Katika uchambuzi uliopita tuliona Bansier na Kobbi wakikubaliana kwenda kuomba ushauri kuhusu utajiri kutoka kwa mtu aliyekuwa tajiri sana pale ababeli ambaye alikuwa ni Arkad. Arkad alikubali kuwapa siri yake na alianza kwa kuwaambia jinsi gani alipata elimu hiyo.

Aliwaambia jinsi alivyokuwa mwandishi na siku moja mtu tajiri, mkopeshaji fedha alikuja kwake kuandikiwa sheria. Arkad alimwomba, kama akijitahidi na kumaliza kuandika sheria ile basi kwana yule amfundishe elimu ya kuwa tajiri, bwana yule alikubali.

Mtu tajiri kuliko wote babeli sehemu ya 2.

Algamish alimwambia Arkad, ‘”niligundua njia ya utajiri pale nilipoamua kwamba, sehemu ya kipato changu ni mali yangu ninayotakiwa kuitunza, na wewe ukifanya hivi utakuwa tajiri”. Arkad alimuuliza ndio hivyo tu, akamjibu hiyo ilinitosha kuondoka kwenye kuchunga kondoo na kuwa mkopeshaji wa hela.

Arkad alimwambia lakini kipato changu chote si ni mali yangu? Alimjibu sio kweli hata kidogo. Alimwambia humlipi mtengeneza nguo? Humlipi muuza urembo? Hulipii chakula? Alimwambia unawalipa watu wote hao kasoro wewe mwenyewe. Alimwambia unaendelea kuwa mtumwa kwa sababu kila fedha unayopata unaipeleka kwenye matumizi, badala ya kuifanya fedha hiyo ikutumikie wewe.

Algamish alumuuliza, kama ukiweka sehemu ya kumi ya kipato chako cha mwaka kwa miaka kumi utakuwa na kiasi gani? Arkad alimjibu kiasi ambacho napata kwenye mwaka mmoja. Alimwambia sio kweli, kila dhahabu unayoweka inakufanyia wewe kazi na kukuletea fedha na shaba zaidi. Alimwambia kama unataka kuwa tajiri ni lazima dhahabu yako ikufanyie kazi na ipate watoto na wale watoto wakufanyie kazi nao walete watoto. Hii itakutosha kukuletea utajiri ambao unautaka.

Algamish alimwambia Arkad kama unaona nakudanganya jua nakulipa mara nyingi sana zaidi ya kazi uliyoifanya. Sehemu ya kipato chako ni mali yako na itunze, isiwe chini ya moja ya kumi ya kipato chako hata uwe na kipato kidogo kiasi gani. Inaweza kuwa kiasi kikubwa uwezavyo, jilipe wewe kwanza. Unapopata kipato usianze kununua vitu au kulipa madeni, jilipe wewe kwanza na kinachobaki ndio ununue vitu. Aliendelea kumuambia, utajiri kama ilivyo mti hukua kutoka kwenye mbegu ndogo, shaba ya kwanza unayoweka ndio mbegu ya utajiri wake. Jinsi utakavyopanda mbegu yako mapema ndivyo mti wako utakavyoota mapema. Na jinsi utakavyoutunza mti wako vizuri kwa kuendelea kuweka akiba ndivyo utakavyokua na kufikia utajiri mkubwa. Baada ya kusema hayo Algamish alichukua sheria zake na kuondoka.

Arkad alifikiria sana yale aliyoambiwa na aliamua kujaribu kuyafanya. Kila alipolipwa alichukua sehemu ya kumi ya malipo yake na kuiweka pembeni. Baada ya muda mfupi haikuwa ngumu kwake na hakuona tofauti ya matumizi kabla ya kuondoa sehemu ya kumi na baada ya kuondoa sehemu ya kumi na pia alianza kuondoka kwenye ukwasi wa kutokuwa na hela kabisa. Mara kwa mara alipata tamaa ya kutumia fedha ile kununua vitu vizuri alivyoona kwa wauzaji lakini alijizuia.

Baada ya miezi kumi na mbili Algamish alirudi tena na kumuuliza vipi ushauri wangu umeufanyia kazi? Alimjibu ndio nimeweza kuweka sehemu ya kumi ya kipato changu. Amamuuliza umeifanyia nini fedha hiyo? Arkad akamjibu nimempa Azmur ambaye ni mtengeneza matofali, amesafiri kwenda nchi za mbali na amesema atanunua madini adimu na akirudi atauza tugawane faida. Algamish alimwambia wewe ni mpumbavu na unatakiwa kujifunza. Kwa nini uamini ushauri wa mtengeneza matofali kuhusu madini ya thamani? Alimuuliza unaweza kwenda kwa mtengeneza mikate kuomba ushauri wa nyota? Alimwambia umepoteza akiba yako yote, ila usikate tamaa anza tena kuweka akiba na kama utataka ushauri kuhusu madini mtafute sonara, ukitaka ushauri kuhusu kondoo mtafute mfuga kondoo.

Alimwambia ushauri ni kitu ambacho kinatolewa bure ila kuwa makini sana unachukua ushauri gani. Maana ukichukua ushauri kwa mtu ambaye hajui utaishia kupata hasara. Na kama alivyosema Algamish, yule mtengeneza matofali aliuziwa vipande vya chupa akiambiwa ni almasi na hivyo Arkad kuishia kupata hasara.

Miezi kumi na mbili mingine Algamish alirudi tena kwa Arkad na kumuuliza maendeleo yake yakoje? Arkad alimwambia ameweka sehemu ya kumi na ameiwekeza kwa mkopesha fedha na hivyo huwa anamlipa faida ya kile alichowekeza. Algamish alimwambia vizuri sana, akamuuliza unafanya nini na hiyo faida unayopata? Arkad alimjibu anasherekea na kula vizuri na ana mpango wa kununua farasi ili awe anatembea juu ya farasi. Algamish alimcheka sana na kumuuliza kama unakula watoto wa akiba yako unategemea watakuzaliaje? Na watakuaje na watoto ambao nao watakufanyia kazi wewe? Alimwambia wekeza zaidi ili fedha iendelee kukutumikia na baadae utaweza kuishi maisha yoyote unayotaka.

Baada ya maneno hayo Algamish aliondoka na Arkad hakumuona tena kwa miaka miwili. Aliporudi tena alionekana kuwa amezeeka sana. Alimuuliza Arkad je umeshapata utajiri uliokuwa unatarajia? Arkad alimjibu bado ila ana vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaendelea kumzalishia kila siku hivyo muda sio mrefu atafikia malengo yake. Akamuuliza tena je bado unachukua ushauri wa mtengeneza matofali? Akamjibu kuhusu matofali ndio nachukua ila kuhusu mambo mengine hapana.

Algamish alimwambia umejifunza masomo yako vizuri sana.

Kwanza umejifunza kuishi chini ya kipato chako na kujilipa wewe mwenyewe kwanza.

Pili umejifunza kuchukua ushauri kwa watu ambao wana uzoefu na kitu husika.

Na tatu umejifunza kuifanya akiba yako ikufanyie wewe kazi.

Umejifunza JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA, JINSI YA KUTUNZA FEDHA NA JINSI YA KUIFANYA FEDHA IKUFANYIE KAZI. Hivyo umeshakuwa na utaalamu wa kutosha na unaweza kuchukua majukumu makubwa.

Algamish alimwambia Arkad kwamba yeye amezeeka na mtoto wake hana muelekeo mzuri kwani anafikiria tu jinsi ya kutumia utajiri wa baba yake. Hivyo alimuomba aende akawe msimamizi wa vyanzo vyake vya mapato. Arkad alikubali na alisimamia vizuri sana mali zile na wote wakafaidika sana.

Baada ya kumaliza kuwahadithia ni jinsi gani alivyopata elimu ile ya fedha waliokuwa wanamsikiliza walisema Arkad una bahati sana, mtu tajiri alikupa usimamizi wa mali zake na ndio maana umekuwa tajiri.

Aliwaambia bahati ni kwamba yeye alionesha mafanikio ndio maana aliaminiwa na kupewa usimamizi. Hii sio bahati kwa sababu alifanya kazi na kujinyima ili kuweza kuwekeza. Na hata alipopoteza uwekezaji wake wa mwaka mzima bado hakukata tamaa na ndio maana alifanikiwa. Na pia alikuwa tayari kujifunza na kuchukua hatua.

Mtu mwingine alimuuliza Arkad, kama unachosema ni kweli na kama kila mtu akitumia mbinu zako je kutakuwa na fedha za kutosha kuwafanya watu wote matajiri? Arkad alijibu utajiri unakua pale ambapo mtu anaweka nguvu na jitihada. Aliwapa mfano kama mtu tajiri akiamua kujenga jumba kubwa je fedha zake zinakwenda wapi? Si zinakwenda kwa mafundi, wapaka rangi, wauza thamani,na hata vibarua. Na hata jengo hilo linapokamilika, ardhi ile inakuwa na thamani kubwa na hata ardhi iliyopo jirani na ile inakuwa na thamani kubwa zaidi. Aliwaambia utajiri unakuwa kwa njia za ajabu na hakuna anayeweza kuuzuia kuenda kwa wengine kwa sababu yeye anao.

Mtu mwingine aliuliza, kwa hiyo unatushauri tufanye nini ili na sisi tuwe matajiri? Alijibu, Tumieni busara ya Algamish kwamba SEHEMU YA KIPATO CHANGU NI MALI YANGU YA KUWEKA AKIBA. Aliwaambia wasema maneno hayo kila mara na kuyafanyia kazi. Aliwaambia pia wajifunze kufanya akiba yao iwafanyie kazi na pia wapate ushauri kwa watu ambao wana uzoefu na watu wazee pia.

ZOEZI LA KUFANYA.

Orodhesha mambo matano uliyojifunza kwenye sehemu hii ya uchambuzi na utushirikishe kwenye sehemu ya maoni hapo chini. Kisha kwenye kitabu chako mwenyewe andika ni jinsi gani utaanza kuyatumia mambo hayo kwenye maisha yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.

P.S Usisahau kutushirikisha mambo matano uliyojifunza kwenye sehemu hii ya uchambuzi hapo chini kwenye maoni.