Kule kwetu Moshi, ukitaka kujua vizuri mtu ni nani basi kama mmepakana ongeza mpaka wako uzidi ule wa kwake. Yaani ongeza hatua moja tu kwenye mpaka wako na yeye. Atafanya kila jambo kuhakikisha anarudisha hatua ile moja uliyoongeza. Atakushitaki, mtagombana na anaweza kuapa kwamba hata akifa usifike kwenye kaburi lake. Hiyo ni hatua moja tu ya ardhi.

UNAONA HUYO JAMAA ANAIBA NINI?
UNAONA HUYO JAMAA ANAIBA NINI?

Utalinda fedha zako kwa nguvu na gharama kubwa sana. Utahakikisha hakuna mtu anayejaribu kukuibia au kuzichukua na kuzitumia hovyo. Hongera sana, unajua ni kipi cha thamani na unakilinda ipasavyo.

Lakini unachonishangaza sasa ni kwamba kuna kitu kingine cha thamani zaidi lakini hukilindi kama unavyolinda fedha na mali zako. Kitu hiki kina thamani kubwa sana ambayo huwezi kulinganisha na fedha au mali unazolinda sasa.

Uko tayari ununue gari na ulikatie bima kubwa(comprehensive) ili ikitokea ajali au likiibwa upate kulipwa, unajua kulinda sana. Lakini kitu hiki cha msingi kuliko hata hilo gari unakiacha kinapotea hovyo na watu wanakitumia watakavyo.

Yaani ukilinganisha kitu hiki na hizo mali zako ni sawa na kulinganisha kokoto na almasi.

Ngoja nikuulize, kwa mfano umeenda mahali, ukakuta mtu anakazana kuokota kokoto, na anazuia watu wasizishike, ila eneo hilo hilo kuna almasi lakini haziokoti wala kuzilinda, utamchukuliaje mtu huyo? Utaona amechanganyikiwa eh? Usitumie maneno makali sana, maana mtu huyo ni wewe mwenyewe.

Swali kati ya muda na fedha ni kipi chenye thamani?

Mtu akikuibia laki moja leo, je amekuzuia wewe kupata laki moja nyingine siku zijazo?

Je mtu akikuibia sekunde moja leo, anaweza kuilipa tena? Vipi kuhusu dakika, saa, siku na kadhalika?

Sasa umekuwa mlinzi mzuri sana wa fedha zako na mali zako. Lakini umesahau kulinda kitu cha thamani sana kwako ambacho ni muda wako.

Umekuwa unaruhusu kila mtu achezee muda wako akama anavyotaka mwenyewe. Umeruhusu hako kakifaa kanakoitwa simu kawe ndio mwizi mkubwa wa muda wako. Umeruhusu mitandao ya kijamii iwe ndio mwizi mkubwa wa muda wako. Umekubali habari zisizo na faida yoyote kwako ziwe ndio kipaumbele cha muda wako. Huku wewe unakazana kulinda mali na fedha, watu wanaiba na kuchezea muda wako kama wanavyotaka mwenyewe.

Labda sasa hivi unaweza usielewe, labda unaona ah muda mbona bado upo tu. Lakini itafika siku ambapo maisha yako yatapita mbele yako kama sinema na utajiuliza hivi nilikuwa nafanya nini? Mbona sikuishi? Mbona sikuwa na muda wa kufanya yale ambayo ni ya msingi kwangu? Mbona maisha yamekuwa mafupi sana?

Ukweli ni kwamba maisha sio mafupi, ila umekuwa unapoteza muda kwenye vitu ambavyo sio vya msingi kwako.

Swali la mwisho ni je utaanza kulinda muda wako leo kama unavyolinda fedha na mali zako? Maisha ni yako na chaguo ni lako.

TAMKO LA LEO;

Nimekuwa natumia nguvu nyingi kulinda fedha na mali zangu kwa kuwa naamini ndio zina thamani kubwa kwangu. Lakini nimekuwa naruhusu watu waibe na kuchezea muda wangu kama wanavyotaka wao wenyewe. Kuanzia sasa naweka kipaumbele kikubwa sana kwenye muda wangu, nitaulinda kuliko ninavyolinda kitu kingine chochote. Kwa sababu najua muda wangu ndio maisha yangu na ninapopoteza muda maana yake napoteza maisha yangu mwenyewe. Kuanzia leo nitaacha kufanya mambo yote ambayo ni upotezaji wa muda kwangu, ili nipate muda mzuri wa kufanya kazi zangu, muda wa kuwa na familia yangu na muda wa kuwa na mimi mwenyewe.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.