Kwenye maisha hakuna mtu ambaye anapenda kuteseka. Kila mmoja wetu anapenda kuwa na maisha mazuri na yenye furaha. Lakini pamoja na hali hii ya kupenda furaha bado ni wachache sana ambao wanaweza kupata furaha idumuyo, wengi huendelea kuteseka kwenye maisha wakiikimbizi furaha bila ya mafanikio.

Leo katika kipengele hiki cha ushauri kwa wahitimu tutajadili umuhimu wa kuvumilia mateso ya muda mfupi ili kuweza kufaidi furaha idumuyo.

Tunaelewa vizuri sana kwamba ulikuwa na mipango mingi sana kipindi chote umekuwa kwenye elimu. Pia tunakumbuka ndoto nzuri ulizokuwa unaota kwamba ukimaliza masomo ni jinsi gani maisha yatakuwa mazuri baada ya kupata kazi uliyosomea na kupata kipato kizuri.

Lakini sasa umefika mtaani mambo ni tofauti kabisa, kazi ya ndoto yako imekuwa ngumu kupata na hata kama umeipata kipato ni kidogo sana ukilinganisha na matarajio yako.

Sasa unafanya nini? Unaendelea kuzunguka na bahasha kutafuta kazi tu? Unaendelea kulalamika ni jinsi gani kazi uliyopata inakuchosha huku malipo yakiwa ni kidogo? Yote haya hayatakusaidia zaidi ya kukufanya uendelee kuwa mtumwa wa fikra zinazoendelea kukurudisha nyuma.

Kitakachokusaidia kwenye hali hii ni kufanya maamuzi magumu ambayo yatakuumiza kwa muda mfupi ila baadae mambo yatakuwa mazuri sana.

Unafanyaje ili kuweza kuvumilia mateso haya ya muda mfupi na baadae kufurahia maisha?

Ili kuweza kuvumilia mateso haya ya muda mfupi na baadae kufurahia maisha kwanza kabisa amua ni kitu gani unataka kufanya kwenye maisha yako. Chagua kitu kimoja ambacho unapenda kukifanya na upo tayari kukifanya bila ya kukereka au kulazimishwa. Inaweza kuwa kitu ambacho umesomea au wakati mwingine ikawa kitu tofauti kabisa. Inaweza kuwa kilimo, biashara, usanii na kadhalika

Baada ya kujua ni kitu gani umeamua kufanya, wekeza muda wa kutosha katika kujifunza na kufanya kitu hiko mpaka uweze kufikia viwango vya kimataifa.

Kumbuka kwamba unapoanzia chini, hasa pale unapokuwa na mtaji kidogo au huna fedha kabisa rasilimali yako kubwa ni elimu(ujuzi), muda na ubunifu. Vitu hivi vitatu ukiongeza na uvumilivu vitakufikisha kwenye mafanikio makubwa sana.

Elimu; unahitaji kujua vizuri kile unachofanya ili uweze kukifanya vizuri zaidi. Hivyo tumia muda wako mwingi kwenye kujifunza na kujisomea ili kuwa na uelewa wa kutosha wa kile unachofanya.(Soma; wahitimu kujifunza ndio kumeanza rasmi).

Muda; Muda ni muhimu sana kwako kuweza kufikia mafanikio makubwa. Hakuna mafanikio yadumuyo yanayotokea haraka, unahitaji muda wa kujifunza na kufanya mpaka pale utakapobobea. Hivyo jipe muda wa kutosha wa kufanya na kujifunza ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Ubunifu; Kama huwezi kujitofautisha na wengine ambao wanafanya kile unachofanya utapata shida kwa muda mrefu sana. Ni muhimu sana kuwa mbunifu kwa chochote kile unachofanya ili kuweza kupata mafanikio makubwa. Uzuri ni kwamba wewe ni mbunifu mkubwa, sema tu hujajua hilo(soma; kila mtu ni mbunifu, wewe umetumia ubunifu wako)

Uvumilivu; Bila ya uvumilivu ndugu yangu utahangaika sana kwenye maisha haya. Utafanya kitu kimoja, utaona hakilipi, utahamia kwenye kingine nako utaona hakina soko, utaenda kingine na kingine mpaka siku unastuka miaka imeenda na huna chochote cha kusimamia. Chagua kitu kimoja unachopenda kufanya kutoka moyoni mwako kama nilivyosema hapo juu, kisha jitoe kufanya kitu hiki kwa moyo mmoja na tumia kila rasilimali iliyo ndani yako na hata nje yako mpaka pale utakapofikia mafanikio

Hakuna kitu ambacho hakiwezekani au hakilipi, inategemea na wewe mwenyewe umejitoa vipi na pia una mtazamo gani.

Unasubiri nini? Fanya maamuzi leo hii na uanze kuyatekeleza ili baadae mambo yako yawe vizuri sana. Pia karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambapo utajifunza mengi sana yatakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio.

TUKO PAMOJA.

KWA-NINI-SIO-TAJIRI4