Kama ambavyo tumekuwa tunakubaliana mara nyingi, maisha ni kichagua.
Chochote kinachotokea kwenye maisha yako, basi umechagua mwenyewe, iwe ni sasa au siku zilizopita.

image
MAISHA NI RAHISI SANA, UKIJUMLISHA UNAKWENDA JUU, UKITOA UNAKWENDA CHINI. JE WEWE UNACHAGUA NINI?

Sasa mambo yote unayoweza kuchagua kwenye maisha yamegawanyika kwenye makundi mawili.
Makundi haya ni kujumlisha(chanya, +) na kutoa(hasi-).
Ukifanya jambo lolote ambalo ni chanya unajumlisha(kuongeza) kitu kwenye maisha yako.
Kwa mfano ukimwongelea mtu vizuri, ukimtia mtu moyo, ukimwambia mtu maneno ya kumjenga, unajumlisha vitu vingi. Unaongeza uhusiano na watu, utajisikia mwenye furaha, utatoa mchango wako kwa wengine na kadhalika.
Ukifanya jambo lolote ambalo ni hasi unatoa(unapunguza) kitu kwenye maisha yako.
Kwa mfano ukimwongelea mtu vibaya, ukimkatisha tamaa, ukimwambia maneno ya kubomoa, utatoa vitu vingi. Utapunguza mahusiano yako, utajiona wewe ni mbomoaji na utakosa furaha.
Hata kwenye maisha yako tu, unapofikiria mawazo hasi kwenye akili yako unapunguza vitu vingi kwenye maisha yako.
Na unapofikiria mawazo chanya kwenye maisha yako unaongeza vitu vingi.
Je unachagua kufanya nini leo kwenye maisha yako? Utajumlisha au utatoa? Maisha ni yako na uamuzi ni wako.
Mimi kama kocha wako nakusihi sana ujumlishe na epuka kabisa kutoa.

TAMKO LA LEO;
Nimejua ya kwamba mimi mwenyewe ndio najenga au kubomoa maisha yangu. Mimi ndio naongeza vitu kwenye maisha yangu kwa kuwa na mawazo chanya na kuwasemea wengine kwa mtizamo chanya. Na mimi piq ndio nimekuwa nabomoa maisha yangu kwa kuwa na mawazo hasi kwangu na kwa wanaonizunguka. Kuanzia sasa nimeamua kuwa na mawazo chanya tu ili niendelee kuwa na maisha ya mafanikio.

Asante sana kwa kusoma ukurasa wa leo, naamini utaondoka na kitu cha tofauti, kifanyie kazi.
Tukutane kwenye ukurasa wa 235 kesho.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.