Ndugu yangu ni vyema kama utatambua kuwa uliumbwa ili uje uishi vile unavyotakiwa kuishi, kuna watu wapo hapa kazi yao ni kuiga, kushindana na wengine, yaani wao muda mwingi wanautumia kwa kuangalia nani anafanya nini na wao kujaribu kuiga au kufanya kile kile, si jambo baya sana kuiga lakini ni vyema ikiwa utaiga kitu ambacho walau unakipenda na unafurahia kukifanya, usiige tu kwa kuwa yule anafanya kinamlipa na kumpa faida kubwa. Au pengine unataka kufanya ili ushindane na yule, umuonyeshe jinsi unavyokubalika kuliko yeye.
 

USISHINDANE NA WENGINE, SIO SAIZI YAKO, NI WAKUBWA SANA AU WADOGO SANA KWAKO.


Ndugu tambua kuwa haya maisha si mashindano na watu wengine. Mashindano uliyo nayo na unayotakiwa kushindana basi ni kuhakikisha kila iitwapo leo unapata kitu kipya cha kukufanya uzidi kuwa bora zaidi. Maana uliumbwa kwa kusudi maalumu na ulipewa uwezo wa kuwa vile unatakiwa kuwa. Wengi hatujui ukweli huu kwa kuwa hatukupata watu wa kutuambia au kutuongoza, lakini shukuru kwamba umesikia hili sasa kama hukujua. Ni wajibu wako wewe kuishi na kutembea katika huu ufahamu mpya ulioupata kuhusu wewe ili uweze kuwa bora zaidi, ili kila siku mpya uzidi kuongezeka kwa kugundua na kujifunza mapya zaidi yanayokuhusu. Hebu ndugu yangu amua kwa dhati kwamba badala ya kupoteza muda kufanya yasiyokuhusu, yasiyokuwa na tija kwako, basi amua kufanya ya maana, amua leo kuhakikisha kuwa unakuwa bora zaidi kwa kuwekeza kwenye vitu vitakavyokusaidia na kukuwezesha kuwa bora zaidi tafuta maarifa zaidi, lakini yawe ni maarifa sahihi.
SOMA; Unaweza Kuwa Vile Unavyotaka Uamuzi Ni Wako
Ndugu yangu pengine unatamani kuwa kama mtu fulani , ni mara nyingi unakuta mtu anafanya juhudi nyingi sana kuhakikisha anamshinda mtu mwingine katika kitu fulani, lakini unaweza ona kwamba hata mtu yule akifanikiwa katika hilo bado hapati ile amani ya moyoni, bado ataona kuna kitu kinakosekana tu na atajikuta anaendelea na mapambano zaidi, maana kama umeamua kushindana na mtu utahakikisha kila anachofanya nawe umo ilimradi tu umshinde, naweza sema ni kama unakuwa umeweka maisha yako rehani , umeacha kuishi vile ulivyotakiwa kuishi na unahangaika tu na ulimwengu kwa kufanya vitu ambavyo bado havikupi furaha ya kweli, havikufanyi ufurahie maisha hata unapovipata, maana kila siku lipo jipya la kukuchanganya na kukufanya uingie mashindanoni.
Ndugu tambua kuwa mtu pekee unayetakiwa kuwa kwenye mashindano naye ni wewe pekee, maana wengi tunaishi chini ya viwango ya namna tunavyotakiwa kuwa, tuliumbwa na kupewa uwezo wa kufanya mambo makubwa sana, lakini wengi hatuelewi hilo au hata tukiambiwa tunashindwa kuamini kirahisi, lakini ukweli ni kwamba wewe hapo kipo kitu ulichoumbwa uje ufanye na kila kitu cha kukuwezesha kufanya hilo kipo, lakini ni mpaka ujielewe, uelewe hilo, ukubali na kuamini. Tambua kuwa u wa pekee sana na hakuna aliye kama wewe , na upo hapa kwa kusudi maalumu na aliyekuweka alikupa na kila kitu cha kukuwezesha , hivyo acha kupigana vita visivyokuhusu, acha kutamani kuwa kama wengine, acha kushindana na wengine maana haikusaidii , haikusogezi kule unatakiwa kuwa, bali utaishia kuchanganyikiwa tu, maana waweza ona unatumia nguvu nyingi zaidi na matokeo yasikupe furaha.
SOMA; KIMBIA MBIO ZAKO MWENYEWE
Hivyo ndugu yangu ingia kwenye mashindano na wewe, tamani kuwa bora zaidi ya jana, fanya utafiti ugundue huo mgodi ulivyo na mawe ya thamani sana, na ambayo yanasubiriwa mahali fulani na hayo yanachimbwa hapo kwako tu, hakuna mahali pengine yanapatikana, hivyo kazana ongeza kasi ya kuyatafuta ndugu yangu, na ukiyapata usikurupuke kuyachimba tu, tulia, shukuru kwamba umeyaona kisha jipange uone ni kwa namna gani utayachimba na kuyatumia kwa faida. Na ukifanya hayo uwe na uhakika wa kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa awali.
Mwandishi wa makala haya ni Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772