Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya 5 ambayo ni USIMKOSOE MTU MBELE YA WENGINE
Na kwenye kanuni hiyo ya TANO tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;
Mtu anapokosea, hata kama ni kosa la wazi, usimkosoe mbele ya wengine. Badala yake muite mtu faragha na kisha mweleze jinsi anavyoweza kuboresha zaidi.
Wasifie watu hadharani lakini wakosoe faraghani. Kumbuka kuwakosoa wale ambao wanakulipa au wanawajibika kwako moja kwa moja na nje ya hapo achana nayo kwa sababu wewe siyo kiranja wa dunia. Jali mambo yako au biashara yako ndiyo kitu muhimu zaidi.
SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Tano
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya SITA ambayo ni ; Tafuta Kitu Cha Kusifia.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Wanasaikolojia wanatufundisha njia mbili za kuwabadili watu ambazo ni zawadi na adhabu. Watu huwa wanafanya kile wanachosifiwa kufanya na kuacha kile wanachoadhibiwa wakifanya. Lakini katika njia hizi mbili, zawadi ina nguvu kuliko adhabu.
Pale unapotaka kuwabadili watu, angalia kitu kizuri wanachofanya kisha sifia hicho. Kwa kuwa watu wanapenda sifa, watafanya hicho ulichowasifia. Pendelea kuwa mpelelezi wa kuchunguza vile ambavyo watu wanavipenda. Angalia kupitia mitandao yao ya kijamii, huwa wanashirikisha vile wanavyopenda. Kwa kujua kile ambacho mtu anafanya au anapenda hata ukimpa sifa unakuwa umepiga kwenye maumivu.
Kwenye kitabu chake cha how I raised myself from failure to success in selling, mwandishi Frank Bettger anatushirikisha jinsi siku moja alivyokutana na wakili mmoja na kumshawishi akate bima ya maisha. Licha ya kuwa na mazungumzo marefu na wakili huyo, lakini alishindwa kumshawishi kukata bima ya maisha.
Sasa wakati wanaagana, mwandishi Bettger alitumia mbinu ya kutafuta kitu cha kusifia na akamwambia, Mr Barnes ninaamini una kesho kubwa sana mbele yako. Kamwe sitokusumbua, lakini kama hutajali , mara kwa mara nitakuwa ninakuwa nawasiliana na wewe.
Baada ya kusema maneno hayo, wakili yule alimuuliza kwa shauku kubwa, “una maanisha nini unaposema nina kesho kubwa? Kwa namna alivyouliza, Bettger alijua ameona anamsifia tu uongo. Na akamjibu akamwambia,; ‘’ wiki chache zilizopita nilikusikia ukiongea kwenye mkutano na nadhani ulitoa hotuba bora sana kuwahi kusikia. Hayo ni maoni yang utu, natamani ungesikia mambo mazuri ambayo wengine walisema kuhusu wewe kwenye mkutano huo.
Baada ya kusikia maneno hayo, yule wakili alifurahi na kuanza kujieleza namna alivyoingia kwenye uneni na jinsi ambavyo amepiga hatua. Aliongea kwa muda mrefu na mwisho akisema, Mr. Bettger unakaribishwa kuniona muda wowote.
Hapa tunajifunza kwamba, ukianza kwa kusifia unamfanya mteja ajisikie vizuri kitu ambacho kitapelekea wewe kupata ushindi kwenye kile unachotaka mkubaliane.
Ziko namna nyingi za kuwasifia watu hata kama kwa macho umekosa cha kusifia. Habari njema ni kwamba uzuri wa kitu upo machoni pa mtu. Hivyo mtu anapokuwa anasifia ukweli kutoka ndani ya moyo kabisa, mhusika anakuwa anajisikia vizuri kiasi cha kukubaliana na wewe. Kwa hiyo, namna nyingine ya kumsifia mtu na kuweza kujielezea yeye mwenye na kujisikia vizuri ni kumuuliza, uliwezaje kuanza biashara yako? Hili swali ambalo watu wengi wanapenda kuulizwa ila hawaulizwi.
Swali linawanya watu wajieleze namna walivyoanza na mpaka pale walipo sasa. Katika kujieleza kwa watu, wewe ndiyo unapata sasa mambo ya kweli ya kuwasifia au kuwatia moyo. Na watakuamini na kukuona wewe ni rafiki yao wa kweli.
Kumbuka, hakuna kitu ambacho watu wanapenda kama kuthaminiwa, kusifiwa na kutiwa moyo kwenye kile wanachofanya. Hilo linapofanyika kwa ukweli kabisa kutoka ndani ya moyo wa mtu, anayelengwa anajua na anashawishika zaidi. Huwa tunasikia kwamba watu wanakufa kwa kukosa chakula. Lakini nikuambie kitu, watu wengi zaidi wanateseka na njaa ya kukosa kuthaminiwa, kusifiwa na hata kutiwa moyo.
Kadiri unavyoonekana kukumbuka mambo muhimu ya watu, ndivyo wanavyokuamini, kuvutiwa na kushawishika na wewe. Hii ndiyo nzuri ya kujenga na kutunza urafiki na wengine. Wasaidie watu kuona mafanikio makubwa ambayo yapo mbele yao.
Usiwe mtu wa kuwakosoa watu kama wengine wanavyofanya. Wengi hukimbilia kuwakosoa watu na kutokuwa tayari kuwasifia. Wewe kuwa kinyume, penda kuwasifia watu na epuka kuwakosoa. Watu watakuwa tayari kukubaliana na wewe lakini pia kushirikiana na wewe
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504