Wiki iliyopita katika makala hizi za kujenga tabia za mafanikio, tuliona aina za uwekezaji ambazo mtu aliyejiajiri au anayefanya biashara anaweza kuzifanya. Aina hizo ni zile ambazo zinahitaji muda mwingi wa kufuatilia ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ile isome kwa kubonyeza maneno haya.

Leo tutajadili aina za uwekezaji ambazo mtu aliyeajiriwa au ambaye hana muda wa kutosha wa kusimamia uwekezaji wake anaweza kufanya. Aina hizi pia zinaweza kufanyika na wale ambao wamejiajiri au wanafanya biashara kulingana na mtu anavyopendelea mwenyewe. Kumbuka tunajadili njia hizi za uwekezaji ili kuweza kuongeza thamani ya fedha zetu tofauti na zinavyokaa benki au kwenye mifumo mingine ya akiba.

Zifuatazo ni baadhi ya aina za uwekezaji unazoweza kufanya kama bado upo kwenye ajira au huna muda wa kutosha kusimamia uwekezaji wako.

1. Kununua vitu vinavyoongezeka thamani kwa muda mrefu.

Kuna vitu ambavyo kwa sasa vinaweza kuwa na dhamani kidogo ila miaka kumi ijayo vikawa na thamani kubwa sana. Kama utakuwa na akiba kidogo na ukaanza kuwekeza kwenye vitu hivi miaka mingi ijayo uwekezaji wako utakuwa wa thamani kubwa kuliko fedha uliyowekeza sasa. Mfano wa vitu hivyo ni ardhi, nyumba, madini na kadhalika.

Kwa upande wa ardhi, unaweza kununua ardhi kwenye maeneo ambayo kwa sasa ardhi bei yake ni ndogo, ukafanya uendelezaji kidogo na miaka mingi ijayo ardhi hiyo ikawa na thamani kubwa sana. Ila ni muhimu kuwa mwangalifu unapofanya uwekezaji huu kwa sababu unaweza kununua ardhi nyingi na ukashindwa kuiendeleza baadae ukaipoteza.

Kwenye nyumba vile vile unaweza kujenga nyumba kwenye maeneo ambayo gharama sio kubwa sana kwa sasa na baadae ukaja kuuza au kupangisha nyumba hizo.

Kuhusu madini, kuna baadhi ya benki zinaruhusu mtu kununua madini kama dhahabu na kuyaweka. Kwa kuwa madini haya yanaongezeka thamani siku nyingi zijazo fedha uliyowekeza sasa itakuwa imeongezeka sana. Ila kwenye madini kuna taratibu nyingi na inahitaji kuwa na fedha nyingi tofauti na ardhi au nyumba.

Uwekezaji huu wa ardhi au nyumba unahitaji uvumilivu na sio kutaka kupata haraka.

2. Kufanya kilimo cha muda mrefu.

Unaweza kuwekeza kwenye kilimo kinachochukua muda mrefu na ambacho hakihitaji sana muda wako. Mfano wa kilimo hiko ni kilimo cha miti. Kilimo cha miti inachukua kati ya miaka nane mpaka miaka kumi na tano. Unaweza kuwekeza fedha kidogo ila baada ya muda huo ukapata fedha nyingi sana. Kwa mfano kuna maeneo ambapo ekari moja unaweza kununua kwa shilingi laki mbili mpaka tatu, ukapanda miche ya miti karibu mia sita ambapo mche mmoja unauzwa shilingi mia mbili hamsini. Baadae wakati wa kuvuna utauza mti mmoja sio chini ya elfu hamsini. Kwa hesabu za haraka kwa ekari moja utakuwa umetumia shilingi milioni moja na utakapovuna utapata milioni thelathini, sasa ukiwa na ekari nyingi ndivyo utakavyozidi kuwa na kipato kikubwa. Kuna gharama ndogo ndogo utakazoingia kati kati ila kikubwa unachohitaji ni uvumilivu huo wa muda.

3. Kuingia ubia kwenye makampuni madogo na hata makubwa.

Kampuni nyingi sana zinafanya biashara vizuri ila zina kikwazo cha mtaji. Kwa kuwa wewe una fedha unaweza kuingia ubia na kampuni za aina hii na ukawekeza fedha zako wao wakazitumia kama mtaji na baadae wakakugawia sehemu ya faida. Hii inaitwa kununua hisa. Wewe hutahusika moja kwa moja kwenye shughuli za kila siku za kampuni ila utapata faida kulingana na ukuaji wa kampuni. Hii ni njia nzuri ya uwekezaji ila pia ina hatari kubwa, kwa sababu kampuni ikipata hasara na wewe unaingia kwenye hasara hiyo na hivyo unaweza kupoteza fedha zako.

Unahitaji kuijua vizuri kampuni na kuwa na uhakika na uendeshwaji wake ili usije kupoteza fedha zako kirahisi.

4. Kununua vipande.

Kuna aina nyingine ya uwekezaji ambayo sio maarufu sana hapa kwetu. Uwekezaji huu ni wa kununua vipande na baada ya muda vipande hivi vinaongezeka thamani na hivyo wewe kupata faida pale utakapokuja kuuza vipande hivyo baadae. Hii nayo ina hatari kwa sababu uchumi ukiyumba inapelekea bei ya vipande kuweza kushuka kwa kasi na wewe kupoteza fedha zako. Ila vipande ni rahisi zaidi kwa mtu kufanya ukilinganisha na kununua hisa. Hapa kwetu Tanzania kuna mfuko unahusika na kuuza vipande uanitwa UMOJA FUND ambao uko chini ya UTT(Unity Trust of Tanzania).

Kutokana na umuhimu wa aina hii ya uwekezaji nitaandaa makala ya kuchambua uwekezaji huu wa UMOJA FUND na nitakushauri kama unaweza uwekeze huko kwani mimi nimewekeza huko na naona ukuaji mkubwa wa fedha ninazoweka. Makala hii itakuja kwenye kipengele cha FURSA ambapo wale ambao ni GOLD MEMBER wanaweza kuisoma.

Kwa kifupi ni aina nzuri na rahisi sana ya uwekezaji ambayo haiumizi kichwa na ina historia nzuri ya kutopata hasara. Tutaichambua vizuri kwenye makala hiyo nitakayoandaa.

Hizi ni baadhi ya aina za uwekezaji unazoweza kufanya kama bado upo kwenye ajira au huna muda wa kutosha wa kufuatilia uwekezaji wako, pia unaweza kuzifanya hata kama umejiajiri au unafanya biashara. Chagua aina moja unayoona itakufaa na jifunze zaidi huku ukianza kuwekeza kidogo kidogo. Pia unaweza kuwekeza sehemu moja mtaji wako ukakua na ukawekeza kwingine. Kwa mfano unaweza kuwekeza kwenye UMOJA FUND mtaji wako ukakua ukachukua na kwenda kuwekeza kwenye nyumba. Au ukaanza na miti na baadae ukaendelea na uwekezaji mwingine.

Aina hizi za uwekezaji nilizoeleza hapa zinamfaa kila mtu hata awe na kipato kidogo kiasi gani, kwa mfano kwenye UMOJA unaweza kuwekeza hata shilingi elfu kumi kila baada ya muda na kama utakuwa na nidhamu nzuri utajikuta na fedha nyingi sana baada ya muda. Tutajadili zaidi hii ya mfuko wa UMOJA kwenye makala nitakayoandaa kwa wale ambao ni GOLD MEMBERS.

Nakutakia kila la kheri kwenye uwekezaji wa fedha zako ulizojiwekea akiba kwa muda sasa.

TUKO PAMOJA.