Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka kwenye programu yetu ya  CHUO CHA MAUZO.

Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.

Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.

Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 37 na 38.
Kwenye mbinu namba 37 tulijifunza ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 3
Na kwenye ukamilishaji wa namba 38 tulijifunza ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 4.

Na kwenye ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 3 na mbinu ya 37 na 38  tulijifunza kwamba mteja akikuambia nahitaji kufikiria zaidi, mwambie fanya maamuzi sasa ili uweze kuendelea kufikiria vitu vingine vinavyohitaji umakini wako.
Tukamilishe hili.
Kwa kutumia ukamilishaji huu, mteja anasukumwa kufanya maamuzi mara moja badala ya kutumia kufikiri kama kisingizio cha kutokununua.

SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 37-38

Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 39 na 40

Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;

39. Ukamilishaji wa kufikiria zaidi – 5.

Mteja anakuja anaonesha nia ya kutaka kununua kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma unayotoa, inapofika kwenye hatua ya kukamilisha malipo, anakuambia sawa nimeipenda au nimeona ngoja nikafikirie kwanza.

Mteja apokuambia hivyo, unapaswa kumjibu kwa namna hii.
“Naelewa, na mimi kama mteja nimewahi kusema hivyo, wakati ambapo…
a) sikutaka kumkabili muuzaji, b) sikutaka kumwangusha,
c) kulikuwa na mambo sijayaelewa.
Ipi sababu yako?”

Kwa ukamilishaji huu, unachukua muda kuonyesha unaelewa kisha unachimba kujua sababu halisi. Kutumia aina hizi za ukamilishaji unapaswa kuamini kwamba wanaweza kununua, hivyo unawauzia badala ya kukubali wao wakuuzie sababu.

40. Ukamilishaji wa kurudia uwasilishaji/maonyesho.

Wakati mwingine mteja anakuja, anakuambia nahitaji bidhaa fulani, unampatia anaiona lakini anakuwa bado kama vile hajakuelewa. Pale mteja anapokuwa anataka kuondoka tu, unatumia hii mbinu ya ukamilishaji wa kurudia uwasilishaji au maonyesho.
Unamwambia mteja;

“Njoo uone – nataka kukuonyesha jinsi ulivyo karibu na kufanya maamuzi bora kabisa kwako na utakayoyafurahia maisha yako yote.”
( Hapa sasa rudia kueleza/kuonyesha faida za kile unachouza au huduma unayotoa ni kwa namna gani inakwenda kumuondolea maumivu aliyokuwa nayo.

Huu ni ukamilishaji muhimu kutumia. Watu wananunua bidhaa/huduma na siyo bei. Rudi kwenye bidhaa/huduma na eleza sifa na manufaa yake kisha kamilisha mauzo. Kuwa na shauku kubwa juu ya kile unachouza na wape wakijaribu, hilo litawashawishi zaidi.

Tunajua nguvu ya mfano au maonyesho yalivyo na nguvu kwa mteja. Unapaswa kumpa mteja ajaribu kama ni kitu ambacho kinaweza kujaribiwa au kuoneshwa kwa mfano.
Lengo la mbinu hii ni kumpa umiliki mteja wa kile unachotaka kumuuzia, kama ni nguo unampa kazi avae na atakapoona ameivaa na imempendeza atajisikia vizuri sana na kuinunua na siyo kurudisha.

Hatua ya kuchukua leo; tumia ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 5 pale unapokutana na mteja anakuambia ngoja nikafikirie kwanza. Mkamte kwa kutumia mbinu hii badala ya kukuzuia sababu, mshawishi kutumia ukamilishaji huu kuweza kumuuzia.

Tumia ukamilishaji wa kurudia uwasilishaji au maonyesho. Mpe mtu mfano au ajaribu. Mithali ya Kichina inasema, onyesho moja ni zaidi ya maneno elfu moja.
Hivyo basi, kama kitu kinaweza kuonyeshwa hupaswi kuelezea kwa maneno matupu.

Mwisho, maonyesho au majaribio yanawashawishi wateja zaidi kununua kuliko maelezo matupu. Unapoweza kumhusisha mteja kwenye maonyesho au majaribio ushawishi unakuwa mkubwa zaidi. Kwa chochote unachouza, hakikisha unafanya maonyesho au majaribio ambayo mteja anahusika moja kwa moja.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505 //0767101504