Umeweka malengo ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa muda mrefu na hatiyame muda umefika, umejipanga vya kutosha na una kilakitu kinachohitajika ili uweze kupanda mlima huo. Ni ndoto kubwa sana uliyokuwa nayo na hatimaye sasa unaelekea kuikamilisha. Mmeanza safari ya kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika, mmefika katikati ya safari hali ya hewa inabadilika ghafla wingu zito na mvua kubwa, baridi ni kali sana na hata mbele hakunekani kutokana na ukungu ulitanda. Je utang’ang’ania kuendelea kupanda ili kutimiza malengo uliyojiwekea kwa muda mrefu ama utarudi ujipange kwa safari nyingine? Ni bora kurudi na kujipanga kwa safari nyingine kuliko kung’ang’ania na kuishia kupoteza maisha kutokana na mazingira hayo magumu.

  Mfano huo hapo juu upo kwenye kila nyanja ya maisha yetu, kuna vitu tunakuwa tumejipanga vizuri kabisa kuvifanya ila mambo fulani yanatokea na inashindikana kukamilisha mipango yetu. Katika hali kama hiyo huwezi kusema umeshindwa, wala hupaswi kujilaumu bali kuangalia jinsi ya kufanya kwa wakati mwingine ukitumia na uzoefu ulioupata.

  Maisha hayana ramani iliyo kamili, hakuna kitu ambacho tuna uhakika nacho kwa asilimia 100. Hakuna anaeijua kesho hivyo tegemea chochote kinaweza kutokea.

  Unapopanga mipango yako weka nafasi ya kinachoweza kutokea ambacho hakipo kwenye mpango wako. Hiyo itakusaidia kutoumia sana pale kinapotokea kitu ambacho hukutarajia.

  Pamoja na yote yanayoweza kutokea maisha yanaendelea hivyo usilazimishe kufanya jambo ambalo linaweza kukatisha maisha yako, zipo njia nyingi za kufanya mambo, ikishindikana moja basi tafuta nyingine.