Tatizo la ajira hapa Tanzania limeshakuwa kubwa na siku zinavyozidi kwenda tatizo linazidi kukua zaidi. Wapo wanaolifananisha tatizo hili na bomu lililoteguliwa na siku moja litalipuka. Pamoja na tatizo hili kuwa kubwa, maandalizi kwa kila anaehusika hayapo ama yapo kidogo sana.
Wenye mamlaka ya kushughulikia tatizo hili wamelala na hawajastushwa na ukubwa wa tatizo. Walioko kwenye ajira wameshakuwa watumwa na wengi wanashindwa kutoka hata kama mambo sio mazuri. Wanaojiandaa na wanaotafuta ajira bado wako kizani na hawajui upande wa pili nini kinaendelea.
Katika kipindi hiki waajiri wako kwenye neema kubwa kwa sababu upatikanaji wa wafanyakazi hata wa bei rahisi sio tatizo kwao.
Ukiangalia hali yote kwa ujumla wanaoumia ni waajiriwa na wanaoumia zaidi ni wale wanaoandaliwa kuingia kwenye soko la ajira. Maana hawa wanamatumaini makubwa ambayo ni vigumu sana kufikiwa kwa mazingira yalivyo sasa.
Kama umeajiriwa, unatafuta ajira ama unaandaliwa kuingia kwenye soko la ajira kuna hesabu rahisi sana za ajira ambazo unatakiwa kuzijua.
Kwa wastani wa sasa, kila mwaka vyuo vikuu na vyuo mbalimbali nchini vinatoa wahitimu zaidi ya elfu hamsini. Hao wote wanaingia kwenye soko la ajira kwa wakati mmoja. Idadi ya wafanyakazi wanaokufa na wanaostaafu hawazidi elfu kumi kwa mwaka. Idadi ya ajira rasmi zinazozaliswa kwa mwaka hazizidi elfu kumi. Kwa kuzifatilia hesabu hizo kwa makini kuna zaidi ya wahitimu elfu thelathini ambao watakuwa wanakosa ajira kila mwaka kwanzia mwaka huu.
Hesabu hizi zinatufundisha nini?
1. Kama upo kwenye ajira ni vyema kuelewa ajira hazina tena heshima iliyokuwepo kipindi cha nyuma wakati wataalamu walikuwa wachache. Kila siku mazingira ya kazi yanakuwa magumu na kila kukicha makampuni mbalimbali yanapunguza wafanyakazi. Hivyo ni vyema kujipanga kama unataka kusalia kwenye ajira(soma; jinsi ya kulipwa zaidi) ama ni wakati muafaka wa wewe kuingia upande wa pili wa kujiajiri.
2. Kama ndio unaandaliwa kuingia kwenye soko la ajira ama kama ndio unatafuta ajira unatakiwa kujua kabisa kwamba nafasi za ajira ni finyu(soma; kabla ya kuzunguka na bahasha). Waliopo hawatoki na hakuna nafasi nyingi zinazozalishwa, hivyo kujiandaa kujiajiri kunaweza kukusaidia sana kutoka kwenye hali hii.
3. Kwa yeyote ambae ajira inamsumbua, kama yupo kwenye ajira ama ndio anatafuta ajira, kujiajiri ndio kimbilio kubwa kwa sasa. Fursa zipo nyingi ila kabla hujajiajiri kuna vitu vya muhimu unatakiwa kujiandaa.
Kwanza elewa tofauti ya kuajiriwa, kujiajiri na kutokuwa kwenye ajira kabisa(bonyeza kusoma)
Pili zijue tabia zitakazokukwamisha unapojiajiri(bonyeza kusoma)
Tutumie elimu tulizopata, uwezo na vipaji vyetu kuweza kujikwamua kwenye tatizo hili kubwa la ajira. Tuache kuweka mategemeo makubwa kwa watu wengine, tuache kuyakabidhi maisha yetu mikononi mwa wengine. Tuna haki ya kuamua tuishi vipi, na tuna uwezo mkubwa wa kuishi maisha tunayotaka.
Reblogged this on Jicho la ujasiriamali and commented:
HESABU NDOGO ZINAKUSHINDA EBU TWENDE SAWA HAPA
LikeLike