Kuna vitabu vingi sana vimeandikwa kuhusu maendeleo binafsi ya mtu. Kitabu cha Napoleon Hill, Think And Grow Rich kimekuwa ni kitabu cha kipekee sana kwenye eneo hili. Kitabu hiki kimeandikwa zaidi ya miaka 70 iliyopita ila mpaka leo bado watu wanakisoma na kujifunza mambo mengi.

think and grow

  Watu wengi waliofanikiwa sana duniani wanatoa shuhuda za jinsi kitabu hiki kimewasaidia kufikia mafanikio yao. Kitabu hiki kimekuwa maarufu sana na kila aliyekisoma na kutumia mafundisho yake ameweza kuona mabadiliko makubwa kwenye maisha yake.

  Sababu kubwa ya kitabu hiki kuwa maarufu sana ni kuonesha kwamba mafanikio na utajiri sio bahati wala haihusiani na imani fulani. Mafanikio na utajiri vinakuja kwa mtu aliyeamua na kujipanga kufaikiwa.

  Kitabu hiki ni tofauti na vitabu vingine kwa sababu Hill aliwahoji watu zaidi ya mia tano waliokuwa wamefanikiwa sana kwa kipindi hicho nchini marekani. Na alifuatilia maisha yao kwa zaidi ya miaka ishirini ndipo akatengeneza sheria za mafanikio ambazo amezieleza kwenye kitabu hiki.

  Licha ya kitabu hiki kubeba jina linalomaansisha utajiri hakitoi mafunzo ya kupata utajiri tu bali mafundisho yake yanaweza kukusaidia kufanikiwa kwenye uongozi, kazi zako za kawaida, familia na hata maisha ya kawaida. Ni kitabu ambacho kinabadili mtazamo na kukuonesha kwamba lolote linawezekana kama kweli utaamua na kuweka mipango ya kufikia.

  Katika ukurasa mmoja kwenye kitabu hiki Hill anaelezea hatua sita za kubadili wazo la utajiri kwenye utajiri wenyewe. Hatua hizo ni;

1. Weka kwenye akili yako kiwango cha fedha unachotaka, usiseme unataka fedha nyingi, weka kiwango kwa namba.

2. Jua ni kitu gani utakachotoa ili kupata kiwango hicho cha fedha, hakuna kitu cha bure.

3. Weka tarehe ambayo unataka uwe tayari umeshapata kiasi hiko cha fedha.

4. Andaa mpango wa kile ulichokusudia kufanya ili kupata fedha hizo na anza mara moja. Anza kutekeleza mipango hiyo hata kama hujajiandaa vya kutosha.

5. Andika vyote ulivyofanya hapo juu, kiwango cha fedha, tarehe ya kupata, utakachofanya ili kupata fedha hizo na mpango mzima wa kupata fedha hizo.

6. Soma maelezo uliyoyaandika mara mbili kwa siku, asubuhi kabla ya kuianza siku na usiku kabla ya kulala. Wakati unasoma pata hisia na amini tayari unamiliki kiasi hiko cha fedha.

  Kitabu hiki kina mengi sana ya kujifunza. Kama mpaka sasa hujakisoma kisome na kama umeshakisoma kisome tena na tena ili kupata mambo haya mazuri.

  Kupata kitabu Think And Grow Rich cha Napoleon Hill tafadhali bonyeza maandishi ya kitabu kwenye email uliyotumiwa kwa wale ambao wapo kwenye mtandao huu.  Kama haupo kwenye mtandao huu bonyeza hapa na uweke email yako kisha utatumiwa kitabu hiki na vingine vingi.

  Endelea kuwa kwenye mtandao huu wa AMKA MTANZANIA uendelee kupata mambo mazuri. Pia waalike marafiki zako nao wapate mambo haya mazuri kwa kuwashirikisha ujumbe huu.

  Kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.