Tukitaka kupima ukuu wako, hatuna haja ya kutumia nguvu kubwa, hatuna haja ya kujua umri ulionao na wala hatuna haja ya kujua historia yako umetokea wapi mpaka ulipo sasa.
Ni rahisi sana kupima ukuu wa mtu kama utapata muda mchache wa kuwa naye. Kwa muda huu utaweza kujua vitu viwili muhimu vitakavyokupa kiashiria huyu mtu ni wa aina gani. Na kama unataka kujipima ukuu wako mwenyewe basi kuna njia mbili ambazo unaweza kutumia kujipimia.

JE UPO TAYARI KUPOKEA MAJUKUMU KIASI GANI?
JE UPO TAYARI KUPOKEA MAJUKUMU KIASI GANI?

Njia ya kwanza ni majukumu aliyonayo mtu. Nenda sehemu yoyote na yule mwenye majukumu mengi na makubwa ndiye mkuu. Wakati mwingine hata kama majukumu hayo sio makubwa sana, ila ni mengi ukilinganisha na wengine wanaomzunguka basi jua mtu huyo ni mkuu.
Watu wengi hukimbia majukumu, watu wengi hukwepa majukumu, ukiona mtu anayekubali majukumu, basi jua huyo ni mkuu sana. Na majukumu mengi tunayozungumzia hapa sio yale ya kujisemea, unajua mimi nina mambo mengi sana, wakati unayatumia kama sababu tu. Bali ni yale majukumu ambayo tunamwona mtu kweli anayafanya na wala hayalalamikii.

SOMA;  Nenda Hatua Ya Ziada…
Njia ya pili ni mambo yanayompa hofu. Kaa na mtu au jichunguze wewe mwenyewe ni vitu gani ambavyo unavihofia. Kama vitu vidogo vidogo vinakupa hofu kubwa basi jua ya kwamba wewe sio mkuu. Au unapomwona mtu ambaye vitu vidogo vodogo vinamchanganya sana unajua huyo hayupo kwenye ukuu.
Kama vitu vinavyompa mtu hofu ni vitu vikubwa, vitu ambavyo vinaonekana haviwezekani kwa watu wa kawaida, lakini mtu ndio anavifikiria basi huyo ni mkuu.
Hatupimi ukuu huu ili kuona nani ni mkuu kuliko wengine, bali tunapima ukuu huu ili kujua kama tutafikia mafanikio makubwa tunayotazamia. Na kama unataka mafanikio makubwa, anza kukubali majukumu makubwa na yafanye bila ya kulalamika na pia achana na kuhofia vitu vidogo, fikiria vitu vikubwa ambavyo watu wengine hawathubutu hata kufikiria na hivi ndio vikusukume wewe.

TAMKO LA LEO;
Najua ukuu wangu ndio utakaopima mafanikio yangu. Na ukuu wangu nitaweza kuupima kwa majukumu niliyonayo na mambo yanayonipa hofu. Kuanzia sasa nitayakubali majukumu makubwa na kuyafanyia kazi bila ya kulalamika. Kwa sababu najua ninapofanyia kazi majukumu makubwa najiweka kwenye nafasi ya kukua zaidi. Na pia nitaacha kuhofia vitu vidogo vidogo na badala yake nitafikiria vitu vikubwa ambavyo kwa wengine vinaonekana haviwezekani kabisa. Najua hakuna kitakachonishinda kwa sababu nimeshaamua.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.