Unazikumbuka newton laws of motion? Kama ulisoma somo la fizikia utakuwa umekumbuka kidogo sheria hizi za mwendo zilizowekwa na mwanasayansi aliyejulikana kama Isaac Newton. Sina lengo la kukurudisha darasani, ila leo nataka tuangalie jinsi tunavyoweza kutumia sheria hizi kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yetu.

Kwa wale ambao hawajui au hawakumbuki ni nini nazungumzia hapa, Newton alikuwa mwanasayansi ambaye aligundua vitu vingi sana vinavyokwenda kwa sheria za asili, kwa mfano kwa nini ukirusha kitu juu kinarudi chini. Na pia alitoa sheria tatu za mwendo ambazo hazijawahi kubadilika na hazitakuja kubadilika.

ACTION_thumb[1]

Jinsi sheria hizi za mwendo zisivyobadilika ndivyo na sheria za mafanikio zisivyobadilika. Bila ya kukuchosha naomba twende moja kwa moja kwenye sheria hizi tatu.

Sheria ya kwanza; Sheria ya utulivu(law of inertia)

Sheria hii inasema kitu chochote ambacho kipo kwenye hali ya utulivu kitaendelea kuwa kwenye hali hiyo kama hakuna nguvu yoyote itakayokifanya kiondoke kwenye hali hiyo. Kwa mfano ukiweka kitabu juu ya meza kitakaa hapo miaka nenda miaka rudi mpaka nguvu itakapowekwa kukiondoa au kukisukuma.

Unatumiaje kwenye mafanikio? Hivyo ulivyo utaendelea kuwa hivyo hivyo kama hutatumia nguvu yoyote kubadili hali uliyonayo sasa. Kama kila siku unaamka unakwenda kufanya kazi, unarudi unapumzika unalala utaendelea hivyo hivyo kuwa na maisha yasiyokuwa na mafanikio mpaka utakapoweka nguvu kubadili hali hiyo. Moja ya nguvu unazoweza kuweka sasa na kubadili maisha yako ni kuweka malengo makubwa na kuanza kuyatekeleza. Bonyeza hapa kujua zaidi.

Sheria ya pili; Sheria ya mwendo kasi(law of momentum)

Sheria hii inasema kitu chochote ambacho kipo kwenye mwendo kitaendelea na mwendo huo huo kama hakuna nguvu itakayowekwa kupunguza au kuongeza mwendo huo. Kwa mfano kama kusingekuwa na nguvu ya mvutano kwenye dunia, ungerusha kitu kingeenda angani na kupotea kabisa.

Unawezaje kutumia sheria hii kwenye mafanikio?

Mara baada ya kuweka malengo yako na kuanza kuyatekeleza hakikisha huachi hata siku moja kile unachofanya. Kama usipoacha utaendelea vizuri na utafikia mafanikio. Kama ukiacha itakuwa vigumu sana kwako kuanza tena kama ilivyo kwenye sheria ya kwanza. Kama umeamua kufanya mazoezi ili kuweka afya yako vizuri usiache, kama umeamua kuacha kupoteza muda endelea hivyo hivyo na lazima utafikia mafanikio makubwa.

Sheria ya tatu; vitendo(law of action and reaction)

Sheria hii inasema kwamba nguvu unayoweka kwenye kufanya kitendo ndio nguvu hiyo hiyo unayoipata kutoka kwneye kitendo hicho. Yaani kama unasukuma ukuta na ukuta nao unakusukuma kwa nguvu sawa na unayoiweka.

Unatumiaje sheria hii kwenye mafanikio?

Jinsi utakavyoweka juhudi kubwa kwenye kufikia mafanikio ndivyo utakavyopata mafanikio makubwa zaidi. Sina haja ya kuzungumzia hili sana kwa sababu tumeshalijadili sana kwneye makala mbalimbali. Kama ukifanya kazi/biashara kawaida na wewe utaishia kuwa wa kawaida. Kama ukifanya kazi/biashara kipekee utakuwa wa kipekee. Kile unachoweka ndio unachopata.

Kumbuka sheria hizi tatu kila siku ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

1. Kama hupendi hali uliyonayo sasa ibadili, na sio kuilalamikia.

2. Ukianza kufanya jambo endelea kulifanya, usikate tamaa wala kuishia njiani.

3. Kama unataka kupata mafanikio makubwa, weka juhudi kubwa kwenye kazi au biashara yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kutengeneza mafanikio makubwa sana.

TUKO PAMOJA.

kitabu kava tangazo[4]