Una mawazo mengi sana, na asilimia kubwa ya mawazo hayo ni mazuri mno. Mazuri kiasi kwamba ukiyatekeleza yanaweza kubadili maisha yako na ya wanaokuzunguka. Nini kinakuzuia mpaka sasa hujatekeleza mawazo hayo? Ni nini kinakuzuia hata kuanza utekelezaji?
Ardhi imebeba mawazo mengi mazuri sana ambayo hayakupata nafasi ya kutekelezwa duniani. Na wengi tunatembea na mawazo mpaka yanapotea na tunapata mengine nayo yanapotea bila ya kufanyiwa utekelezaji.(soma; jinsi unavyopoteza mawwazo yako)
Nimekuwa nikizungumza na watu wengi, na wengi wanamawazo mazuri sana. Lakini kwa nini hatuyatekelezi mawazo yetu mazuri? Sababu kuu tunayotoa ni kwamba hatujajiandaa vya kutosha. Tunataka tuandae kila kitu ili tutakapoanza utekelezaji tusikumbane na changamoto nyingi. Tunapenda kuwa sahihi kabla hatujaanza ili tusishindwe maana tunaogopa sana kushindwa.
Ni vizuri sana kujiandaa vya kutosha kabla ya kuanza kufanya jambo lolote. Ila kama maandalizi yanakufanya usianze hata kulifanya hilo jambo hayana maana yoyote. Kama ukitaka kusubiri mpaka kila kitu kikamilike ni dhahiri hutoanza kutekeleza mawazo yako, na hii ndio inayowatokea wengi.
Anza na vichache ulivyonavyo, huku ukiendelea kujifunza na kupata uzoefu zaidi. Anza kwa kitu kibaya kisha fanya marekebisho mpaka utakapopata kitu kizuri. Kwa njia hii inakuwa rahisi sana kutekeleza mawazo yako kwa sababu unajijengea udhubutu mkubwa na unazizoea changamoto.
Kama umebahatika kuandaa kila kitu na kwa usahihi kabisa, ukaanza, changamoto zikajitokeza(na ni lazima zijitokeze) utavunjika moyo sana tofauti na alieanza bila ya kukamilika. Hii inatokana na wewe kuweka imani yako kubwa kwenye usahihi na hivyo dalili za kushindwa zinapojitokeza unajiona bado haukuwa sahihi na inakuwa rahisi kwako kukata tamaa.
Unapoanza bila ya kukamilika ama kuwa sahihi unajua kabisa kwamba changamoto ni nyingi utakazokutana nazo na hivyo zinapojitokeza inakuwa rahisi kwako kuzikabili. Kwa kuzikabili changamoto kunaongeza uelewa wako kwa jambo unalolifanya na sio rahisi kwa wewe kuvunjiaka moyo na kukata tamaa.
Unapoanza bila ya kukamilika pia inakusaidia sana kukabiliana na changamoto ambazo zilikuwa zinakutisha kabla ya kuanza. Mara nyingi kabla ya kuanza kufanya jambo kuna changamoto nyingi tunaziona tukiwa nje, kama ukiwa mtu wa kupenda usahihi unaweza kutumia muda mwingi kutafuta suluhisho la changamoto hizo na bado usipate. Kwa kuanza ni rahisi kukabiliana na changamoto na mara nyingi inakuwa rahisi kukabiliana na changamoo unayokutana nayo kuliko ya kufikiri.
Acha kusubiri kuwa sahihi, kinachojali sio usahihi bali kuanza. Anza kwa vidogo ulivyonavyo na itakuwa rahisi kwa wewe kukua. Naposema uanze simaanishi uanze tu kama kichaa ila uanze kwa malengo na mipango itakayokufikisha kule unakotaka kufika. Cha msingi ni kutokwamishwa na maandalizi na kutaka usahihi.