Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, naamini upo vizuri na unaendelea kufanyia kazi yale ambayo unajifunza ili kuboresha maisha yako. Nikupe hongera sana kwa hilo na nakupa moyo endelea kuweka juhudi, hakuna kinachoshindikana.
Na kama bado hujaanza kufanyia kazi, unasubiri nini? Unafikiri kuna wakati utakuwa bora kuliko sasa? Unakosea sana. Leo ndio siku yenyewe ya kuanza. Kama kuna kitu kizuri umejifunza anza kukifanyia kazi leo, na sio useme kesho, kesho ni mbali sana na huwa haifiki. Anza leo anza kidogo na baadae utaendelea kukua.

 Leo katika kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa tutajadili kuhusu ushindani wa kibiashara. Na ushindani tutakaozungumzia leo sio ule wa mtu kuenda kuanzisha biashara sehemu yenye ushindani, bali kuanzisha biashara sehemu ukiwa mwenyewe halafu watu wakaja na kuibua ushindani mkubwa.
Hii ni changamoto ambayo imewakuta watu wengi na kuwazuia kuweza kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara zao. Leo kupitia makala hii utajifunza mambo muhimu sana ya kuzingatia ili usiingie kwenye hali hii na kama umeshaingia basi uweze kuondoka na uendeshe biashara yenye mafanikio makubwa.
Kabla hatujaangalia ni nini unaweza kufanya, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na changamoto hii.

Changamoto yangu ni Kupungua Kwa Wateja Ambapo Kumesababishwa Na Kuibuka Kwa Biashara Nyingi Kama Yangu. Hapo Nifanyeje? M.K

Changamoto ya msomaji mwenzetu ni kuibuka kwa ushindani kwenye biashara yake na hivyo kupungua kwa wateja wake.
Kwa kuwa msomaji anasema wateja wamepungua kutokana na ushindani, ni hakika kwamba yeye ndiye alikuwa wa kwanza kuwepo kwenye biashara hiyo kabla hata ya hao washindani, na hivyo akawa na wateja wengi. Ila walipokuja wengine basi wateja wakaondoka na kwenda kwa wale wafanyabiashara wengine.
Mpaka hapo umeshapata picha ni kitu gani kimetokea?
Kama bado hujapata picha, basi ni hivi. Wateja uliokuwa nao mwanzo hawakuwa wanaridhika na jinsi ambavyo unafanya nao biashara. Ila kwa sababu hawakuwa na sehemu nyingine ya kununua, walilazimika kuendelea kufanya biashara na wewe. Ila walipokuja wafanyabiashara wengine, walienda kuwajaribu na kukuta kile ambacho walikosa kwako, kinapatikana kwa wafanyabiashara hao. Na hivyo wakabaki kule kule na hawawezi kuja tena kwako hata kama utalalamika kiasi gani. Ni lazima ubadilike ndio wateja hawa watakuja tena kwako.
Ulipoanza biashara na ukawa upo mwenyewe huenda ulijisahau ukawa unaendesha biashara yako kwa mazoea, hukuona sababu ya kuiboresha kwa sababu uliona wateja ni wengi na hakuna mtu mwingine anayefanya biashara kama yako. Ni rahisi sana kujisahau, ila kujisahau ndio kunaleta matatizo makubwa kama hayo uliyonayo sasa.
SOMA; Kama Una Tabia Hii Moja Una Uhakika wa Zaidi ya 90% Wa Kufanikiwa Kwenye Chochote Unachofanya.
Wakati umejisahau na kuendesha biashara kama kawaida, wenzako walikuwa wanakusoma na wakajua udhaifu wako uko wapi, hivyo walifanyia kazi udhaifu huo na sasa wamekunyang’anya wateja wako. Huenda mmoja kati ya wateja wako aliiona fursa hiyo ya kutoa huduma nzuri kuliko wewe na kuwa na uhakika wa kuvuna wateja wengi kutoka kwako.
Nimekukumbusha mambo hayo ili ujue ulifikaje hapo ulipo sasa, ili pia ujue mbinu za kukutoa hapo na pia kuzuia kuingia kwenye hali kama hiyo kwa siku za mbeleni.
Baada ya kujua umefikaje hapo ulipo, sasa tuangalie ni hatua gani unazoweza kuchukua ili kuondoka hapo ulipo.
1. Fanya tathmini ya biashara yako.
Mapema sana kaa chini na uitathmini biashara yako kwa kina. Jua ni biashara gani unayofanya, jua wateja wako ni wa aina gani, jua ni tatizo gani biashara yako inatatua kwa mteja na jua kama mteja anaridhika na huduma unazotoa. Katika tathmini hii unaweza kuwauliza wateja pia ni kitu gani wangependa kiboreshwe kwenye biashara yako ili iweze kuwahudumia vizuri. Pia katika kutathmini biashara yako jua ni kitu gani cha kipekee ambacho kinapatikana kwenye biashara yako na wateja wanakipenda au kinawasaidia sana.
2. Wajue washindani wako vizuri.
Kile walichokifanya washindani wako kwako, sasa na wewe inabidi ukifanye kwao. Jua ni kitu gani cha ziada ambacho wanatoa na wateja wanapenda sana kwenda kwao. Jua ni vitu gani wako bora kuliko wewe. Na pia jua ni vitu gani ambavyo wana udhaifu. Kwa kujua maeneo haya mawili muhimu, kutakuwezesha kufanya mabadiliko makubwa kwenye biashara yako na wateja wakarudi kwenye biashara yako.
3. Toa huduma bora kabisa kwa wateja wako.
Kama kuna kitu kimoja ambacho unatakiwa kukifanya kwenye biashara yako kila siku na kila wakati ni kutoa huduma bora. Watu wanapenda vitu vizuri, watu wanapenda kujaliwa, watu wanapenda kuonekana ni wa muhimu, watu wanapenda kupata thamani ambayo ni sawa sawa na fedha wanayotoa. Kama utafanikiwa kutoa huduma bora sana na zinazomridhisha mteja, mteja hana sababu ya kwenda kwa mtu mwingine. Akafanye nini na wakati anajua akija kwako anaondoka akiwa ameridhika kuliko akienda kwingine?
SOMA; Kama Unataka Kufanikiwa Achana Na Demokrasia Na Kuwa Dikteta.
4. Usijiingize kwenye ushindani ambao utakuumiza.
Pamoja na kwamba nimekuambia uwajue vizuri washindani wako, usije ukajiingiza kwenye ushindani ambao utakuumiza. Kwa mfano usijaribu kabisa kujiingiza kwenye ushindani wa bei, usishushe bei zaidi ya washindani wako ukiamini utawavutia wateja zaidi. Kwa kufanya hivyo na wao wanaweza kushusha zaidi yako wewe na ukajikuta kwenye hatari kubwa zaidi. Hivyo ni vyema kwako kuepuka ushindani wa aina hii na kuwekeza nguvu zako nyingi kwenye kutoa huduma bora kwa wateja wako.
5. Boresha biashara yako kila siku.
Kila siku, narudia tena, kila siku hakikisha unaiboresha biashara yako. Usithubutu hata siku moja kufanya jambo lolote kwenye biashara yako kwa mazoea. Chochote unachofanya jiulize je kinamsaidia vipi mteja kutatua tatizo lake? Jiulize kinaiwezeshaje biashara yako kufikia wateja wengi zaidi? Kama hakina faida achana nacho mara moja, huna muda wa kupoteza kufanya vitu ambavyo havisaidii biashara yako. Na ukijisahau tena ukarudi kufanya vitu kwa mazoea, utatoa nafasi ya watu kukusoma na kutumia udhaifu wako kuchukua wateja wako.
Biashara za sasa sio za kuendesha tena kwa mazoea. Wateja hawatanunua kwako kwa sababu wewe ndio mwanzilishi wa biashara hiyo. Bali wateja watanunua kwako kwa sababu wanapata huduma bora kabisa ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote. Na wewe unaweza kutoa huduma hizi bora kama utaijali biashara yako.
Je utafanya hivyo? Kama biashara yako ndio inakutegemea ili na wewe uweze kuitegemea? Naamini unaweza. Nakutakia kila la kheri na karibu kama utakuwa na changamoto yoyote ya kibiashara.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.