Moja ya changamoto kubwa ambazo zinawazuia watu wengi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni wao kujiwekea kikomo. Ndio, karibu kila mtu anapenda kuwa na maisha bora, lakini kuna wakati unafika mtu anajiwekea kikomo mwenyewe.
Na baada ya kujiwekea kikomo hiki hakuna tena jitihada kubwa zinazofanyika kujiondoa pale ambapo mtu anakuwa amefika.

Kwa mfano mtu unaanza biashara, mwanzoni unaweka juhudi kubwa sana, unatafuta wateja. Lakini baada ya muda fulani biashara inakuwa ni kama imefikia kilele, hakuna tena wateja wapya wanaoingia kwenye biashara yako. Kwa kifupi unakuwa umejiwekea kikomo cha kuongeza wateja kwenye biashara yako.
Au unaanza kazi, na mwanzoni unakuwa na juhudi kubwa sana, juhudi hizi zinakuwezesha kufanya vizuri na kukua sana kwenye kazi yako hiyo mwanzoni. Lakini baada ya muda ni kama unafika kileleni na hakuna tena ukuaji mkubwa kama wa mwanzo.
Hali hizi za kujiwekea kikomo zinaletwa na mambo mawili makubwa;
Jambo la kwanza ni kuridhika na kuona tayari umeshaweza kila kitu na hivyo kuacha kuweka juhudi kubwa.
Jambo la pili ni kuendelea kufanya kile ambacho umezoea kufanya, hata kama hakileti yale majibu ambayo umezoea kupata.
Elewa kwamba kuridhika ni adui mkubwa sana wa maendeleo. Lakini hii pia haimaanishi kila siku ujiumize, ila elewa kwamba kila siku kuna kitu kipya unachoweza kufanya na ukaboresha hali iliyopo.
Pia elewa kwamba kilichokufikisha hapa hakitakupeleka mbele. Kwa sababu njia fulani uliyokuwa unatumia zamani ndio imekufikisha hapo ulipo, haimaanishi ukiendelea kutumia njia hiyo utafika mbali zaidi. Mambo yanabadilika sana na wewe badilika pia.
Kuwa na maisha bora na yenye mafanikio, jua kila siku kuna kitu unaweza kuboresha na jua kwamba mabadiliko ni lazima.
TAMKO LA LEO;
Najua ya kwamba mimi mwenyewe nimekuwa adui yangu mkubwa wa kufikia mafanikio makubwa. Nimekuwa naridhika na kuona kwamba nimeshafika mbali sana na hivyo kuacha kuweka juhudi kama za mwanzo. Pia nimekuwa nafanya mambo kwa mazoea, kitu ambacho kinaninyima fursa ya kunufaika na mabadiliko yanayotokea kila siku. Kuanzia sasa nitakuwa naweka juhudi kila siku na pia nitabadilika kadiri mambo yanavyobadilika.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.