Moja ya njia unazotumia kupoteza muda na rasilimali nyingine kwenye biashara yako, ni kujaribu kumuuzia kila mtu kile unachouza. Ni vigumu sana kila mtu kuona thamani ya ile biashara ambayo unafanya.
Hivyo katika harakati zako za kutafuta wateja utakutana na watu wengi. Kuna ambao wataiona thamani na kuchukua hatua haraka, kulipia na kuipata. Na kuna ambao hawataiona thamani na hivyo hata ukiwashawishi vipi bado hawatakuwa tayari kulipia.
Lengo lako wewe kama mfanyabiashara ni kuhakikisha unawatafuta wale ambao wanaijua thamani ya biashara unayofanya ili iwe rahisi kwako kuwauzia. Pia kuwa na njia ambayo utawajua haraka wale ambao hawaioni thamani na kupunguza muda ambao unatumia nao.
Muda wako kwenye biashara ni mchache, huwezi kuutumia sawa kwa kila mteja. Ndio maana ni muhimu kuweza kuwachuja wateja wako na kujua ni wapi ambao kweli wapo tayari kununua na ni wapi ambao wanapita tu ila wamejisikia kuuliza.
Pamoja na yote, usimfanye mteja ajisikie vibaya, hata kama haoni thamani. Mawasiliano yako mazuri na yeye yanaweza kupelekea yeye kukuletea mteja ambaye anaiona thamani unayotoa.
Pia usiumie pale ambapo unakazana kumweleza mteja faida za kile ambacho unataka kumuuzia na mwisho wa siku anakuambia hanunui. Hajakukataa wewe, hajakataa biashara yako ila ni kwamba hajaona thamani kwenye kile kitu ambacho unataka kumuuzia.
Unaweza kupata wapi wateja ambao wanaijua thamani unayotoa?
- Uza zaidi kwa wateja ambao tayari unao kwenye biashara yako. Hawa tayari wanakuamini na unaweza kufanya nao biashara zaidi.
- Washawishi wateja ulionao sasa wakuletee wateja wengine zaidi. Hawa wanajua watu ambao wataiona thamani kwenye biashara yako na kuifanyia kazi.
- Tangaza kwa kulenga wateja ambao wataona thamani kwenye biashara yako. Usiandae matangazo kwa kila mtu, bali lenga wale watakaoiona thamani kwenye kile unachotaka kuwauzia.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa.
Kama una swali au changamoto yoyote ya kibiashara au kijasiriamali basi iweke kwenye FORUM YETU YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI. Bonyeza hayo maandishi kuuliza swali lako na utapata michango kutoka kwa wengine. Karibu sana.
Jiunge na COACHING/MENTORSHIP PROGRAM ambapo utapata muongozo wa hatua kwa hatua mpaka ufikie mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya. Bonyeza haya maandishi kupata maelekezo ya programu hii.