Habari za wakati huu rafiki?
Naamini uko vizuri sana, na najua unafanyia kazi yale ambayo unajifunza ili maisha yako yaweze kuwa bora sana. Hongera sana kwa hilo, na ninakusihi sana usifike mahali na kuona kwamba haiwezekani halafu ukarudi kwenye yale maisha ya zamani. Kama umechagua maisha mapya hakikisha unaendelea nayo na siku sio nyingi utaona matunda mazuri.
Katika mazungumzo yetu ya leo nataka nikushirikishe habari njema sana ya kwamba mwezi huu wa tisa nitaanza kujifunza lugha ya Kilatini. Lugha ya kilatini? Ndio nitaanza kujifunza lugha ya kilatini na muda sio mrefu nitakupa sababu kwa nini nitajifunza lugha hiyo.
Mwezi huu wa tisa tunaanza program yetu ya GAME CHANGERS ambapo ni kundi dogo la watu ambao wana vitu vikubwa wanavyotaka kufanya lakini wamekuwa hawapati muda wa kuvifanya au wamekuwa wakiahirisha na kuona kuna siku watapata muda mzuri wa kuweza kuvifanya. Lakini kama ambavyo wote tunajua tabia ya muda, hakuna siku ambayo utakuwa na muda zaidi. (kama unafikiri kuna siku utapata muda w akufanya kitu fulani, unajidanganya, chochote kikubwa unachotaka kuanza kujifunza, anza sasa)
Hivyo basi kwenye program hii ya GAME CHANGERS kutazaliwa vitu vingi sana vikubwa ambavyo vitawasaidia wale wanaovifanya na hata jamii kwa ujumla. Hivyo pia huu utakuwa muda mzuri kwangu kufanya mambo makubwa ambayo nimekuwa nasema nitafanya lakini sifanyi. Kwenye GAME CHANGERS kunakuwa na mfumo mzuri sana ambao unakubana wewe kufanya kile ambacho umepanga kufanya.
Mambo muhimu kuhusu lugha ya kilatini.
Kwanza kabisa lugha ya kilatini ni lugha ambayo imekufa (dead language), ni lugha ambayo haitumiki tena kwa mawasiliano, ukitoa vatican. Ni lugha ambayo haipati tena misamiati mipya.
Lugha hii ilitumika kwenye utawala wa Roma, nafikiri baada ya roma kuanguka ndipo mwisho wa lugha hii. Lakini pia lugha hii imetumika sana kwenye misingi ya sayansi, dini na hata falsafa. Maandiko mengi ya kisayansi na falsafa yaliandikwa kwa lugha hii ya kilatini.
Kwa nini mimi najifunza kilatini.
Pamoja na yote hayo kwamba hii ni lugha iliyokufa na haitumiki tena, kwa nini nipoteze muda wangu kuisoma, kwa nini nisifanye mambo mengine muhimu? Au nataka kwenda kuongea na papa? (ha ha haa, natania). Hapana nina sababu za msingi sana, na hapa nitakushirikisha baadhi.
- Kujifunza lugha ya ziada.
Sababu mojawapo kwa nini najifunza kilatini ni kwa sababu nataka kujifunza lugha ya ziada. Mpaka sasa naweza kuongea, kuandika na kuelewa kwa ufasaha lugha tatu, kiswahili, kichaga na kiingereza. Nahitaji kuongeza lugha nyingine kadhaa, sijapanga hasa ni ngapi, lakini nitaendelea kujifunza lugha zenye soko kubwa duniani. Kama kihispania, kifaransa, kijerumani na hata kichina. Sasa kama lengo ni kujifunza lugha nyingine kwa nini usianze na hizo ambazo zinatumika na badala yake unaanza na lugha ngumu na ambayo haitumiki? Jibu la swali hili soma namba mbili hapo chini.
- Kilatini ni msingi wa lugha nyingi.
Sehemu kubwa ya lugha hizi kubwa imetokana na lugha ya kilatini. Inasemekana asilimia 60 ya maneno yote ya kiingereza yametoholewa moja kwa moja kutoka kwenye lugha ya kilatini. Hivyo kujifunza kilatini kutaimarisha kiingereza changu na pia lugha nyingine nitakazojifunza.
Kitu kingine muhimu sana ni kwamba misingi ya kujifunza lugha mpya ni ile ile, hivyo nikishajifunza kilatini ni rahisi kuendelea kujifunza lugha nyingine.
- Nataka kitu kipya cha kufanya, cha kuniondoa kwenye woga.
Mara nyingi sana huwa natafuta kitu kipya cha kufanya, ambacho kitaniondoa kwenye hali ya woga kwamba labda hiki siwezi. Kwa kujifunza kilatini nitakuwa na kitu kipya kabisa cha kufanya na hii itanifanya niumize kichwa zaidi. Kwa jinsi ninavyojijua mwenyewe, nikiwa na kitu kipya cha kufanya hamasa yangu huwa inakuwa kubwa sana kuliko ninapofanya kitu ambacho nimezoea kufanya.
Pia napenda kufanya kitu ambacho watu wengine wanaona hakiwezekani au ni ujinga au vyovyote vile ambavyo wanafikiria. Mara nyingi sana vitu vya aina hii huwa vinakuwa na thamani kubwa sana kwangu kwa baadae.
- Kujifunza ustaarabu wa kale.
Kama nilivyokushirikisha hapo juu, kilatini ni moja ya lugha ambayo ilitumika kujenga ustaarabu wa kale. Lugha nyingine ni kigiriki. Hizi taaluma zote ambazo tunasoma sasa, zimetokana na ustaarabu huu wa kale, udaktari, falsafa, dini, siasa na mengine mengi, yote yametoka kwenye ustaarabu huu wa kale. Kama umesoma sekondari na kama ulisoma somo la biolojia utakumbuka kwenye somo la classification, majina ya viumbe wote yanatamkwa kwa kilatini kwa mfano binadamu tunaitwa Homo sapiens. Kuna mmea uligunduliwa kilimanjaro, na kwa kuwa majina ya kisayansi lazima yawe kwa kilatini au yatamkwe kilatini basi mmea ule uliitwa Cuscuta kilimanjari
Sasa kikubwa hapa ni kwamba kadiri siku zinavyokwenda ustaarabu huu wa kale unabadilishwa kutokana na matakwa ya watu wenyewe. Kwa kuwa mimi napenda kujifunza, nitafurahi sana kama nitaweza kujifunza ustaarabu huu kwa lugha ile ile ambayo uliandikwa.
Naamini zaidi kwenye ustaarabu ulioweza kudumu miaka mingi, chochote kinachodumu zaidi ya miaka 500 ni kitu kizuri sana.
- Napenda kujifunza zaidi falsafa.
Kujifunza falsafa unajifunza kupitia wanafalsafa ambao walifanya vizuri. Wengi wa wanafalsafa hawa walikuwa wakitumia lugha ya kilatini na hivyo maandiko yao bora kabisa yapo kwa lugha ya kilatini.
- Kuongeza uwezo wa kufikiri.
Hili nimejifunza wakati nafuatilia lugha hii. Wanasema ambao wanajifunza, kuongea au kuandika kilatini wanakuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kuchambua mambo. Naamini uwezo wangu utaongezeka maradufu pia.
- Sijawahi kujifunza kitu kisiwe na manufaa kwangu.
Katika historia yangu ya kujifunza vitu mwenyewe, ndio nimejifunza vitu vingi sana na vyote vimekuwa na manufaa makubwa. Nimeweza kutumia maarifa niliyopata kwenye kujifunza vitu mbalimbali kuweza kutatua matatizo ya wengine na hili limekuwa na malipo mazuri sana kifedha, na hata kuridhika pia.
Naamini kwenye kilatini itakuwa hivyo pia, nitapata fursa nyingi sana akupitia lugha hii. Labda baadae nitaweza kutafsiri maandiko adimu kutoka kilatini kuja kiswahili. Labda mtu atataka nimfundishe kilatini. Labda nitapata nafasi ya kumwandikia papa Francis barua ya kilatini kumshukuru kwa hamasa aliyoingiza kwangu (kama sikuwahi kukuambia, papa Francis ni mtu anayenihamasisha sana, nitaliandika hili kwa undani siku nyingine).
Kwa vyovyote vile nitakuwa na fursa nyingi kwa kujua kilatini kuliko nilizonazo sasa.
- Akili ya binadamu ina uwezo mkubwa sana, nataka kuutumia zaidi wa kwangu.
Hili liko wazi kwamba kila mmoja wetu ana uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yake. Lakini ni wachache sana wanaoweza kutumia uwezo huu. Wengi wanauacha haujatumika na wanakufa nao. Sasa mimi najaribu kujiweka kwenye mazingira kwamba nikifa nife mtupu, yaani kama kuna kitu naweza kufanya kwenye maisha yangu basi nikifanye, tena kwa ubora wa hali ya juu sana. Wacha niutumie uwezo huu.
Naamini safari yangu ya kujifunza kilatini itakuwa nzuri sana na nitaendelea kukushirikisha kadiri ninavyojifunza.
Kama kuna mtu ambaye anajua lugha hii ya kilatini naomba awe mentor wangu kwa kipindi hiki, ili tuwe tunawasiliana kwa kutumia lugha hiyo, hii itanisukuma sana kujifunza kwa haraka.
Umehamasika na wewe unataka ujifunze kilatini? Jifunze zaidi faida za kilatini halafu angalia ni jinsi gani unaweza kuzitumia kwenye maisha yako na kazi zako.
Ningependa kuambatana na mtu yeyote ambaye angependa kujifunza lugha hii, ila njia ninayotumia kujifunza mimi itaweza kuhatarisha maisha ya mtu. Huwa najifunza kwa nguvu sana halafu huwa siweki sababu, sasa tukianza na mtu hapa leo aje na sababu hii, kesho ile kesho kutwa nyingine atanishusha morali wangu wa kujifunza. Hivyo naomba niweke nguvu na akili zangu kwenye lugha hii halafu matunda yatakapokuwa mazuri nitaweza kuendesha darasa la watakaopenda kujifunza lugha hii.
Ufanye nini?
Chagua kitu kimoja kidogo saa cha kufanya, ambacho hujawahi kufanya kwenye maisha yako, hata kama ni kidogo kiasi gani, na hakikisha unakifanya kila siku. Anza na chochote, labda ni kusoma kitabu kila siku, na fanya hivyo, usiruke siku hata moja, hata kama unaumwa, chukua kitabu soma kurasa chache. Chochote kile ambacho utachagua kufanya, ondoa kabisa nafasi ya kujipa sababu kwa nini huwezi au kwa nini uache. Acha akili yako iwe huru na ona jinsi ambavyo maisha yako yatabadilika.
MAKALA ZA KUSOMA.
Soma makala hizi nzuri, ujifunze na kuhamasika.
- Soma mambo haya 20nyatakayokuwezesha kuwahamasisha wanaokuzunguka; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha 100 Ways To Motivate Others(Njia 100 Za Kuwahamasisha Wengine)
- Upangaji wa bei ni eneo nyeti sana kwenye biashara yako, hapa kuna mambo manne muhimu ya kuzingatia; Mambo Manne (4) ya Kufikiria Unapopanga Bei ya Huduma au Bidhaa Yoyote Ile
- Chochote ambacho kinatokea kwenye maisha yako sasa, ulishakiona siku za nyuma. Kubadili maisha yako yajayo anza kubadili kile unachoona. Soma kujua zaidi; Unaona Nini?
- Umeajiriwa na ungependa pia uwe na biashara? Je mtaji na muda ni tatizo? Soma hapa kuna biashara tano zinazokufaa sana; Biashara Tano(5) Unazoweza Kuanza Kufanya Wakati Bado Umeajiriwa, Na Kwa Mtaji Kidogo.
- Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo utapata nafasi ya kusoma makala nyingi nzuri na kuwa kwenye kundi la wasap ambapo utajifunza na kuhamasika kwa mambo mbalimbali. Bonyeza hapa kupata maelekezo na kujiunga.
Naamini kuna kitu kipya umejifunza leo rafiki, kifanyie kazi haraka sana, usisubiri upate muda, muda wenyewe ndio huu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz