Babeli ulikuwa ni mji ambao umebarikiwa sana na uliokuwa na watu ambao ni matajiri sana katika enzi hizo. Sio kwamba mji huu ulianza na utajiri, bali utajiri wake ulitokana na busara za wananchi wa mji ule. Kitu cha kwanz akabisa walichofanya ni kujifunza kuhusu utajiri.

Baada ya mfalme Sargon kurejea babeli kutoka kwenye vita, kansela wake alimfata na kumuambia. Baada ya miaka mingi ya utajiri kwa watu wetu kutokana na miradi ya kujenga mifereji na majumba, sasa kazi hizo zimekwisha na wananchi wengi hawana chanzo cha kipato. Wafanyakazi hawana kazi, wafanya biashara hawana wateja na hata wakulima hawawezi kuuza mazao yao. Watu hawana dhahabu za kutosha kununua chakula na mahitaji mengine.

Mfalme alimuuliza, dhahabu zote ambazo zilikuwa zinapatikana wakati wa ujenzi zimekwenda wapi? Kansela akamjibu; zimefuata mkondo wake, zimekwenda kwa matajiri wachache wa mji huu. Watu wengi hawana njia ya kupata tena dhahabu hii kutoka kwa matajiri hao wachache. Mfalme alifikiri kwa muda na kisha akamuuliza inawezekanaje watu wachache sana kuwa matajiri kuliko wengine? Kansela alimjibu kwa sababu wanajua ni jinsi gani ya kupata utajiri. Akaendelea kumwambia hatuwezi kumshitaki mtu kwa sababu amekuwa tajiri kutokana na yeye kujua mbinu hizo na pia hatuwezi kumnyanganya mazi hizo na kuwagawia masikini.

Mfalme aliendelea kumuuliza, kwa nini watu wote wasijifunze mbinu za kuwa matajiri na kisha kuwa na utajiri na mafanikio? Kansela alimjibu, inawezekana sana, lakini nani atakayewafundisha? Wahubiri hawawezi kuwafundisha hilo maana hata wao hawajui chochote kuhusu fedha na utajiri.

Mfalme alimuuliza kansela, ni mtu gani kwenye mji huu ambaye anajua sana kuhusu fedha? Kansela akamjibu, bila ya ubishi ni mtu ambaye ni tajiri kuliko wote hapa babeli. Mfalme alimwambia mtu huyo ni Arkad na hivyo aliagiza Arkad aitwe kwa mfalme siku inayofuatia.

Kesho yake Arkad alifika kwa mfalme kama alivyoagizwa.

Mfalme alimuuliza, Arkad je ni kweli kwamba wewe ndio mtu tajiri kushinda wote hapa babeli? Arkad alijibu, ndio inasemekana hivyo na hakuna ambaye amewahi kupinga hilo. Mfalme alimuuliza umewezaje wewe kuwa tajiri sana? Arkad alimjibu, kwa kutumia fursa zinazopatikana kwa wananchi wote wa mji wetu huu. Mfalme alimuuliza tena hukuanza na chochote? Arkad akajibu, sikuanza na chochote zaidi ya hitaji kubwa la kutaka kuwa tajiri.

Mfalme alimwambia, mji wetu upo kwenye hali ya huzuni sana kwa sababu watu wachache wanajua jinsi ya kupata utajiri na wameshaumiliki wakati wananchi wengi wakiwa hawajui na hivyo kushindwa kuwa matajiri. Ni hitaji langu kwamba babeli ume mji tajiri kuliko yote dunniani na ili kufikia hivyo ni lazima wananchi wake wawe matajiri sana. Na ili wananchi waweze kuwa matajiri ni lazima wafundishwe jinsi ya kufikia utajiri.

Mfalme akamuuliza tena Arkad, je kuna siri ya kupata utajiri? Na je siri hii inaweza kufundishwa? Arkad alimjibu, inawezekana, kile mtu mmoja anachojua anaweza kuwafundisha watu wengine.  Mfalme alimwambia Arkad umeongea maneno niliyotaka kusikia, je unaweza kuwafundisha waalimu wa mji huu siri hizo nao wakaenda kuwafundisha wengine mpaka siri hizi zikamfikia kila mwananchi? Arkad alijibu ndio ninaweza na nitajisikia vizuri sana kuwafundisha wananchi wenzangu siri hizi. Alimwambia mfalme amwambie kansela aandae darasa la watu mia moja na atawafundisha mbinu saba alizotumia kutunisha mifuko yake iliyokuwa imesinyaa.

Baada ya muda kupita, watu mia moja waliandaliwa na kukutana kwenye ukumbi wa mikutano. Wakati watu wale wanamsubiri Arkad ili aje kuwafundisha mwanafunzi mmoja alimwona wakati anakuja na kusema huyu ndie mtu tajiri kuliko wote babeli, kumbe ni mtu kama sisi.

Arkad alisimama mbele ya watu wale mia moja na kuanza kwa kusema; Nimesimama mbele yenu mimi ambaye nilikuwa kijana masikini sana niliyekuwa na hamu ya kuwa tajiri na nilitafuta maarifa ya kupata utajiri huo ambayo nitakwenda kuwashirikisha hapa. Aliendelea kuwaambia, nilianzia chini sana bila ya kuwa na upendeleo ambao watu wengi wanao sasa. Aliwaambia alianza na mfuko uliosinyaa sana lakini lengo lake ilikuwa kuutunisha kwa dhahabu ili awe tajiri sana. Na ili kufikia lengo hilo alitafuta sana maarifa ya kutibu mfuko uliosinyaa na alipata njia saba ambazo atakwenda kuwafundisha.

Aliwaambia kila siku kwa siku saba nitawafundisha tiba moja ya kutunisha kifuko iliyosinyaa ambayo anashauri kila mtu ambaye anataka kufikia utajiri ni lazima azitumie. Aliwaambia sikilizeni kwa makini elimu ninayowapatia, jadilianeni, niulizeni maswali na kaitumieni elimu hii na itawasaidia sana. Na mkishaweza kuitumia elimu hii mtaweza kuwafundisha na wengine pia ili nao waweze kufanikiwa.

Tutaendelea na kujifunza tiba hizo saba za mifuko iliyosinyaa kwenye uchambuzi ujao.

Tushirikishane kwenye maoni hapo chini ni vitu gani umejifunza kwenye sehemu hii ya uchambuzi.

Nakutakia kila la kheri, TUPO PAMOJA.