Habari njema muuzaji bora  kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya KUMI NA MBILI  ambayo ni WAPE WATU CHANGAMOTO.

Na kwenye kanuni ya KUMI NA MBILI tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni; kama unataka kuwashawishi watu wakubaliane na wewe basi wape changamoto.
Weka hali ya ushindani kwenye kile unachotaka kuwashawishi watu na watakuwa tayari kukifanya.
Kwenye biashara unayofanya wape wateja wako changamoto ya kufanya manunuzi makubwa. Wape namba kwamba atakayefikia manunuzi ya kiasi fulani kwenye biashara, atapata zawadi fulani.
Utashangaa watu watakapopambania kufanya manunuzi makubwa.

Tumehitimisha masomo ya jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako ambapo mpaka sasa tayari tumejifunza kanuni kumi na mbili.

SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Kumi Na Mbili

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki ambayo ni kuwa kuwa kiongozi kanuni ya kwanza ambayo ni anza kwa kusifia.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Kazi ya kiongozi ni kuwashawishi watu wengine kufanya vitu ambavyo wanaweza kuwa hawataki kuvifanya, lakini vina manufuu kwao.
Kwa mfano, watu ni wavivu kupiga simu kwa wateja licha ya kuwa hawapendi kufanya hivyo lakini ni kitu ambacho kina manufuu kwao.

Uongozi ni ushawishi, bila ya ushawishi uongozi unaishia kuwa wa mabavu. Kwa mfano, Mtume Mohammad na Yesu ni miongoni mwa watu ambao walikuwa na ushawishi mkubwa kiasi cha kutuvuta hata sisi leo kwenye imani ambazo tunazo leo.
Mmoja wa viongozi ambaye alikuwa anatumia sana mabavu katika uongozi wake, ambaye ni aliyekuwa mtawala wa Ufaransa na jemedari wa kijeshi Napoleon Bonaparte aliwahi kunukuliwa akisema, niliwavuta watu wangu kwa mabavu lakini Yesu aliwavuta watu wake kwa upendo.
Hapa tunajifunza kwamba uongozi siyo mabavu bali ni ushawishi.

Kama kiongozi utahitaji kuwabadili watu na wakati mwingine kuwarekebisha pale wanapokosea.

Hayo siyo mambo rahisi, wengi wanapojaribu kuyafanya huwa wanaishia kuibua hasira na chuki kwa wengine.

Kwenye sehemu hii nyingine ya ushawishi, tunakwenda jinsi unavyoweza kuwashawishi, kuwabadili na kuwarekebisha watu bila hata ya kuibua chuki au hasira ndani yao.

Na kanuni ya kwanza ni anza kwa kusifia.

Kama kiongozi kuna wakati utahitaji kutoa taarifa mbaya kwa wengine, labda ni mahali wamekosea au kufanya vibaya.
Ukiwakabili watu na kuwapa taarifa hizo mbaya moja kwa moja, hawatazipokea vizuri na watatafsiri hilo vibaya.

Njia sahihi ya kutoa taarifa za aina hiyo ni kuanza na kitu cha kusifia kwa mtu huyo.
Kama ni kazi, anza kusifia yale maeneo ambayo ni mazuri. Na baada ya sifa ndiyo unaweza kueleza maeneo ambayo siyo mazuri.

Na pia katika kueleza maeneo hayo yasiyo sahihi, usieleze kama makosa tu, badala yake eleza kama maeneo yanayoweza kuboreshwa zaidi.
Kwa mfano hapa, usimfie mtu kisha ukasema lakini.
Hongera kwa kupendeza lakini viatu vyako ni vichafu.
Neno lakini linakuwa limefuta kila kitu. Badala ya kusema lakini tumia na. Kwa mfano, hongera Juma kwa kupendeza leo na ukinyoa ndevu zako utapendeza zaidi.

Hapo umemsifia na kumtaka kumshawishi kubadilika pasipo hasira au chuki. Hapo Juma atajisikia vizuri sana, kumbe nimependeza na nikinyoa ndevu zangu nitapendeza zaidi atapata hamasa ya kwenda kunyoa ndevu ili aonekane akiwa amependeza zaidi.

Muuzaji bora kuwahi kutokea, unapoenda kwa daktari wa meno kung’olewa meno, huwa anaanza na kukuchoma ganzi kabla ya kukung’oa jino.
Ganzi inapunguza maumivu unayopata wakati wa kung’olewa jino.

Hali kadhalika unapomsifia mtu kabla ya kumweleza alipokosea au kuharibu, unakuwa umempa ganzi itakayopunguza maumivu ya taarifa anayokwenda kupokea.

Kwenye mauzo tumia mbinu hii kwa wateja wako, kabla hujawataka wanunue kile unachouza iwe ni huduma au bidhaa.

Kumuuzia tu mteja bila kumsifia ni kama kutaka kung’oa jino lake bila ganzi.
Mauzo ni vita isiyoruhusu umwagaji wa damu. Na kutoa hela kunauma ni kama kung’oa jino.
Kabla hujamtenganisha mteja na fedha zake, mchome kwanza sindano ya ganzi ambayo ni kumsifia kwanza.

Tafuta kitu chochote ambacho umekiona ni kizuri kwa mteja na msifie kutoka ndani ya moyo wako kabisa. Hata kama alikuwa hataki kununua kitendo tu cha kumsifia unakuwa umemshawishi akupe fedha zake alizozipata kwa shida.

Wewe ni Muuzaji bora kuwahi kutokea na moja ya kazi ya muuzaji ni kumsaidia mteja kufanya maamuzi. Uuzaji ni ushawishi na siyo mabavu. Na muuzaji ni kiongozi nenda kawe kiongozi bora kwa kuwashawishi wateja wako kufanya vitu ambavyo wanaweza kuwa hawataki kuvifanya lakini vina manufuu makubwa kwao. Kwa mfano, wewe una bidhaa au huduma bora, ambayo unaamini kabisa kwamba mteja akipata bidhaa au huduma yako itakwenda kufanya maisha yake kuwa bora na kupata manufuu makubwa.

Mshawishi mteja anunue kwa kumsifia kwanza kabla ya kumwambia anunue.
Kumbuka watu ni wabinafsi, hivyo anza kujali maslahi yao kwanza. Kumbuka sisi ni viumbe vya hisia, unapoanza kuteka hisia za mtu, inakuwa ni rahisi kumshawishi kununua kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.
Chukulia mtoto wako hataki kula chakula utaanza kumkosoa ili ale chakula? Utaanza kwa kumsifia na kumbembeleza kidogo ili aingie laini na kisha kushawishika kula yeye mwenyewe.

Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504