambie hivi;
“Vizuri, watu wengi huwa wanahitaji muda kufikiria kabla hawajafanya maamuzi. Naomba nikuulize, kwa kipimo cha 1 mpaka 10, 10 ikiwa una uhakika wa kuchukua na 1 ikiwa ni hutachukua hata iweje, upo kwenye namba ipi kwa sasa?” Akikupa jibu, endelea; “Nini kitakufanya uwe kwenye 10?”
Ukamilishaji huu una maana gani sasa kwetu kama wauzaji bora kuwahi kutokea, jibu ni kwamba ukamilishaji huu utakusaidia kujua mapingamizi sahihi kama yapo au anakuzingua tu.
Kwa kukubaliana nao kwenye kutaka kufikiria zaidi, kisha kumuuliza anakosimama sasa, inakupa nafasi ya kujua kitakachomfanya mteja anunue.
Hatua ya kuchukua leo; wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, kwa kila pingamizi unalokutana nalo kuhusu mteja kukuambia ngoja nikafikirie kwanza, mkamate kwa mbinu hizi za ukamilishaji ambazo tumetoka kujifunza. Mbinu hizo ni ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 3 na 4.
Mwisho, nenda kayafanyie kazi haya uliyojifunza leo. Kama mkamilishaji na muuzaji bora kuwahi kutokea unapaswa mwonyesha mteja matokeo mazuri anayokwenda kuyapata baada ya kuwa amenunua.
Elezea matokeo ambayo mteja atayapata baada ya kupata kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma na siyo kueleza sifa za biashara.
Lakini pia, hoji zaidi kwenye kila pingamizi analokupa mteja, mteja anakuwa na hisia tofauti nyuma yake zinazomfanya asichukue hatua. Kwa sababu kwenye kila hisia kuna mabadiliko.
Hivyo watu hawapendi mabadiliko hivyo unapokuwa unajua hisia za mteja utaweza kumshawishi kununua kile anachouza kwa sababu kinachowasukuma watu kununua ni hisia walizokuwa nazo na kwenye hisia za mteja kuna mabadiliko ndani yake na watu huwa wanaogopa kuchukua hatua juu ya mabadiliko mapya watakayokwenda kukutana nayo kupitia bidhaa au huduma unayotoa. Kwa mfano, wewe unauza simu, na mteja anahitaji kweli lakini akifikiria mabadiliko anayokwenda kukutana nayo, kutumia simu mpya ili hali alishazoa kutumia simu yake ya zamani hivyo wewe kama muuzaji ukiweza kumwondolea mteja wako wasiwasi atachukua hatua kupitia kile unachouza.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505 //0767101504