Sikutegemea kabisa kama angeweza kunifanyia hivi…
Siku hizi amebadilika sana…
Huyu ni msaliti….
Ni baadhi ya kauli ambazo watu hutumia baada ya kuumizwa na maamuzi ya watu wengine. Unaweza kutumia kauli hizo na nyingine kama hizo kujiridhisha kwamba ni kweli umeumizwa lakini hazina msaada wote kwako. Hata iwe umeumizwa kiasi gani na maamuzi ya wengine, kuwalalamikia hakutaleta mabadiliko yoyote kwako na kwao pia.

Kwa kuwa kwenye maisha utaumizwa sana, leo nataka nikupe mbinu moja muhimu ya kuepuka kuumiza na maamuzi ya watu wengine. Kwa mbinu hii sio kwamba watu hawatakuumiza, ila watakapofanya hivyo wewe haitakuuma wala kuvuruga maisha yako. Utaweza kuendelea na maisha yako kama kawaida.
Mbinu moja muhimu itakayokuepusha na kuumizwa na maamuzi ya wengine ni kutokutegemea makubwa kutoka kwao, au vizuri zaidi ni kutegemea mabaya kabisa.
Unapotegemea mtu afanya mambo mazuri na makubwa, na kujihakikishia kwamba atafanya hivyo, unatengeneza nafasi kubwa sana ya wewe kuumizwa. Lakini unapoondoa haya mategemeo, hata asipotimiza haitakuumiza. Au kama utafikiria yeye kufanya vibaya zaidi, kama hatafanya haitakuumiza sana.
Wape watu nafasi ya kukosea, wape watu nafasi ya kubadili mawazo yao. Usiwashikilie kwa matarajio ya juu kama wao ndio malaika. Kila mmoja wetu ana changamoto zake na ni vigumu kujua kwa nini mtu amefanya kitu ambacho kinakuumiza yeye. Lakini kwa vyovyote vile, alichofanya ni bora zaidi kwake, hivyo badala ya kulalamika kwamba amekuumiza, furahi kwamba amefanya kilicho bora kwake. Na kama amevunja ahadi aliyokupa, pia furahi kwa sababu umejua msimamo wake ni upi kuliko angekuja kukusumbua zaidi baadae.
SOMA; Ni Ruhusa Kwako Kubadili Mawazo.
Maisha ni yako, chaguo ni lako, usiruhusu kabisa maamuzi ya watu wengine yawe mwiba kwenye maisha yako. Usitegemee makubwa kutoka kwa wengine. Na wakati mwingine tegemea mabovu kabisa.
TAMKO LA LEO;
Najua ya kwamba watu wanakosea na pia najua ya kwamba watu wanabadili mawazo yao. Pia najua ya kwamba kuweka mategemeo makubwa kwa watu ni kujitengenezea nafasi kubwa ya kuumizwa. Ili kuondokana na hili sitaweka mategemeo makubwa kwa watu na mara nyingi nitategemea mabaya kabisa. Kwa njia hii lolote litakalotokea halitaniumiza sana.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.