Watu wengi wanaamini kuwa ili mtu aweze kufikia viwango bora vya mafanikio anayoyataka na hatimaye kuwa tajiri ni lazima mtu huyo awe na bahati ya pekee au ni lazima ajihusishe sana na mambo ya giza. Wengine wanaamini utajiri upo kwa ajili ya watu fulani tu katika jamii na si  vinginevyo.
Zipo imani nyingi sana katika jamii zetu tunazoishi zinazohusiana na juu ya utajiri. Na imani hizi zimekuwa zikitofautiana kati ya mtu na mtu na pia sehemu na sehemu. Kitu pekee na cha muhimu kujiuliza je, imani hizi ni za kweli kiasi gani? Na wewe unaamini nini hasa juu ya mafanikio na kuweza kufikia viwango bora vya mafanikio.
Uwezo wa kufikia mafanikio unayoyataka unao endapo tu utaamua kufanikiwa na kukubali kukabiliana na vikwazo kadhaa ambavyo pengine vinaweza vikakukatisha tamaaa kama usipokuwa makini. Unawezaje kufikia viwango bora vya mafanikio na kuachana na fikra zinazokuzuia kufikia viwango bora vya mafanikio?
 

Hivi ndivyo unavyoweza kufikia viwango bora vya mafanikio unayoyataka bila ya kutumia uchawi:-

 
1. Jenga dhamira kubwa ya kufanikiwa.
 

Kama unataka kufanikiwa zaidi ya hapo ulipo anza kujenga dhamira kubwa ya kufanikiwa kuanzia sasa. Chapa kazi na kila mara jenga tabia ya kujifunza mambo mapya. Jifunze pia kila siku kufanya jambo ambalo litakuwezesha angalau kufanikisha ndoto zako. Unapokuwa na dhamira kubwa ya kufanikiwa utasababisha mambo yako mengi kusonga mbele na utajikuta unafikia viwango bora vya mafanikio unayo yataka. 
2. Jifunze kuwa mbunifu zaidi.
Kwa kila unachokifanya ongeza ubunifu utaona matunda  zaidi. Watu wote wenye mafanikio ni wabunifu wakubwa kwa vile vitu wanavyofanya. Ukiangalia maisha ya watu waliofanikiwa vitu wanavyofanya wakati mwingine havina tofauti na unavyofanya wewe ila tofauti kubwa ipo kwenye ubunifu tu. Acha kujidharau wala kujishusha kumbuka kila mtu ni mbunifu, je unautumia ubunifu wako kufikia malengo? Kama Unataka kufikia viwango bora vya mafanikio unayoyahitaji  jifunze juu ya ubunifu hii itakusaidia sana.
3. Jenga tabia ya kuwa mtulivu.
Mafaniko yoyote huchukua muda kuyajenga. Acha kupenda utajiri wa haraka haraka kaa chini wewe mwenyewe jiulize ni muda kiasi gani unahitaji ili kufikia mafanikio makubwa  unayoyataka. Unapokuwa na subira hii itakusaidia kupanga mipango na malengo yako vizuri na kuifanikisha. Kumbuka kila kitu kina muda wake na muda wa mafanikio yako upo.
4. Jitoe mhanga.
Watu wenye mafanikio hujitoa mhanga kwenye ndoto zao lakini zaidi na majasiri.Wako tayari kuwekeza na kufanya maamuzi yanayoonekana kuwa ya hatari kwa watu wa kawaida. Ni watu wenye hasira ya kuhakikisha kuona malengo yao yanatimia na  hawana mchezo na hilo. Je, una hasira kiasi gani ya kufikia mafanikio na kuona malengo yako yanatimia na kuweza kufikia viwango bora vya mafanikio unayoyataka? Unaweza ukawa chochote tu kama utaamua kujitoa mhanga juu ya ndoto  zako na utafanikaiwa.
5. Jifunze kutokukata tamaa mapema.
Mara nyingi pia ukitaka kuwa mtu wa mafanikio jifunze kutokukata tamaa katika maisha yako yote iwe kwenye  kufikiri, kuzungumza au hata kwenye hisia zako. Futa kabisa msamiati kukata tamaa kwenye ubongo wako kisha songa mbele hata kukiwa na vikwazo vingi namna gani. Acha kuangalia sana matatizo uliyonayo fata ndoto zako na kuhakikisha unafikia viwango bora vya mafanikio uliyojiwekea.
6. Jenga tabia ya kujifunza kila siku.
Kama unapenda kufanikiwa zaidi jifunze pia kuwekeza kwenye akili zako ama kwa kusoma au kuhudhuria semina na vitu kama hivyo. Hakikisha unasoma vitabu vingi uwezavyo, hii itakusaidia sana kupata majibu ya mambo mengi uyatakayo na usiyoyajua. Kama kwako ni shida kupata vitabu na semina za mafanikio unaweza pia ukatumia njia bora kabisa ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA na kujifunza maarifa bora zaidi yatakayokufanya ufike kwenye kilele cha mafanikio.
7. Jenga uwezo wa kubadilika.
Ili kufikia viwango bora vya mafanikio unayoyataka ni lazima ujifunze kubadilika na kusoma mazingira yalivyo na kuwa king’ang’azi hata kwa mambo yanayokupeleka kubaya. Kama unaona unakokwenda siko sahihi nakushauri badili mwelekeo na kufata njia itakayokufikisha kwenye mafanikio yako.
 
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya ukombozi wa maisha iwe ya ushindi, ansante kwa kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIAna Karibu sana.
 
TUPO PAMOJA!