Niliposikia mpango mpya wa serikali wanaouita ‘Big Result Now’ nilishangazwa sana na mpango huu. Yaani serikali inawaaminisha wananchi kwamba inawezekana kabisa kupata MATOKEO MAKUBWA SASA kwenye sekta ya elimu.
brn
  Lengo la makala hii sio kuchambua huo mpango wa Big Result Now. Na wala sio kuangalia kama unawezekana au hauwezekani, ila baada ya kusoma mpaka mwisho unaweza kuhukumu mwenyewe kama kuna uwezekano wa kupata matokeo makubwa sasa.
  Wakati nashangaa mpango huu wa big result now nilijiuliza maswali machache ya msingi. Swali moja la msingi nililojiuliza ni nini kiliwasukuma viongozi wetu kuja na mpango huu?
  Baada ya kufikiria kwa muda na kuyaangalia mazingira nilipata jibu moja rahisi, hawa viongozi wanatoka miongoni mwa watanzania na watanzania wengi wanapenda vitu vya haraka haraka. Kwa kuwa watanzania tunapenda vitu vya haraka haraka waliotengeneza mpango huu walijua kabisa utawaingia watu haraka na hivyo kuonekana ndio suluhisho kuu la mfumo mbovu wa elimu tulionao.
  Asilimia kubwa ya watanzania tunapenda matokeo ya haraka. Tena hata kwenye hiyo haraka bado tunaona yanachelewa. Hata wewe unapenda sana matokeo ya haraka haraka.
  Unafikiri wewe hupendi matokeo ya haraka? Soma hapa na uyachunguze maisha yako, utajikuta jinsi unavyotekeleza mpango wa Big Result Now kwenye maisha yako mwenyewe.
  Hizi hapa ni TABIA TANO zinazopendelewa na watanzania wengi ambazo ni utekelezaji wa Big Result Now kwenye maisha yao.
1. Kung’ang’ania ajira hata mambo yanapokuwa magumu. Kuna watu wengi wanang’ang’a ajira hata kama mambo ni magumu sana kwenye ajira na anao uwezo wa kujiajiri ama kufanya biashara zake mwenyewe. Sababu kuu ni kwenye ajira kila mwisho wa mwezi una uhakika wa kulipwa mashahara hata kama ni kidogo, ila unapofanya kazi zako mwenyewe huna uhakika huo.(soma; sababu inayokufanya ushindwa kuondoka kwenye ajira)
2. Kupenda sana kuchangia sherehe kuliko mambo ya msingi. Watu wako radhi kuchanga fedha nyingi kwenye harusi ila ukimwambia achangie elimu ama afya anakupa sababu lukuki. Kwa nini? Unapochangia sherehe una uhakika siku sio nyingi utahudhuria kwenye sherehe na utapata huduma nzuri, unapochangia elimu kuyaona mtunda ya mchango wako inachukua muda mrefu.
3. Kupenda hela za haraka haraka. Ukitokea mchezo wowote wa hela ama unaoshawishi watu kupata hela nyingi kwa muda mfupi basi watanzania wengi tunajikuta tunacheza michezo hiyo. Jikumbushe sakata la DECI na mabilioni ya Kikwete.
4. Kupenda sana starehe na ulevi. Sababu kubwa ya watu kuwa walevi wa kupindukia ni kutafuta furaha ya muda mfupi. Unakuta mtu anakunywa pombe kwa kujifariji kwamba anapunguza mawazo ama anayasahau matatizo yake kwa muda. Hataki kujisumbua kutumia muda kutafuta suluhisho la kudumu bali yeye anakunywa pombe ama kutumia mihadarati ili kupata furaha ya haraka na ya muda mfupi. Kama hii sio Big Result Now ni nini?
5. Wizi, ufisadi na kudhulumu. Asilimia kubwa ya watanzania ni wezi na mafisadi. Kila mtu ana njia yake ya kuiba, kufisadi ama kudhulumu wengine kwenye kazi yake anayofanya. Rushwa kwa sasa imetapakaa karibu kila sekta hapa nchini. Sababu kuu ni nini? Mtu anataka afanye kazi miaka mitano awe na nyumba, magari, asomeshe watoto shule za kimataifa na wakati mshahara ni kidogo. Ili kutimiza ndoto yake ya Big Result Now inambidi aibe ama achukue rushwa ili kufanikisha malengo yake.
  Kuna mengi sana hapo yamekuhusu, unachotakiwa kujua ni kwamba hakuna jambo zuri linaloweza kutokea kwa HARAKA. Kila jambo linahitaji muda na maandalizi ya kutosha ili kuweza kupata mafanikio ya kweli. Wengi waliotafuta mafanikio kwa njia za haraka hawakuweza kunufaishwa na mafanikio yao.
success
  Badilika sasa na acha kuitekeleza sera mbovu ya Big Result Now kwenye maisha yako.
  Wanasema hata mbuyu ulianza kama mchicha kuonesha kwamba vitu vinaanza kidogo na baadae kuwa vikubwa sana. Nikuongezee usemi mmoja HUWEZI KUWABEBESHA WANAWAKE TISA MIMBA MOJA ILI WAJIFUNGUE BAADA YA MWEZI MMOJA. Hakuna njia ya kufupisha ubebaji mimba na hata kukua kwa binadamu. Vivyo hivyo hakuna njia ya kufupisha mafanikio na kuwa ya haraka sana.