Usiruhusu Visingizio Vikushinde, Visingizio Vipo Kila Siku, Ila Muda Haukusubiri.

Ni kweli kuwa kuna wakati katika maisha unaweza kuwa na mambo mengi sana yanayokufanya ushindwe kuendelea na mipango yako mingine uliyoipanga. Inaweza kuwa unafanya kitu ambacho kweli kinaonekana ni cha maana na una kila sababu ya kuendelea kukifanya na ukaona una haki zote za kuacha kile kingine kisubiri. Watu wengi wameshindwa kukamilisha mipango mingi wanayoipanga kwa kuwa tu wameruhusu kuharibu ratiba zao, wamekubali yale mambo mengine yanayojitokeza yawazuia kukamilisha ratiba zao walizokwisha anza kuzitekeleza.

MUDA WAKO NDIO HAZINA YAKO KUU, ULINDE SANA.

 
Wengi wetu mara nyingi ikitokea kuwa tumeshindwa kufanya kitu fulani basi ni wepesi wa kutafuta sababu na kusema ooh unajua nilikuwa na kazi/shughuli nyingi sana za kufanya ndio maana nikashindwa kufanya hili, lakini ndugu yangu ni vyema tukielewa kuwa hata kama una shughuli nyingi kiasi gani lazima uwe na ratiba na mpango kazi , kuweza kujua ni yepi unatakiwa kuyafanya , hivyo hata inapotokea kuwa una vitu vingi vya kufanya basi uhakikishe unavifanya vyote kwa ufanisi, inawezekana tu ukiamua na kuwa na nia ya dhati ya kufanya hilo, na pia kama kweli unapenda hicho unachofanya hautakubali kuona unaacha kufanya hata kama itagharimu muda zaidi, utakuwa tayari kujitoa kuweza kufanya hiyo kazi/shughuli na ukiikamilisha nawe utajisikia vizuri na kufurahi pia.
SOMA; Nikipata Muda Nitafanya.
Wengi wetu ni wepesi wa kutafuta visingizio, ndugu yangu tambua visingizio havikusaidii na havitakusaidia kamwe, visingizio havisaidii kutimiza ule mpango kazi wako , vinaweza onekana ni vya maana lakini vinakupoteza , vinakuchelewesha na vinaweza kukuzuia kufika pale unatakiwa kufika, maana ukijipa visingizio utaona una kila sababu ya kutokufanya na kama ikitokea kwa bahari mbaya, ndiyo namaanisha bahati mbaya umekutana na mtu anayekubaliana na visingizio vyako na akakutia moyo kuwa kweli umebanwa sana hivyo huwezi kufanya hayo basi ujue hali yako itazidi kuwa mbaya zaidi. Hakikisha unatafuta muda wa kutimiza kila ulilolipanga, muda upo ndugu yangu, hebu angalia masaa yako 24 unayatumiaje? Unataka kuniambia muda wote unafanya ya maana? Ni masaa mangapi unayatumia kwa kufanya yasiyo na faida kwako? Fikiria ule muda unazurura kwenye mitandao ya kijamii na kujihusisha na mijadala isiyo na tija kwako na jamii, fikiria hata ule muda unautumia kwa kubishana na watu tu katika mambo yasiyo ya muhimu sana kwako kwa wakati huu, kuna ule muda unapiga tu simu kwa watu na kupiga soga tu zisizo na ulazima ndugu yangu, au pengine una muda wa kulala zaidi hata ya masaa 8 kwa siku, kuna mwingine anahakikisha kila tamthilia haimpiti, anafuatilia mwanzo mpaka mwisho na anakumbuka kila kitu kilichotokea, akitakiwa kusimulia basi anasimulia kwa umahiri kabisa, lakini huyu huyu atakuambia ooh unajua nilishindwa kufanya hii shughuli kwa kuwa sina nafasi kabisa, mambo ni mengi sana, ni kweli hayo mambo uliyo nayo ni mengi, lakini je yana maana gani kwako? Yanakuongezea maana ya kuwepo hapa duniani? Au yanakufanya uzidi kuwa msindikizaji wa wengine, mshangiliaji wa wengine wanaoishi kwenye kusudi waliloumbiwa? Hauna muda wewe?
SOMA; Hatua Moja Ndogo Kila Siku Ndio Kitu Pekee Unahitaji.
Masaa 24 yanakutosha sana kufanya kila ulichopanga kufanya kama kweli ndicho ulichoumbiwa ufanye, na una nia ya dhati ya kukikamilisha, vikwazo haviwezi kupata nafasi, vikwazo haviwezi kuishinda ile nia ya ndani kabisa ya wewe kupanga hilo, hivyo ndugu yangu acha kujitetea, kaa mbali na wasiokuambia ukweli wanaofurahia huko kujifariji kwako kuwa ooh niko na mambo mengi siwezi hili hivyo labda tuahirishe, tufanye wakati mwingine n.k Tafuta mtu ambaye atakuambia ukweli, ukizembea anakushtua na kutokukubaliana na sababu zako hata kama waona zina maana, kujitetea kumefanya wengi wasifike kule wanatakiwa kufika kwa wakati muafaka.
Makala hii imeandikwa na Beatrice Mwaijengo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: